Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Biashara ya mazao kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala imeendelea kushika kasi nchini baada ya wakulima kuuza zaidi ya kilo bilioni 1.122 za mazao na kuingiza Shilingi trilioni 2.298 katika mwaka wa fedha 2025/26, ikiwa ni ongezeko la asilimia 43.6 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Asangye Bangu, amesema hayo Julai 31, 2026 jijini Dodoma kuwa ongezeko hilo linaakisi kuimarika kwa matumizi ya mfumo huo, ambao umeendelea kuwapa wakulima fursa ya kuuza mazao kwa ushindani na uwazi kupitia minada ya kidijitali.
Amesema mazao tisa yaliuzwa kupitia mfumo huo, yakiwemo korosho, mbaazi, ufuta, kahawa, kakao, dengu, choroko, soya na chai, huku korosho zikiongoza kwa kiasi kilichouzwa, zikifuatiwa na mbaazi na ufuta.
Bangu amesema mafanikio hayo yamewanufaisha pia Halmashauri zilizokusanya Shilingi bilioni 61.05 kupitia ushuru wa mazao (CESS), wakati thamani ya biashara yote iliyofanyika kupitia mfumo huo ilifikia Shilingi trilioni 2.679.
Ameeleza kuwa mfumo huo umeendelea kuboresha maisha ya wakulima kwa kuwawezesha kupata bei shindani, malipo kupitia benki, kuhifadhi mazao kwenye maghala yenye viwango na kutumia stakabadhi za ghala kupata mikopo kutoka taasisi za fedha.
Kwa mujibu wa Bangu, shughuli za mfumo huo pia zilizalisha ajira 31,875 katika mnyororo wa thamani wa mazao, zikiwemo ukusanyaji, uhifadhi, usafirishaji na upimaji wa ubora, huku WRRB ikiendelea kuimarisha usimamizi wa maghala na ubora wa mazao.
Amesema mwaka 2026 ni wa kihistoria kwa WRRB kutokana na kutimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, ambao sasa unatekelezwa katika mikoa 23 na unahusisha mazao na bidhaa 18, tofauti na ulipoanza ukisimamia zao la korosho pekee.
Kwa mwaka wa fedha 2026/27, WRRB imepanga kupanua mfumo huo kwa kuingiza biashara ya mifugo pamoja na bidhaa nyingine zikiwemo mwani, ngozi na mazao ya bustani, sambamba na kuimarisha matumizi ya teknolojia na ushirikiano na taasisi za fedha ili kuongeza tija na masoko ya mazao ya wakulima.




