Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeibuka mshindi wa pili katika kundi la Taasisi za Udhibiti wakati wa Maonesho ya 21 ya Biashara Afrika Mashariki (MEATF), yanayofanyika katika Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza.
Ushindi huo unaonesha namna TBS inavyoendelea kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha bidhaa na huduma zinazotolewa nchini zinakidhi matakwa ya viwango, pamoja na kujenga uelewa wa matumizi ya viwango miongoni mwa wazalishaji, wafanyabiashara na wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa Mashariki, Happy Brown, amesema ushindi huo unaonesha dhamira ya TBS ya kuendelea kuwafikia wananchi na wadau mbalimbali kupitia utoaji wa elimu kuhusu viwango, ubora na usalama wa bidhaa.
Amesema ushiriki wa TBS katika maonesho hayo umeendelea kuwa fursa muhimu ya kuwahudumia wananchi, hasa wajasiriamali na wafanyabiashara, kwa kuwaelimisha kuhusu viwango vinavyohitajika katika shughuli zao na kuwawezesha kupata huduma mbalimbali za TBS.
“Ushindi huu unaonesha dhamira ya TBS ya kuhakikisha elimu kuhusu viwango inawafikia wananchi na wadau wa biashara, ili kuwawezesha kuzalisha na kuuza bidhaa zenye ubora, usalama na zinazokidhi matakwa ya viwango,” amesema Brown.
Kupitia ushiriki wake katika maonesho hayo, TBS imeendelea kutoa elimu kuhusu viwango, ubora na usalama wa bidhaa, pamoja na huduma zinazotolewa na Shirika ikiwemo upatikanaji na ununuzi wa viwango kupitia Maktaba ya Viwango ya TBS.
Aidha, TBS imeendelea kutoa mwongozo kwa wazalishaji na wafanyabiashara kuhusu mahitaji ya viwango na taratibu za tathmini ya ulinganifu, kwa lengo la kuwawezesha kuzalisha na kuuza bidhaa zenye ubora na zinazokidhi matakwa ya viwango.
Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa maonesho hayo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi, amesema Serikali inalenga kuifanya Tanzania ipige hatua kutoka kuwa soko la bidhaa kutoka nje na kuwa kitovu cha uzalishaji na usambazaji wa bidhaa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.
“Tunataka Tanzania isiwe soko pekee la bidhaa; tunataka iwe kitovu cha uzalishaji na usambazaji wa bidhaa katika Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla,” amesema Mhe. Londo.
Ameongeza kuwa maonesho ya biashara kama MEATF yana nafasi muhimu katika kuwaunganisha wazalishaji, wafanyabiashara, wawekezaji na wadau mbalimbali wa sekta ya biashara, sambamba na kutoa fursa ya kutangaza bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini katika masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.
Maonesho hayo yanayofanyika chini ya kaulimbiu “Usalama na Amani ni Kichocheo cha Biashara na Uwekezaji Hapa Nchini”, yalianza tarehe 28 Agosti 2026 na yanatarajiwa kufikia tamati tarehe 6 Septemba 2026.



