SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeandaa kliniki ya viwango katika maeneo ya Soko Kuu la Biashara Kariakoo na Mwenge jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kusogeza huduma za kitaalamu karibu na wafanyabiashara wa bidhaa za chakula na vipodozi ili kuwawezesha kuendesha biashara zinazokidhi viwango.
Kliniki hiyo itafanyika kuanzia Septemba 7 hadi 11, mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa TBS wa kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi na wafanyabiashara, hususan wanaojihusisha na bidhaa za chakula na vipodozi.
Akizungumza na waandishi wa habari Meneja wa Usajili wa Bidhaa na Majengo wa TBS, Habakuki Kalebo, amesema wataalamu wa shirika hilo watakuwepo katika maeneo hayo kutoa huduma za ushauri na utaalamu kwa wadau wa sekta hizo.
Amesema kliniki hiyo itawapa wafanyabiashara fursa ya kupata elimu kuhusu huduma za usajili wa bidhaa za chakula na vipodozi, pamoja na usajili wa maeneo yanayohusika na uzalishaji, uhifadhi na biashara ya bidhaa hizo.
“Lengo kubwa la kliniki hii ni kuhakikisha kuwa TBS inawapatia huduma ya ushauri na huduma ya usajili wa bidhaa za chakula pamoja na vipodozi,” amesema Kalebo.
Ameongeza kuwa wataalamu hao pia watatoa elimu kwa wafanyabiashara wanaotengeneza maudhui mtandaoni kuhusu umuhimu wa kutumia maudhui sahihi yasiyo na upotoshaji kwa jamii juu bidhaa za chakula na vipodozi.
Kalebo amewataka waingizaji, wasambazaji, wauzaji, wasafirishaji, wahifadhi na wadau wengine wanaohusika na bidhaa za chakula na vipodozi kutumia fursa hiyo kwa kufika katika mabanda ya TBS kupata huduma hizo.
Aidha amesema kuwa, hatua hiyo inalenga kuwasaidia wafanyabiashara kuwa na uelewa sahihi kuhusu ubora na usalama wa bidhaa, huku ikichangia kujenga mazingira bora ya biashara nchini.
Amesema utekelezaji wa kliniki hiyo pia unalenga kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kuhakikisha wafanyabiashara wanauza bidhaa bora, salama na zinazoaminika na walaji.
“Lengo ni kuhakikisha tunakuza uchumi wa nchi hii, kwa maana mfanyabiashara atakuwa na uhakika wa kuuza bidhaa bora na salama na ambayo inaaminika,” amesema.



