Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeonya wananchi kuhusu matumizi ya vipodozi visivyo salama, likisema bidhaa hizo zinaweza kusababisha madhara makubwa kiafya, ikiwemo magonjwa sugu kama saratani.

Onyo hilo limetolewa na Meneja wa Ukaguzi na Uzingatiaji wa Sheria wa TBS, Bi.Nuru Edgar Mwasulama, ambaye amesema shirika hilo linaendelea kuimarisha udhibiti wa ubora na usalama wa vipodozi vinavyouzwa nchini.

Mwasulama ametoa wito kwa wauzaji wavipodozi kuuza bidhaa hizo katika maeneo ambayo yamesajiliwa ili kuhakikisha ubora na usalama wa bidhaa hizo.

“Tumekuwa tukikutana na bidhaa za dawa za cheti kwenye maduka ya vipodozi zikiuzwa kama vipodozi. Hilo ni kosa kisheria kwani inaweza kupelekea usugu wa dawa, hali ambayo inaweza kuathiri uwezo wa dawa hizo kutibu mgonjwa atakapohitaji matibabu baadaye, amesema.

Mwasulama amewakumbusha pia si salama kuuza vipodozi vilivyokwisha muda wa matumizi pamoja na bidhaa zenye viambata sumu ambavyo tayari vimepigwa marufuku kutumika kwani ni hatari kwa afya kwa sababu ngozi inaweza kuruhusu baadhi ya kemikali kuingia mwilini.

TBS pia imekuwa ikifuatilia matangazo ya vipodozi kwenye mitandao ya kijamii, baada ya kubaini ongezeko la maudhui yanayopotosha wananchi kuhusu matumizi na utengenezaji wa bidhaa hizo.

Ameeleza kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakitangaza mitandaoni namna ya kuchanganya bidhaa na kemikali mbalimbali na kuzifungasha kama vipodozi, jambo ambalo linaweza kuhatarisha afya za watumiaji.

TBS imewataka wananchi kuwa makini wanaponunua vipodozi na kuhakikisha wanapata bidhaa zilizosajiliwa na zenye kuthibitishwa ubora na usalama, kutoa taarifa kuhusu bidhaa za vipodozi zinazodhaniwa kuwa hazina ubora, zimepitwa na muda wa matumizi au zina viambata vilivyopigwa marufuku, ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa.