Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma
TAASISI ya Uhasibu Tanzania (TIA) imefikisha wanafunzi 37,397 katika mwaka wa masomo 2025/26, kutoka 24,494 mwaka 2021/22, sawa na ongezeko la asilimia 52.7, huku Serikali ikiwekeza Sh67.9 bilioni katika kuboresha miundombinu ya taasisi hiyo katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Prof. William Amos Pallangyo, ameeleza hayo Wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Septemba 07, 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO, kuhusu utekelezaji wa Taasisi hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27.
Amesema ongezeko hilo limekwenda sambamba na kupanuka kwa taasisi hiyo kutoka kampasi sita mwaka 2021/22 hadi nane mwaka 2025/26, baada ya kuanzishwa kwa kampasi za Tanga na Zanzibar.
Aidha, idadi ya programu za masomo imeongezeka kutoka 49 hadi 54, huku jumla ya wahitimu 62,680 wakihitimu TIA katika kipindi hicho. Wanafunzi 19,342 katika kampasi saba pia wamenufaika na mikopo ya elimu ya juu.
Katika kuimarisha ubora wa elimu, ameeleza Serikali imeiwezesha TIA kupata maprofesa tisa na kufadhili watumishi 78 kusoma Shahada ya Uzamivu (PhD), ambapo 48 tayari wamehitimu na 30 wanaendelea na masomo.
“Hatua hiyo imeongeza uwezo wa taasisi katika ufundishaji, utafiti na ubunifu, pamoja na kuwezesha kuanzishwa kwa programu za Shahada ya Uzamili katika kampasi za Zanzibar, Mbeya, Singida na Mwanza”amesema.
Ameeleza kuwa kati ya Sh67.9 bilioni zilizowekezwa katika miundombinu ya TIA, Sh27.8 bilioni zimetolewa kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), huku Sh22.6 bilioni zikielekezwa katika ujenzi wa miundombinu ya Singida na Mwanza.
Pia amesema uwekezaji huo umeongeza uwezo wa taasisi kuhudumia wanafunzi wengi zaidi na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, huku pia ukichochea ajira na shughuli za biashara katika maeneo yanayozunguka kampasi.
Ameeleza kuwa TIA pia imeongeza mkazo katika kuwajengea wanafunzi ujuzi unaowawezesha kuajiriwa, kujiajiri na kuanzisha biashara.
“Zaidi ya wanafunzi 5,000 wamefikiwa kupitia warsha za ujasiriamali, ubunifu, ajira na fursa za kimataifa, huku zaidi ya 500 wakipata mafunzo maalumu ya ujasiriamali na takribani 100 wakisaidiwa kuanzisha biashara ndogo,”amefafanua.
Ameeleza kuwa Katika Shindano la Ubunifu la mwaka 2025, mawazo 376 yaliwasilishwa, washindi 57 wakapatikana na mawazo 17 kufikia hatua ya kuanza kuwa biashara.
Ametaja Miongoni mwa ubunifu huo ni SmartGlove ya Damian Msonge, inayolenga kutafsiri lugha ya alama kuwa maneno yanayosikika, pamoja na Cotton Track Management System ya Pascal Sabuni inayolenga kuongeza uwazi na kupunguza upotevu katika mnyororo wa thamani wa pamba.
Ameongeza kuwa Mhitimu Nicolaus Carol Mboya naye ameigeuza kazi yake kuwa kampuni ya STEAMORA, inayotoa mafunzo ya teknolojia kwa watoto na vijana, ambayo tayari imewafikia zaidi ya wanafunzi 600, ina watumishi wanane na imezalisha zaidi ya Sh15 milioni.
Katika utafiti na matumizi ya TEHAMA, Mkurugenzi huyo amesema TIA imefanya tafiti nane na kuchapisha machapisho 108 katika majarida ya kitaifa na kimataifa.
“Taasisi pia imeimarisha Student Information Management System (SIMS), unaohudumia takribani wanafunzi 37,143 na kuwezesha huduma za maombi, usajili, malipo, matokeo, transcript, maktaba na e-learning kupatikana mtandaoni,”amesema.



