Dodoma, Septemba 3, 2026.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Hashimu Komba, amesema upatikanaji wa umeme wa uhakika katika migodi una mchango mkubwa kwa uchumi wa Taifa, ambapo sekta hiyo huchangia zaidi ya Shilingi bilioni 340 kwa mwaka kupitia mrabaha, kodi na tozo mbalimbali.

Mhe. Komba ameyasema hayo Septemba 3, 2026, jijini Dodoma, katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya Mpomvu–GGM yenye msongo wa kilovoti 220 (220kV), pamoja na Kituo cha Kupoza Umeme katika eneo la GGM, mkoani Geita. Hafla hiyo ilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi.

Ameipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa juhudi za kuhakikisha umeme unafikishwa katika maeneo ya shughuli za madini, ikiwemo migodi mikubwa kama Geita Gold Mining (GGM), hatua inayosaidia kuongeza uzalishaji na kuchochea ukuaji wa sekta ya madini nchini.

“Tunawapongeza TANESCO kwa kuhakikisha umeme unafika katika maeneo ya migodi mikubwa kama GGM. Umeme wa uhakika ni muhimu katika kuhakikisha shughuli za uzalishaji zinaendelea bila vikwazo na hivyo kuongeza mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa Taifa,” amesema.

Aidha, Mhe. Komba amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi za kuendelea kusogeza huduma ya umeme kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema Mkoa wa Geita umefikia hatua ya vijiji vyote 474 kuwa na umeme, huku mkandarasi Central Electrical Installation akiendelea na kazi ya kupeleka umeme katika vitongoji 528 vya mkoa huo.

Katika hatua nyingine, Mhe. Komba amewaalika Watanzania, wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa pamoja na wawekezaji kushiriki katika maonesho ya madini yanayotarajiwa kufanyika Septemba 23, 2026, mkoani Geita.

Amesema maonesho hayo yatatoa fursa kwa wananchi na wadau mbalimbali kujionea fursa zinazotokana na rasilimali za madini zilizopo mkoani Geita na nchini kwa ujumla.

Mhe. Komba pia ameahidi kuwa uongozi wa Mkoa na Wilaya ya Geita utatoa ushirikiano wa karibu kwa mkandarasi pamoja na watumishi wa TANESCO ili kuhakikisha utekelezaji wa mradi wa Mpomvu–GGM unafanyika kwa wakati na bila vikwazo visivyo vya lazima.

Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha mradi unakamilika kwa ufanisi na kuchangia upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa shughuli za uchimbaji na uzalishaji katika sekta ya madini.