Kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji kwa Umma mwishoni mwa wiki iliyopita imetembelea eneo la hifadhi ya Ngorongoro ambapo pamoja na mambo mengine imejionea vivutio vya utalii ikiwemo mchanga unaohama ambao haupatikani popote Duniani isipokuwa Ngorongoro.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Masanja Kadogosa, wabunge hao wameshauri Ngorongoro na wadau wa utalii kuongeza nguvu katika kuvitangaza vivutio tulivyonavyo kimataifa hasa mchanga huo, bonde la Olduvai, kazi zilizofanywa na watafiti mbalimbali kama Dkt. Luis na Mary Leakey, historia ya binadamu wa kale na ugundunzi wa Nyayo za Laetoli miaka milioni 3.6 iliyopita

“Ukweli ni kwamba Ngorongoro mna mtaji mkubwa wa kuingiza fedha za kigeni na watalii wengi, ni hifadhi ya aina yake, tunachowashauri ni kuongeza nguvu ya kutangaza vivutio hivi katika anga za kimataifa”, alisema mhe Kadogosa kwa niaba ya kamati.

Makamu mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka hiyo Dkt.Harriet Mtae ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania aliwashukuru wabunge hao kwa maelekezo mbalimbali yenye lengo la kuboresha utendaji kazi wa Hifadhi ya Ngorongoro na kuahidi kuyafanyia kazi.

Naibu Kamishna wa Mamlaka hiyo anayesimamia huduma za shirika Aidan Makalla aliwaeleza wabunge hao kuwa Mamlaka imedhamiria kuboresha utoaji wa huduma na sasa imeanza ujenzi wa barabara kipande cha kwanza kutoka Loduare mpaka Seneto kuelekea Golini.