Na Mwamvua Mwinyi, JamhutiMedia, Pwani

KATIBU Tawala Mkoa wa Pwani, Richard Marcellino Kayombo, amekabidhiwa ofisi na kuanza majukumu yake baada ya kuchukua nafasi ya Pili Mnyema, katika hafla iliyofanyika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani.

Kayombo, ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, amechukua nafasi hiyo baada ya Mnyema kuhamishwa na kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga.

Akizungumza septemba 4,2026 baada ya makabidhiano hayo, Kayombo amewataka viongozi na watendaji wa Mkoa wa Pwani, hususan kitengo cha miundombinu, kujiandaa mapema kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño zinazotarajiwa kuanza mwezi Oktoba mwaka huu.

Aidha, Kayombo amesisitiza utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa kuwaapisha viongozi wapya, akielekeza sekta ya elimu mkoani humo kuanza mara moja maandalizi ya kutekeleza maagizo hayo kuelekea mwaka 2028.

Alisema maandalizi hayo yanapaswa kufanyika kwa wakati ili kuhakikisha Mkoa wa Pwani unakuwa tayari kukabiliana na mahitaji ya elimu yatakayojitokeza kutokana na ongezeko la wanafunzi.

Kayombo pia aliahidi kushirikiana na viongozi na watumishi wa Mkoa wa Pwani katika kuhakikisha mkoa unaendelea kuwa kinara katika sekta ya viwanda, uwekezaji na kuongeza uzalishaji, huku akisisitiza utekelezaji wa mipango na vipaumbele vya Serikali katika ngazi ya mkoa.

“Nawategemea sana , msiniangushe. Kikubwa naomba muendelee kuchapa kazi,” alisema Kayombo.

Kwa upande wake, Mnyema amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini na kumpa majukumu mbalimbali ya kulitumikia Taifa, akisema uteuzi huo ni heshima kubwa na unaacha alama katika maisha yake.

“Rais aliniteua kuja Mkoa wa Pwani nikitokea Tanga kumsaidia Mkuu wa Mkoa kuinua mapato, nashukuru kwa ushirikiano wa wakurugenzi, makatibu tawala wa wilaya, wakuu wa wilaya, vitengo, idara, watendaji na watumishi, ambao kwa pamoja tumeweza kufikia malengo aliyoyatarajia,” alieleza Mnyema.

Makabidhiano hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mabadiliko ya kiutumishi yaliyofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Agosti 27, 2026, na viongozi walioteuliwa kuapishwa rasmi Septemba 2, 2026 katika Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar.

Kabla ya uteuzi huo, Kayombo alikuwa Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).