Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Dar es Salaam

LICHA ya Serikali kuendelea kuhamasisha matumizi ya gesi asilia kwenye vyombo vya moto kama mbadala wa mafuta ya petroli na dizeli, matumizi ya nishati hiyo jijini Dar es Salaam bado yako chini, huku gharama za kufunga mifumo ya Compressed Natural Gas (CNG) zikitajwa kuwa miongoni mwa vikwazo vikubwa.

Imeelezwa kuwa, kwa sasa, magari yanayotumia CNG jijini Dar es Salaam ni takribani asilimia 0.7 pekee ya magari yote yaliyopo, hali inayoonyesha kuwa matumizi ya nishati hiyo bado hayajafikia hata asilimia moja.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Msimamizi Mkuu wa Karakana ya Ufungaji wa Mifumo ya Gesi Asilia katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Mhandisi Gerutu Bosinge, amesema gharama za kubadilisha mfumo wa gari kutoka matumizi ya petroli kwenda CNG ni miongoni mwa sababu zinazowafanya baadhi ya wamiliki wa magari kushindwa kuhamia kwenye nishati hiyo.

Amesema kwa baadhi ya magari, gharama za kufunga mfumo wa CNG huanzia kati ya Sh2.2 milioni na Sh2.3 milioni, kiasi ambacho si rahisi kumudu kwa baadhi ya wamiliki wa magari na bajaji.

“Bado hatujafikia hata asilimia moja ya magari ya Dar es Salaam yanayotumia gesi asilia. Tuko kwenye takribani asilimia 0.7. Ukiangalia idadi ya magari yaliyopo na kulinganisha na yale yanayotumia gesi, utaona bado ni machache sana,” amesema Mhandisi Bosinge.

Hata hivyo, amesema pamoja na idadi ndogo ya watumiaji, sekta ya CNG imeendelea kukua, hususan katika ongezeko la wataalamu na karakana zinazotoa huduma za kufunga mifumo hiyo.

Amesema mwaka 2008 kulikuwa na karakana moja pekee ya kufunga mifumo ya CNG jijini Dar es Salaam, lakini kwa sasa idadi hiyo imeongezeka na kufikia zaidi ya karakana 16 hadi 17.

“Mwaka 2008 tulikuwa na karakana moja tu hapa Dar es Salaam, lakini leo tunazungumzia zaidi ya karakana 16 au 17. Wataalamu wengi wanaofanya kazi katika sekta hii wamepata mafunzo yao ndani ya karakana yetu ya DIT,” amesema.

Kwa mujibu wa Mhandisi Bosinge, zaidi ya vijana 200 wamepata mafunzo katika karakana hiyo, huku baadhi yao wakiajiriwa katika sekta ya CNG na wengine wakianzisha karakana zao.

Amesema wataalamu hao pia wamekuwa wakiwafundisha vijana wengine, hali inayochangia kuongezeka kwa wataalamu wanaotoa huduma mbalimbali zinazohusiana na mifumo ya gesi asilia kwenye magari.

“Ukimuandaa kijana mmoja na akapata mafunzo pamoja na cheti, anaweza kwenda kuajiriwa au hata kufungua karakana yake na kuwafundisha vijana wengine. Kwa hiyo, ukiangalia idadi ya vijana walioongezeka na wanaofanya kazi hizi kwa sasa, ni karibu 1,000 na kuendelea,” amesema.

Aidha, amesema matumizi ya CNG yanaendelea kuenea katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo baadhi ya mikoa, ikiwemo Dodoma na Mtwara, imeanza kuwa na miundombinu inayowezesha matumizi ya nishati hiyo..

Amesema pia kuna mipango ya kuongeza vituo vya kujaza CNG katika maeneo mbalimbali nchini, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa watumiaji.

Pamoja na changamoto ya gharama za ufungaji, Mhandisi Bosinge amesema wananchi wengi wanaendelea kuvutiwa na matumizi ya CNG kutokana na gharama ndogo za uendeshaji ikilinganishwa na petroli.

Akitoa mfano wa gari dogo aina ya IST, amesema gesi yenye thamani ya takribani Sh17,000 inaweza kuliwezesha gari hilo kusafiri umbali wa zaidi ya kilomita 200, ingawa kiwango cha matumizi hutofautiana kulingana na aina ya gari, injini na mazingira ya uendeshaji.

“Unaweza kutumia kiasi hicho cha fedha kusafiri umbali mrefu, tofauti na petroli ambapo Sh17,000 inaweza kununua kiasi kidogo cha mafuta ambacho hakiwezi kukufikisha umbali huo huo,” amesema.

Kwa upande wake, Fundi Mkuu wa CNG katika DIT, Agapitus Gurti, amesema kabla ya kuanza kufunga mfumo wa CNG, gari la mteja hupitia ukaguzi wa kina ili kubaini hali yake kiufundi.

Amesema ukaguzi huo huhusisha injini, mfumo wa umeme pamoja na mifumo mingine muhimu ili kuhakikisha gari linaweza kutumia mfumo wa CNG kwa usalama na ufanisi.

“Mchakato wa kufunga mfumo wa CNG kwenye magari huanza kwa ukaguzi wa kina ili kubaini kama gari liko katika hali nzuri kiufundi. Baada ya hapo tunaangalia aina ya gari na mfumo unaohitajika,” amesema.

Hata hivyo, amesema baadhi ya wateja hushindwa kuendelea na mchakato wa ufungaji baada ya kuelezwa gharama zinazohitajika.

Amesema gharama za kufunga mfumo wa CNG hutofautiana kulingana na aina ya gari, idadi ya silinda za injini na ubora wa vifaa vinavyotumika.

“Kuna aina mbalimbali za mifumo ya kufunga CNG na bei yake hutegemea aina ya gari pamoja na ubora wa vifaa vinavyotumika katika ufungaji. Kwa ujumla, sisi tunafunga vifaa vya ubora wa juu,” amesema.

Ameongeza kuwa magari yenye injini za silinda sita na nane huhitaji mifumo yenye gharama kubwa zaidi, ambapo gharama za ufungaji zinaweza kuanzia Sh3 milioni na kuendelea, kutegemeana na aina ya gari na mfumo unaohitajika.
Kwa ujumla, ukuaji wa sekta ya CNG unaendelea kufungua fursa za ajira na mafunzo kwa vijana katika kazi za kufunga, kutengeneza na kuhudumia mifumo ya gesi asilia kwenye magari.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa kuna haja ya kuendelea kutafuta njia za kupunguza gharama za ufungaji wa mifumo hiyo pamoja na kuongeza miundombinu ya vituo vya kujaza gesi, ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kuhamia kwenye matumizi ya CNG.

Kadri idadi ya magari yanayotumia gesi asilia inavyoongezeka, ndivyo mahitaji ya wataalamu wenye ujuzi wa kufunga na kuhudumia mifumo hiyo

yatakavyoendelea kuongezeka, hatua inayotarajiwa pia kuchangia katika upatikanaji wa ajira kwa vijana.