Na John Mapepele – WAF, Washington, D.C.
Serikali ya Tanzania imekubaliana na Chama cha Wafanyabiashara cha Marekani (U.S. Chamber of Commerce) mjini Washington, D.C na Serikali ya Marekani kufanya utekelezaji wa kimkakati wa mkataba wa sekta ya afya ulioingiwa hivi karibuni ili kuzinufaisha pande zote mbili,huku wakiifanya Tanzania kuwa muhimili wa uzalishaji na usambazaji dawa na vifaa tiba Afrika.
Akizungumza katika Mkutano wa Wadau wa Ushirikiano wa Afya kati ya Marekani na Tanzania uliofanyika leo kati ya Serikali ya Tanzania na Chama cha Wafanyabiashara cha Marekani (U.S. Chamber of Commerce) mjini Washington, D.C., na baadaye kufanya kikao viongozi waandamizi Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Waziri wa Afya wa Tanzania, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, alifafanua kuwa tayari Tanzania imejipanga vema kuhakikisha mkataba unatekelezwa kikamilifu.
Amesema Tanzania iko tayari kushirikiana na wawekezaji makini kutoka Marekani na ipo tayari kupokea mtaji, teknolojia.
Akizungumzia historia ya muda mrefu baina ya nchi hizo, mhe Mchengerwa amefafanua kuwa
Mwaka 1970, Rais wa wakati huo, Julius Nyerere, alishirikisha kampuni ya ushauri wa usimamizi kutoka Marekani, McKinsey & Company, kusaidia Tanzania kuimarisha mifumo ya uendeshaji wa serikali.
Amesema kazi hiyo ilichangia mageuzi ya ugatuzi wa madaraka ya mwaka 1972, ambayo yalisogeza huduma za serikali karibu zaidi na wananchi na kuanzisha muundo wa utawala wa mikoa na wilaya ambao unaendelea kuwa na ushawishi katika sekta ya umma ya Tanzania hadi leo.
Kwa Mchengerwa, umuhimu wa uzoefu huo hauishii kwenye historia. “McKinsey haikuiuza Tanzania bidhaa tu Iliisaidia nchi kujenga taasisi—taasisi ambayo ushawishi wake uliendelea kuwepo muda mrefu baada ya mkataba wa kampuni hiyo ya ushauri kumalizika”amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Alieleza kuwa huo ndio mtazamo ambao Tanzania inautafuta kutoka kwa wafanyabiashara wa Marekani leo: si miamala pekee, bali ushirikiano wenye uwezo wa kujenga taasisi, viwanda na uwezo unaodumu kwa vizazi ambapo Chama cha Wafanyabiashara wa Marekani kimeahidi kuwaleta wawekezaji wa madawa nchini Tanzania ili kuja kuona na kuanza mashirikiano kwenye ene hili.
“Naomba niwahakikishie kuwa Serikali ya Tanzania tayari imeshaweka mazingira rafik ya uwekezaji kwenye eneo la afya na hive ninavyoongea hapa tayari kampını za marekani zimeanza kufanya kazi” amesisitiza Mhe. Mchengerwa.
Mhe. Mchengerwa ambaye ameambatana katika msafara wake na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia eneo la dawa na vifaa tiba, Emmanuel Tayari na Watendaji wakuu wa taasisi chini ya Wizara ya Afya alifafanua hatua kubwa iliyofikiwa katika sekta ya afya nchini.
Amesema Chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, Tanzania imeanza kutekeleza mpango kabambe wa mageuzi ya kitaifa unaojengwa juu ya kile anachokiita katika 4R: Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Ujenzi Upya.





