Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

MADEREVA 56 wamefikishwa mahakamani mkoani Pwani kwa makosa mbalimbali ya usalama barabarani, huku madereva wengine 12 wakifungiwa leseni kwa kukiuka sheria za usalama barabarani.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Pwani, Edson Mwakihaba, amesema hayo wakati akieleza hatua zilizochukuliwa katika operesheni za kudhibiti ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani zilizofanyika mwezi Agosti mwaka huu.

Amesema katika operesheni hizo, jumla ya makosa 20,225 ya usalama barabarani yalikamatwa, huku faini zilizotokana na makosa hayo zikifikia shilingi milioni 590.2.

Mwakihaba amesema hatua hizo zinalenga kudhibiti ukiukwaji wa sheria na kupunguza ajali zinazotokana na uzembe, akisisitiza kuwa lengo la operesheni hizo si kukusanya faini, bali kuhakikisha madereva wanazingatia sheria na kulinda maisha ya watumiaji wote wa barabara.

Aidha, amewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani, kuepuka mwendo kasi na uzembe, huku akiwataka watumiaji wa barabara kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za ukiukwaji wa sheria ili kusaidia kupunguza ajali.