*Aipongeza CTI tuzo za PMAYA kwa kuchochea ukuaji wa uchumi

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MAKAMU wa Rais, Deogratius Ndejembi ameitaka Wizara ya Viwanda na Biashara kukaa na wazalishaji wa saruji kuweka mipango kuhakikisha saruji inapatikana kwa wingi na inashuka bei na kurejea ilivyokuwa.

Alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam mara baada ya kutoa tuzo kwa wazalishaji bora viwandani katika tuzo ya Rais ya Kwa Mzalishaji Bora Viwandani (PMAYA), inayosimamiwa na Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI).

Kampuni ya sigara iliongoza kwa kushika nafasi ya kwanza kwa ushindi wa jumla ikifuatiwa na Plasco Ltd na ALAF Limited

Alisema hivi sasa watanzania wanalazimika kununua saruji kwa gharama kubwa kutokana na viongozi kushindwa kuratibu vyema uzalishaji wa bidhaa hiyo viwandani.

“Haya yanasababisha uhaba wa saruji na anayeumia hapa ni mtanzania wa kawaida na serikali hii ya awamu ya sita ya daktari Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake anataka kuona mtanzania anapata mfuko wa saruji kwa gharama nafuu,” alisema na kuongeza

“Sasa nakuagiza Waziri wa Viwanda na Biashara namwona hapa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kanei pamoja mmalize hili suala ili mtanzania apate saruji bei iliyokuwepo,” alisema

“Nataka kuona maono ya Rais Samia kutaka mtanzania wa kawaida anapata saruji kwa bei ya kawaida yanatekelezeka na ninataka kupata ripoti ya suala hilo baada ya kikao hiki, kaeni mjadili suala hili na muandike ripoti tumkabidhi Rais,” alisema

Alisema sekta ya viwanda imeendelea kukua kwa kasi na viashiria mbalimbali vya uchumi vinaonyesha mafanikio chanya ya sekta ya viwanda akitolea mfano mwaka 2025 sekta ya viwanda ilikuwa kwa asilimia 5.2 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.2 mwaka 2024.

Aidha, alisema mchango wa sekta ya uzalishaji katika pato la taifa mwaka 2025 ulifikia asilimia 5.9 na kwamba inakadiriwa kuwa asilimia 12 ya ajira rasmi na bidhaa zilizokuwa zinauzwa nje zilikuwa za viwandani.

“Haya ni mafanikio makubwa kwa takwimu lakini lazima tujiulize viwanda vyetu vimekua kwa kiasi gani na je ukuaji huu unaviwezesha kuwa na ushindani Afrika Mashariki na duniani na je tunajipima kwa hayo au bado tunazalisha kwa kuangalia soko la ndani peke yake,” alihoji Makamu wa Rais

Mkurugenzi Mkuu wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Leodegar Tenga, alisema

PMAYA inalenga kutambua, kuthamini na kuenzi mchango wa sekta ya viwanda katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Alisema tuzo hizo pia ni jukwaa la wazalishaji na wadau wa viwanda kukutana, kujadiliana na kubadilishana uzoefu kuhusu namna ya kuendeleza sekta hiyo.

Alisisitiza kuwa tuzo hizo zinapaswa kuwa kichocheo cha kuongeza tija, ubunifu na ushindani katika uzalishaji wa viwandani.

Tenga alisisitiza umuhimu wa uzalishaji endelevu unaozingatia mazingira Environmental, Social and Governance (ESG), akisema ESG inazidi kuwa muhimu katika upatikanaji wa fedha, uwekezaji, masoko na kuingia katika minyororo ya thamani ya kimataifa.

Alisema kwa PMAYA 19, CTI imeanzisha Mabalozi 10 wa ESG, ambao watafuatiliwa kwa mwaka mmoja ili kupima utekelezaji na matokeo ya kanuni hizo katika kampuni zao.

Kampuni itakayofanya vizuri zaidi itatambuliwa kama ESG Champion katika PMAYA 20.