Aziza Nangwa,Jamhuri Media, Dar es Salaam
Wakati tukielekea katika maazimisho ya siku ya utambulisho Duniani Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa nchini (NIDA) imezindua kampeni ya “Kipo, Chukue, Kamilisha Safari Yako,” ikiwa na lengo la kuhamasisha wananchi waliokwisha sajiliwa kuchukua vitambulisho vyao na kuvitumia kwa usahihi
Kauli hiyo ilitolewa na msemaji mkuu wa Serikali Gerson Msigwa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Utambulisho Duniani, akieleza kuwa Serikali imepiga hatua kubwa katika usajili na utambuzi wa wananchi pamoja na matumizi ya namba ya utambulisho katika huduma mbalimbali.
Msigwa, amewataka Watanzania kutotoa vitambulisho vyao vya Taifa kwa watu wengine kwa ajili ya kusajili laini za simu au kupata huduma nyingine, akisema hatua hiyo inaweza kuwaingiza katika matatizo ya kisheria endapo vitambulisho hivyo vitatumika kufanya uhalifu.
Amesema hadi kufikia Agosti 2026, jumla ya taasisi 157, zikiwemo 72 za Serikali na 85 za sekta binafsi, zimeunganishwa na mfumo wa usajili na utambuzi wa watu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), hatua inayowezesha taasisi hizo kuhakiki taarifa za watu wanaowahudumia na kupunguza uwezekano wa matumizi ya taarifa bandia.
Msigwa ammesema mfumo huo una umuhimu katika kuimarisha usalama na uwajibikaji, kwa kuwa taasisi zinazohudumia wananchi zinaweza kuthibitisha utambulisho wa mtu kabla ya kumpatia huduma au kuingia naye katika shughuli mbalimbali.
“Kitambulisho chako cha NIDA ni utambulisho wako binafsi na kinapaswa kutumiwa na wewe mwenyewe, si mtu mwingine,” alisema Msigwa, akisisitiza kuwa mwananchi anaweza kuwajibishwa iwapo kitambulisho chake kitatumiwa katika tukio la uhalifu.
Amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakikabidhi vitambulisho vyao kwa ndugu au marafiki kwa nia ya kuwasaidia kusajili laini za simu, hasa watu ambao hawana sifa za kufanya usajili huo, bila kufahamu matumizi ambayo yanaweza kufanywa kwa laini hizo.
Kwa mujibu wa Msigwa, mfumo wa NIDA pia unasaidia taasisi za usalama katika kukabiliana na uhalifu wa mtandao, utakatishaji fedha na vitendo vingine vya kihalifu kupitia uthibitishaji wa taarifa za
watumiaji wa huduma.
Aidha, amesema matumizi ya namba ya Taifa yamepanuka katika sekta mbalimbali, ikiwemo usajili wa walipa kodi, huduma za kifedha, bima ya afya, mikopo ya elimu ya juu, huduma za TASAF, usajili wa biashara na uwekezaji.
Msigwa amesema Serikali imepanga kuendelea kuboresha mfumo wa vitambulisho vya Taifa kwa kuanza kutumia teknolojia mpya ya uchapishaji itakayoongeza ubora, uimara na usalama wa taarifa zilizomo kwenye vitambulisho.
Amesema Serikali inalenga kuwezesha kitambulisho cha Taifa kubeba taarifa zinazohusiana na huduma nyingine, ikiwemo bima ya afya, hati ya kusafiria ndani ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na leseni ya udereva, hatua ambayo itasaidia kupunguza idadi ya vitambulisho ambavyo mwananchi anapaswa kubeba.
Mpango mwingine ni kuanza usajili na utambuzi wa watu wenye umri chini ya miaka 18 ili kuwapatia namba ya utambulisho wa kipekee itakayowawezesha kupata huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi tangu utotoni.
Msigwa amesema NIDA pia inaendelea kuboresha mfumo wa utambuzi wa watu kwa kutumia teknolojia za kibaiolojia, ikiwemo utambuzi wa sura na mboni za macho, hasa kwa watu ambao alama zao za vidole hazijakamilika.
Aidha amewataka Watanzania ambao vitambulisho vyao vya Taifa vimekamilika lakini hawajavichukua kwenda katika ofisi za NIDA na kuvichukua,ambapo kwa sasa zaidi ya vitambulisho milioni 21 vimekwishatengenezwa, huku zaidi ya milioni moja na nusu vikiwa bado havijachukuliwa na wananchi.
“Serikali imewekeza fedha nyingi kuhakikisha Watanzania wanapata vitambulisho hivi. Inawezekana kwa sasa unaona hukihitaji, lakini iko siku utakihitaji,” amesema
Amesema kampeni ya kitaifa ya Septemba ya Utambulisho imeanza Septemba 1 na kilele chake kitakuwa Septemba 16, ambayo ni Siku ya Utambulisho Duniani, huku shughuli za utoaji huduma, elimu na ugawaji wa vitambulisho zikiendelea hadi Septemba 30.
Msigwa aliwataka wananchi, taasisi za Serikali na sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kampeni hiyo, akisema utambulisho wa mtu ni msingi wa kupata huduma, kuimarisha usalama na kuwezesha ushiriki katika uchumi wa kidijitali.


