Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia ,Dodoma

Sekta ya uchimbaji mdogo wa dhahabu (ASGM) imeendelea kuwa nguzo muhimu kwa sekta ya madini nchini kwa kuchangia sehemu kubwa ya uzalishaji wa dhahabu na kutoa ajira nyingi, huku matumizi ya zebaki yakitajwa kuwa moja ya changamoto kubwa inayohitaji hatua za haraka kutatuliwa.

Hayo yamebainishwa Julai 30,2026 Jijini hapa wakati wa Warsha ya Wadau wa Mazingira na madini kupitia Mradi wa Marekebisho ya Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki unaotekelezwa na AGENDA kwa kushirikiana na IPEN.

Afisa Programu wa AGENDA, Angel Shaniva amesema sekta ya uchimbaji mdogo wa dhahabu nchini inakadiriwa kuchangia takribani asilimia 40 ya dhahabu yote inayozalishwa nchini.

Amesema sekta hiyo inachangia takribani asilimia 90 ya nguvu kazi katika sekta ya madini, jambo linaloonesha umuhimu wake katika shughuli za kiuchumi na maisha ya wananchi wanaotegemea shughuli hizo.

Amefafanua kuwa zaidi ya watu milioni 1.2 wanajihusisha moja kwa moja na shughuli za uchimbaji mdogo wa dhahabu, huku takribani watu milioni 7.2 wakitegemea sekta hiyo kwa njia isiyo ya moja kwa moja kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi.

“Pamoja na mchango huo, matumizi ya zebaki katika uchimbaji mdogo wa dhahabu yameendelea kuwa changamoto kutokana na athari zake kwa afya za wachimbaji, mazingira na jamii zinazozunguka maeneo ya migodi,”amesema.

Ameeleza kuwa shughuli za uchimbaji mdogo wa dhahabu, zebaki hutumika katika kutenganisha dhahabu na madini mengine, lakini matumizi yasiyo salama ya kemikali hiyo yanaweza kusababisha uchafuzi wa ardhi, mito na samaki pamoja na madhara kwa afya ya binadamu.

Anaeleza kuwa maeneo yenye matumizi makubwa ya zebaki nchini ni pamoja na Geita, Shinyanga, Mbeya na Mara, ambako wachimbaji hutumia kemikali hiyo katika mchakato wa uchakataji wa dhahabu.

Licha ya hayo amesema kwa upande wa ushiriki wa makundi mbalimbali katika sekta hiyo, wanawake wanatajwa kuwa kati ya asilimia 20 hadi 30 ya wafanyakazi katika shughuli za uchimbaji mdogo wa madini, huku takribani watoto 10,000 wakihusishwa na shughuli hizo.

Kutokana na hali hiyo, wadau wa mazingira na madini wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kuondoa matumizi ya zebaki na kuhamasisha matumizi ya teknolojia mbadala zisizotumia kemikali hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la mtandao kwa ajili ya maendeleo ya jamii(NESODO)Alfred Lugela,amesema miongoni mwa teknolojia zinazopendekezwa ni pamoja na njia za gravity concentration na borax ambazo zinaweza kusaidia wachimbaji wadogo kuchakata dhahabu bila kutegemea zebaki.

Lugela amesema marekebisho yanayopendekezwa katika Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki yanalenga kuweka mwaka 2032 kuwa mwisho wa matumizi ya zebaki katika uchimbaji mdogo wa dhahabu, hatua ambayo inalenga kulinda afya za wachimbaji na kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kwa misingi salama na endelevu.

Ameeleza kuwa kuimarisha matumizi ya teknolojia salama katika uchimbaji mdogo wa dhahabu kutasaidia kuongeza tija, kulinda mazingira na kuboresha maisha ya wananchi wanaotegemea sekta hiyo.

Mkataba wa minamata umetokana na Mji wa Minamata (Japani)uliopo katika Mkoa wa Kumamoto, Japani, ambao ulipata umaarufu duniani kutokana na janga la uchafuzi wa zebaki lililotokea kuanzia miaka ya 1950.

Kiwanda cha kemikali cha Chisso Corporation kilitoa maji taka yenye zebaki baharini, zebaki hiyo ikaingia kwenye samaki na viumbe vya baharini.

Watu waliokula samaki hao walipata ugonjwa mkali wa mfumo wa fahamu uliokuja kuitwa Ugonjwa wa Minamata.

Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki (Minamata Convention on Mercury)
Ni mkataba wa kimataifa uliopitishwa mwaka 2013 chini ya United Nations Environment Programme (UNEP) kwa lengo la kulinda afya ya binadamu na mazingira dhidi ya madhara ya zebaki. Mkataba huu unadhibiti uzalishaji, biashara, matumizi na utupaji wa zebaki.