Na John Mapepele – WAF

Washington, D.C.

Serikali ya Tanzania imekubaliana na Chama cha Wafanyabiashara cha Marekani (U.S. Chamber of Commerce) mjini Washington, D.C na Serikali ya Marekani kufanya utekelezaji wa kimkakati wa mkataba wa sekta ya afya ulioingiwa hivi karibuni ili kuzinufaisha pande zote mbili,huku wakiifanya Tanzania kuwa muhimili wa uzalishaji na usambazaji dawa na vifaa tiba katika bara la Afrika.

Akizungumza leo Septemba 4,2026 kwenye Mkutano wa Wadau wa Ushirikiano wa Afya kati ya Marekani na Tanzania uliofanyika kati ya Serikali ya Tanzania na Chama cha Wafanyabiashara cha Marekani (U.S. Chamber of Commerce) mjini Washington, D.C., na baadaye kufanya kikao viongozi waandamizi Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Waziri wa Afya wa Tanzania, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, alifafanua kuwa tayari Tanzania imejipanga vema kuhakikisha mkataba unatekelezwa kikamilifu.

Akielezea zaidi kuhusu mazingira rafiki ya uwekezaji kwenye sekta ya dawa amesema Tanzania inafanya kazi ya kuoanisha utaratibu wa kutoza kodi na ushuru kwa malighafi na vifungashio vya dawa na mifumo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kwa lengo la kufanya uzalishaji wa ndani uwe na ushindani zaidi kuliko kuagiza bidhaa zilizokamilika kutoka nje.

Pia amesema,Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji na kiongozi wa Huduma za Ununuzi wa Pamoja za SADC (SADC Pooled Procurement Services), mpango unaolenga kuunganisha mahitaji ya dawa na bidhaa za afya katika nchi 16 wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.

Hili linaunda fursa yenye nguvu kwa wazalishaji.

Badala ya kuanzisha uzalishaji nchini Tanzania kwa lengo la kuhudumia soko la takribani watu milioni 60 pekee, wawekezaji wanaweza kuitumia Tanzania kama kituo cha uzalishaji na usambazaji kwa soko la kikanda linalojumuisha nchi 16 za SADC na zaidi ya watu milioni 300.

Amesema Tanzania iko tayari kushirikiana na wawekezaji makini kutoka Marekani na ipo tayari kupokea mtaji, teknolojia.

Ameongeza kuwa Serikali imepanua na kuboresha vituo vya afya nchini kote, huku Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, iliyosainiwa mwaka 2023, ikiweka msingi wa kisheria wa mfumo wa bima ya afya unaolenga nchi nzima na kwamba hivi karibuni, Tanzania inapanga kuzindua rasmi Bima ya Afya kwa Wote kitaifa, ikiwa na azma ya kuwaingiza hatua kwa hatua zaidi ya watu milioni 60 katika mfumo mmoja wa kugawana hatari za gharama za matibabu.

Aidha amesema, Serikali inatekeleza lengo jingine la kimkakati: kuibadilisha Tanzania kutoka nchi inayoagiza kwa kiwango kikubwa dawa kutoka nje na kuwa nchi inayozalisha dawa.

Anafafanua Mhe. Mchengerwa “Kufanya Tanzania iwe rahisi zaidi kuwekeza

Serikali inatambua kuwa kuvutia uwekezaji katika uzalishaji wa dawa kunahitaji zaidi ya kutangaza fursa. Kunahitaji kubadilisha mazingira ambayo kampuni zinafanyia kazi.

Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Wizara ya Afya imeanzisha Kikosi Kazi cha Kuharakisha Uwekezaji katika Sekta ya Dawa (Pharmaceutical Investment Acceleration Taskforce – PIAT), kinachowakutanisha taasisi muhimu zikiwemo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (Tanzania Investment Centre), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), Bohari ya Dawa (MSD), Mamlaka ya Mapato Tanzania na Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Kiuchumi”.

Pia amesema, Tanzania inaendeleza eneo maalum la kiuchumi kwa ajili ya sekta ya dawa huko Mloganzila, nje ya Dar es Salaam, ambako viwanja vilivyoandaliwa kwa ajili ya wawekezaji vinapatikana. Ugawaji wa awali wa baadhi ya maeneo tayari umefanyika.

Aidha, nchi inaunda mpango wa Kiwanda cha Taifa cha Uzalishaji wa Chanjo na Bidhaa za Kibiolojia, ikiwa ni sehemu ya azma yake pana ya kujenga uwezo wa uzalishaji wa ndani.

Aidha amesema TMDA imefikia Kiwango cha 3 cha viwango vya WHO, hatua inayoiweka Tanzania miongoni mwa nchi zenye mifumo ya udhibiti iliyoendelea zaidi barani Afrika.

Mamlaka hiyo pia inaandaa mifumo ya kutegemea maamuzi ya mamlaka nyingine za udhibiti, jambo linaloweza kupunguza kurudiwa kwa taratibu kwa bidhaa ambazo tayari zimeidhinishwa na mamlaka za udhibiti kama Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani (U.S. Food and Drug Administration).