
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi, amewasalimu Wananchi wa Mbuyuni, Wilayani Moshi waliokusanyika kumlaki akiwa katika ziara binafsi mkoani Kilimanjaro leo tarehe 01 Septemba 2026.
Akiwasalimu wananchi hao, Makamu wa Rais amewasihi kuendelea kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na yeye ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Amesema kwa imani ya maombi ataweza kumsaidia kwa hekima na utii Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Makamu wa Rais amesema ataendelea kutekeleza wajibu wake kwa uadilifu, umakini na kujituma, akisisitiza utayari wake wa kushirikiana na viongozi pamoja na wananchi.
Akizungumza kwa msisitizo, Makamu wa Rais amesema: “Hatawazingua Wana wala hatamzingua Mama,” kauli ambayo aliitoa pia mkoani Dodoma, kwa wananchi wa Chamwino, mara baada ya kuapishwa.
Awali, Makamu wa Rais aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ambapo alipokelewa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Viongozi wa Dini na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kilimanjaro.






