Na Mwandishi Wetu,Jamhuri Media,Dar es salaam

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Tano la Kimataifa la Uchumi wa Buluu, litakalofanyika Septemba 7 hadi 9, 2026 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Kongamano hilo linatarajiwa kuwakutanisha wataalamu, watafiti, wanasayansi, watunga sera na wadau mbalimbali wa Uchumi wa Buluu kutoka Tanzania, Afrika na mataifa mengine duniani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Septemba 3, 2026, Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam, Tumaini Gurumo, amesema kongamano hilo la siku tatu linalenga kujadili fursa zilizopo katika sekta ya Uchumi wa Buluu na namna bora ya kuzitumia kwa ajili ya kukuza uchumi na maendeleo endelevu.

Amesema washiriki watapata fursa ya kusikiliza mawasilisho ya kitaalamu pamoja na matokeo ya tafiti mbalimbali zinazohusu Uchumi wa Buluu, zitakazosaidia kubaini changamoto zilizopo na kutafuta suluhisho kwa ajili ya kuendeleza sekta hiyo nchini Tanzania na barani Afrika.

“Lengo ni kuwakutanisha wabobezi wa masuala ya Uchumi wa Buluu pamoja na wadau mbalimbali, wakiwemo wale wenye uelewa mkubwa wa sekta hii na wale wanaotaka kujifunza zaidi,” amesema Gurumo.

Amesema kongamano hilo pia litatoa elimu kuhusu fursa za kiuchumi zinazopatikana kupitia bahari, mito, maziwa na rasilimali nyingine za maji, huku likilenga kuchochea ubunifu, ajira na matumizi endelevu ya rasilimali hizo.

Kwa mujibu wa Gurumo, kongamano hilo linaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika, ambazo zinasisitiza matumizi endelevu ya rasilimali kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Amesema hadi sasa washiriki kutoka ndani na nje ya Tanzania wamethibitisha kushiriki, wakiwemo kutoka Kenya, Ghana, Afrika Kusini, Comoro, Seychelles na Uganda.

Kwa upande wa mataifa ya nje ya Afrika, amesema washiriki wanatarajiwa kutoka Japan, Sweden, Urusi na nchi nyingine, huku mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini Tanzania, taasisi za kitaifa na kimataifa, viongozi wa serikali na sekta binafsi, wanasayansi na watafiti wakitarajiwa kushiriki.

Aidha, waandaaji wamewaalika vijana kutoka vyuo vikuu, shule za sekondari na shule za msingi kushiriki katika kongamano hilo, ikiwa ni sehemu ya kuwajengea uelewa kuhusu Uchumi wa Buluu na fursa zinazopatikana katika sekta hiyo.

Gurumo amesema ushiriki wa vijana ni muhimu ili kuhakikisha agenda ya Uchumi wa Buluu inafahamika na kubebwa na kizazi kijacho, pamoja na kuwawezesha kutambua nafasi yao katika kutumia fursa zinazotokana na rasilimali za maji.

Amewataka Watanzania kushiriki katika kongamano hilo ili kupata uelewa mpana kuhusu Uchumi wa Buluu na namna rasilimali za bahari, mito, maziwa na vyanzo vingine vya maji zinavyoweza kutumika kuchochea maendeleo endelevu nchini na barani Afrika.