Shirika la Masoko ya Kariakoo limewarejesha wafanyabiashara wa pembejeo na viuatilifu katika Soko Kuu la Kariakoo ambao walikuwa hawajarejeshwa sokoni hapo baada ya soko hilo kufunguliwa Februari 8, 2026.

Kurejeshwa kwa wafanyabiashara haokunatoka na majadiliano baina ya uongozi wa Shirika na wafanyabiashara hao kuhusu kuwa na eneo la kufanyia biashara zao zinazokidhi mahitaji yao kwa mujibu wa sheria, kanuni, na taratibu zinazosimamia biashara hiyo nchini.

Akizungumza wakati wa urejeshaji wa wafanyabiashara hao, Meneja Mkuu Shirika la Masoko ya Kariakoo, CPA. Ashraph Abdulkarim amesema kurejeshwa kwa wafanyabiashara hao kutakuwa kichocheo muhimu kwa biashara zilizopo sokoni hapo kwakuwa biashara zilizopo zinataegemeana.

“Sisi Soko Kuu la Kariakoo tunayo bahati kwani ndio eneo pekee ambalo unaweza kupata bidhaa zaidi ya moja katika eneo moja, ukitaka mahitaji ya nyumbani utapata, ukihitaji huduma za afya utapata, ukihitaji nguo utapata nk bila kutoka nje ya jingo letu, hivyo tunaendelea wananchi kuendelea kuchangamkia fursa ya uwepo wa soko hili kwa kupata huduma mbalimbali” amebainisha CPA. Abdulkarim

Kwa upande wao wafanyabiashara wa pembejeo na viuatilifu wameupongeza na kuushukuru uongozi wa soko hilo kwa namna walivyoshughulikia changamoto ya wao kuwa nje ya soko hilo na sasa wanajisikia faraja kurejea katika mazingira ambayo wamekuwa wakiyatumia kwa biashara zao kwa muda mrefu kabla ya soko hilo kupata ajali ya moto mwaka 2021.