Watanzania kutoka makundi mbalimbali wanatarajiwa kukutana Novemba 7 mwaka huu , kwa ajili ya kuliombea Taifa, kuimarisha umoja na mshikamano, huku viongozi, vijana na wanawake wakishiriki katika mjadala wa kujenga Tanzania yenye maadili.
Mwenyekiti wa Tanzania National Prayer Breakfast, Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye, alisema mkutano huo utafanyika jijini Dodoma .
Alisema,Jukwaa hilo linalenga kuwaunganisha Watanzania bila kujali tofauti za dini, vyama au makundi yao, pamoja na kutoa nafasi ya kujadili masuala ya uongozi, maadili, utumishi wa umma na maendeleo ya Taifa.
Alisema lengo kuu ni kuendelea kujenga umoja wa kitaifa kwa kuwakumbusha Watanzania wajibu wao wa kushirikiana na kuheshimiana katika kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa taifa moja.
“Lengo letu ni kuendelea pamoja, taifa moja na watu wamoja,ni wajibu wetu kukumbushana kama taifa umuhimu wa kuwa kitu kimoja,” alisema.
Sumaye alisema mwaka huu maandalizi ya tukio hilo yamepangwa kufanyika kwa kiwango kikubwa zaidi ili Watanzania wengi watambue umuhimu wa jukwaa hilo, huku Serikali na Bunge zikitarajiwa kulitambua kama sehemu ya kuimarisha umoja, maadili na mshikamano wa Taifa.
Alisema Tanzania National Prayer Breakfast si jukwaa la dini moja au kundi fulani, bali linawakutanisha watu wa dini mbalimbali, vyama tofauti na makundi mbalimbali kwa lengo la kuliombea taifa na kujenga misingi ya kuendelea pamoja.
Kwa mujibu wa Sumaye, shughuli za mwaka huu zitaanza Novemba 5 kwa semina, huku Novemba 6 kukiwa na mjumuiko wa wanawake, ambao alisema wamekuwa wakibaki nyuma katika kushiriki katika majukwaa ya aina hiyo.
Alisema vijana nao watapewa nafasi katika programu hiyo, kwa kuwa jukwaa hilo ni sehemu ya programu ya kiuongozi inayolenga kuwajenga katika maadili, uongozi bora na uwajibikaji.
Alisema kilele kitakuwa Novemba 7, siku ya Tanzania National Prayer Breakfast, ambapo wanatarajia mgeni rasmi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema washiriki wanatarajiwa kutoka ndani na nje ya Tanzania, wakiwamo wawakilishi wa mabunge, mahakama, mashirika ya kimataifa, vijana na wanawake kutoka maeneo ya mijini na vijijini.
Alisema ushiriki huo unaonyesha kuwa jukwaa hilo lina mtazamo mpana wa kuunganisha watu kupitia uongozi wa maadili, maombi na ushirikiano.
Alisema jukwaa hilo linashirikisha wadau mbalimbali, wakiwamo KLNT, Kingdom Leadership, Tanzania World Vision pamoja na kikundi cha waombaji wa wabunge, ambao wamekuwa sehemu ya maandalizi ya tukio hilo.
Sumaye alisema wanataka Tanzania National Prayer Breakfast kuwa jukwaa linalotambulika zaidi kitaifa na kutarajia Serikali pamoja na Bunge kuona umuhimu wa kulibeba na kuliendeleza katika miaka ijayo.
Alisema endapo Bunge litaridhia, mwakani wanataka suala hilo lipewe nafasi kubwa zaidi kwa kuwa jambo linalolenga kuwaunganisha Watanzania halipaswi kuishia njiani wala kukosa kuendelezwa.
Kwa upande wake, Katibu wa Tanzania National Prayer Breakfast, Isack Mpatwa, alisema jambo la msingi ni kuwa na mkakati madhubuti wa kuwakutanisha watu kutoka makundi mbalimbali ili kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa.
Mpatwa alisema jukwaa hilo linapaswa kuendelea kuwa eneo la kukumbushana kuhusu maadili, uongozi bora na wajibu wa kila mmoja katika kulijenga Taifa.
Alisema lengo si kwa kundi moja pekee, bali dini na vyama vyote vinapaswa kuwa sehemu ya juhudi hizo kwa kuwa Tanzania ni ya watu wote.
Alisema Tanzania National Prayer Breakfast ni sehemu ya programu pana ya uongozi wa maadili, utumishi wa umma na maombi jumuishi, inayolenga kuwaunganisha viongozi na wananchi katika kujenga taifa lenye umoja na mshikamano.
Alisema kupitia mikutano hiyo, Watanzania wanapata nafasi ya kukutana, kuombea nchi yao na kukumbushana umuhimu wa kuendelea kushirikiana katika kulinda umoja na amani ya Taifa.


