📌 Kukamilika kwa njia mpya kutatoa fursa kwa njia ya awali kuendelea kunufaisha wananchi wa mkoa wa Geita na kuchochea shughuli za kiuchumi.

📌 Serikali yawekeza takribani Shilingi bilioni 63.19 kuutekeleza

Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) inaendelea kuimarisha miundombinu ya umeme nchini kupitia utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Mpomvu hadi kituo cha kupokea na kupoza umeme cha GGM, wenye urefu wa takribani kilomita 6.7.

Akizungumza Septemba 3, 2026, jijini Dodoma, wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa utekelezaji wa mradi huo, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuchochea shughuli za kiuchumi, ikiwemo uzalishaji, ajira, ongezeko la mapato na uwekezaji.

Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na TANESCO na wadau wa sekta ya nishati kuhakikisha miundombinu ya umeme inaendana na kasi ya ukuaji wa mahitaji.

“Serikali itaendelea kushirikiana na TANESCO na wadau wote wa sekta ya nishati kuhakikisha miundombinu ya umeme inaendana na kasi ya ukuaji wa mahitaji. Tunataka kuona umeme unaozalishwa nchini ukitumika kikamilifu kuchochea uzalishaji, kuongeza ajira, kuongeza mapato na kuvutia uwekezaji zaidi. Mradi huu ni kielelezo cha falsafa hiyo,” amesema Mhe. Salome.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amesema mradi huo unatekelezwa kwa miezi 18 kutoka tarehe ya utiaji saini mkataba ukilenga kukidhi ongezeko la mahitaji ya umeme kwa GGM.

“Mradi huu unagharimu takribani Shilingi bilioni 63.19 za Kitanzania na kutokana na kuwa GGM ni miongoni mwa wateja wetu wakubwa wenye kuchangia kiasi kikubwa cha mapato kwa Shirika, tutahakikisha mradi huu unafanikiwa kama inavyotarajiwa kukidhi ongezeko la mahitaji yao kwa manufaa ya pande zote mbili na pato la Taifa kwa ujumla,” amesema Bw. Twange.

Aidha, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Mhe. Balozi Zuhura Bundala, amesema utiaji saini wa mkataba huo ni sehemu ya hatua za kimkakati za kujenga uwezo wa TANESCO kukidhi mahitaji ya wateja na kufungua fursa za uwekezaji na ajira.

“Utiaji saini huu ni sehemu ya kimkakati kujenga uwezo wa TANESCO kukidhi mahitaji ya wateja na kufungua fursa za uwekezaji na ajira. Bodi tutaendelea kuisimamia TANESCO kukidhi ongezeko la hitaji la umeme kwa kuimarisha na kuwekeza kwenye ujenzi wa miundombinu ya umeme,” amesema Mhe. Bundala.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO kwa namna inavyosimamia Shirika katika ujenzi wa uchumi wa kisasa kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Niipongeze Bodi ya Wakurugenzi TANESCO kwa namna mnavyosimamia Shirika hili kujenga uchumi wa kisasa kuelekea Dira 2050. Utekelezaji wa mradi huu unatupa nguvu zaidi kwa sababu sekta zote, nishati na madini, zipo chini yetu,” amesema Mhe. Mgalu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Hashimu Komba, akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa huo amesema Uongozi wa Mkoa umejipanga kushirikiana na mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha utekelezaji wake haupati kikwazo, akisisitiza umuhimu wa nishati ya umeme katika kuchochea maendeleo ya sekta mbalimbali.

“Ni dhahiri, nishati ya umeme inachagiza maendeleo ya sekta zote. Tunampongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anavyosukuma kwa dhati agenda ya nishati ya umeme kuwafikia wananchi. Mamlaka ya Mkoa imejipanga kushirikiana na Mkandarasi wa mradi wa umeme wa Mpomvu–GGM kuhakikisha mradi haupati kikwazo,” amesisitiza Mhe. Komba.

Kukamilika kwa mradi huo, kutatoa fursa ya njia ya awali ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoto 33 iliyokuwa ikipelekea umeme GGM, kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika Mkoa wa Geita na maeneo ya pembezoni , vilevile kuwezesha wananchi kuendesha shughuli zao za uzalishaji kwa ufanisi, pamoja na kuweka mazingira wezeshi kwa uwekezaji mpya ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha na kuongeza uwezo wa mfumo wa usafirishaji na usambazaji wa umeme kukidhi mahitaji ya sasa na yajayo.