*Malalamiko ya wakazi yachochea ukaguzi Kisota, mdhibiti ataka maelezo ndani ya siku saba

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeingilia kati ujenzi unaohusishwa na mpango wa kuanzisha Bandari Kavu (ICD) katika eneo la makazi la Kisota, Kigamboni, Dar es Salaam, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi.

TASAC imefanya ukaguzi katika eneo la mradi na kubaini ujenzi wa miundombinu mbalimbali ukiendelea, hatua iliyolisukuma Shirika kutaka maelezo kuhusu matumizi yanayokusudiwa ya eneo hilo.

Katika barua ya Septemba 4, 2026 ambayo JAMHURI imeiona, TASAC inasema ilipokea malalamiko kuhusu mpango wa kuanzisha ICD katika Plot Na. 1163, eneo lililotengwa kwa matumizi ya makazi.

“Malalamiko yalifuatia tangazo la umma lililoonyesha nia ya kubadilisha matumizi ya ardhi kutoka makazi kwenda shughuli za bandari kavu,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.

Baada ya malalamiko, TASAC ilifanya ukaguzi na kubaini ujenzi wa miundombinu ukiendelea.

Shirika limetaka maelezo ya maandishi ndani ya siku saba kuhusu iwapo eneo linaloendelezwa linakusudiwa kutumika kwa shughuli za ICD.

Hatua hiyo imekuja wakati wakazi wa Kisota wakiendelea kupinga mpango wa kubadilisha matumizi ya ardhi katika Kitalu Na. 6, Barabara ya Damiani/Saranga, kutoka makazi kwenda kuwa ya kibiashara na ujenzi wa ICD.

Katika barua yao ya Agosti 24, 2026, wakazi wanasema hawapingi uwekezaji wa bandari kavu, ila wanataka ufanyike katika maeneo yaliyopangwa kwa shughuli za aina hiyo.

“Shughuli hizo zinapaswa kuendelezwa katika maeneo yaliyopangwa na kutengwa mahsusi kwa matumizi hayo, bila kuathiri usalama, ustawi, amani na haki za wakazi,” wanaeleza.

Hoja yao ni kuhofia malori makubwa kuingia katika barabara za makazi ya watu na kuongeza msongamano, kelele, vumbi, hatari kwa watembea kwa miguu na watoto pamoja na uchakavu wa miundombinu.

Chanzo cha habari cha JAMHURI Digital kinasema eneo linaloandaliwa lipo Kisota Block 6, Barabara ya Saranga/Damiani, mkabala na Makaburi ya Kisota.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, eneo la awali linakadiriwa kuwa na mita za mraba 10,000, huku nyumba kadhaa zinazolizunguka zikinunuliwa kwa lengo la kuongeza ukubwa wake.

Chanzo hicho kinadai takribani nyumba sita zimenunuliwa na eneo la takribani mita za mraba 1,700 za ziada kuongezwa, huku juhudi za kupata maeneo mengine zikiendelea.

Ili kuanzisha ICD, miongozo na taratibu za TASAC zinamtaka mfanyabiashara kuwa na eneo lisilopungua mita za mraba 40,000; ukubwa ambao, kwa mujibu wa vyanzo vyetu, haujafikiwa na mwekezaji katika eneo la Kisota.

JAMHURI Digital bado haijathibitisha kwa nyaraka ukubwa halisi wa sasa wa eneo lililounganishwa wala idadi ya nyumba zilizonunuliwa.

“Tayari malori yameanza kuonekana katika eneo linaloandaliwa, hali inayoongeza hofu miongoni mwetu, kwamba shughuli za ICD zinaweza kuanza kabla ya taratibu zote kukamilika,” anasema mtoa taarifa wetu.

Wakazi wenyewe walieleza katika pingamizi lao kwamba waliharakisha kuwasilisha malalamiko kutokana na kasi ya ujenzi, kabla “magari ya makasha ya mizigo hayajaanza kuingia.”

Kwa mujibu wa barua ya TASAC, kanuni za bandari kavu zinamtaka anayekusudia kuanzisha ICD kuwasilisha eneo na mpango wa shughuli zake TASAC kwa tathmini ya awali na kupata kibali kabla ya kuanza ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya shughuli hizo.

Kwa sasa, TASAC imetaka maelezo kuhusu ujenzi unaoendelea Kisota, huku wakazi wakisubiri hatua zitakazofuata baada ya mdhibiti kuingilia kati.