Wakati viongozi wa dini nchini wakisisitiza umuhimu wa kuendelea kumuomba Mungu sambamba na kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi mapya ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona, COVID-19, mjadala wa gharama za matibabu nchini umeshika kasi.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari vya Gazeti la JAMHURI; hospitali za Aga Khan, Kairuki na Rabininsia zimekuwa zikitoza kiasi kikubwa cha fedha kwa yeyote anayekwenda kutibiwa magonjwa yanayoendana na mfumo wa kupumua au anayeonyesha dalili za kuwa na magonjwa ya aina hiyo.

“Ukipeleka mgonjwa Aga Khan mwenye dalili za magonjwa ya kupumua, utatakiwa kutoa malipo ya utangulizi (advanced payment) kabla ya kuanza matibabu, vinginevyo hawampokei,” kinasema chanzo chetu cha habari.

Malipo hayo yanadaiwa kufikia hadi Sh milioni 6 kwa Aga Khan, huku vyanzo vingine vikisema zinatumika hadi Sh milioni 10 kwa wiki, Sh milioni 2 Hindu Mandal, huku Kairuki na Rabininsia zikitoza kati ya Sh 600,000 hadi Sh milioni 1.

Mtoa habari mwingine amesema: “Ni lazima ulipe kwanza. Kama huwezi, utaondoka na mgonjwa wako. 

“Wao wanadai kuwa vifaa tiba kwa ajili ya vipimo vya corona ni ghali sana na kikishatumika kwa mgonjwa mmoja inabidi kitupwe. Hiyo ndiyo sababu ya kutoza kiasi hicho kikubwa cha fedha.

“Aghalabu, wagonjwa wenye matatizo katika mfumo wa kupumua hutakiwa kuwekewa oksijeni. Hiyo nayo ni ghali. Ipo haja kwa serikali kuingilia kati na ikiwezekana itoe ruzuku kwa hospitali hizo.”

Hospitali hizo pamoja na Hindu Mandal, Regency na Mloganzila ni miongoni mwa zile zilizotajwa na serikali mapema mwaka jana kuwa maalumu kwa kulaza na kutibu wagonjwa wa corona jijini Dar es Salaam, zikiaminika kuwa na vifaa na huduma bora.

Wiki iliyopita taarifa zilizagaa katika mitandao ya kijamii zikionyesha fomu ya mkataba kati ya mgonjwa na Hospitali ya Kairuki yenye kichwa cha habari; ‘Mkataba wa malipo ya matibabu ya magonjwa ya mfumo wa hewa’.

Fomu hiyo imeainisha gharama ya Sh 600,000 kwa siku kwa mgonjwa asiyehitaji mashine ya kumsaidia kupumua (ventilator) na Sh 850,000 kwa siku kwa anayehitaji mashine hiyo.

“Kwamba, mgonjwa au ndugu wa mgonjwa au mdhamini wa mgonjwa atatakiwa kulipa malipo ya awali Sh milioni 1 wakati wa kusaini mkataba huu.

“Kwamba, malipo tajwa hapo juu hayahusiani na malipo ya dawa na vipimo,” inasomeka sehemu ya fomu ya mkataba huo.

Corona iliyotangazwa kuingia nchini kwa mara ya kwanza Machi 17, mwaka jana, ilidhibitiwa na maisha kurejea kama kawaida kuanzia Juni, mwaka huo.

Hata hivyo, vifo mfululizo vya watu mashuhuri na wasio mashuhuri vilivyoripotiwa kuanzia mwanzoni mwa mwezi uliopita vimesababisha Kanisa Katoliki kuwataka wananchi kurejea katika tahadhari kama ilivyokuwa mwaka jana.

“Corona ipo na Tanzania si kisiwa. Kwa hiyo pamoja na kumuomba Mungu, ni muhimu pia kuendelea kuchukua tahadhari kama zinavyotolewa na wataalamu wa afya,” anasema Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Juda Thadaeus Ruwa’ichi.

Rais Magufuli anena

Siku chache baada ya kauli hiyo ya Askofu Mkuu Ruwa’ichi, Rais John Magufuli akasema wapo watu waliokwenda nje ya nchi kupata chanjo ya corona ambao wameleta nchini “Corona mbaya sana.”

Akizungumza jijini Dodoma wiki iliyopita, Rais Magufuli amewatahadharisha Watanzania juu ya matumizi ya dawa za kupambana na COVID-19 zinazotoka nje. Amewataka Watanzania kutumia dawa za asili katika mapambano dhidi ya COVID-19.

Amesisitiza matumizi ya miti shamba na kujifukiza katika mapambano dhidi ya COVID-19. Pia amesema si kila dawa zinazotoka nje ya nchi ni nzuri kwa Watanzania.

“Kuna dawa inaitwa Covidol, Bugiji zinafanya kazi kwa sababu zimekuwa proved (zimethibitishwa) na Mkemia Mkuu. Kamwe msifikirie kila dawa inayotoka nje ni kwa ajili yenu… ingekuwa hivyo malaria ingeisha. Tujitambue, tusitumike. Madawa haya yalipigwa vita na wakoloni kwa sasabu ya uchumi. Ukiwa na mti wako, hata kama unaponyesha malaria utaambiwa ni wa kishamba,” amesema Rais Magufuli.

“Mungu ametupa hii mimea na ikabarikiwa, tuitumie, lakini tuitumie kwa kufuata masharti na utaalamu mzuri. Kwa hiyo taasisi yetu ya Wizara ya Afya inayosimamia dawa za asili, huu ni wakati wa kuzitumia kikamilifu. Na Wizara ya Afya isiwakatishe tamaa watu hawa, na madaktari wanatumia hizo hizo dawa, wao wanaenda wanakunywa, wanajifukiza, wakija huku wanawatwanga masindano [watu wengine],” amesema.

Amewataka Watanzania kwa wakati wote kumtanguliza Mungu na kuendelea kujilinda, hivyo wanapaswa kuendelea kuchukua tahadhari.

Shirika la Afya duniani (WHO) limetangaza mpango wa muda kuhusu nchi zitakavyopewa chanjo za corona mwaka huu, huku Tanzania na Burundi zikiwa hazimo katika orodha yake ya nchi zitakazopata chanjo.

Kwa upande mwingine, serikali inawataka wananchi kutumia chakula lishe na dawa za asili kupambana na magonjwa ya mfumo wa kupumua na kichomi (pneumonia).

Hospitali ya Kairuki wakana, Aga Khan wazungumza

JAMHURI limemtafuta Ofisa Habari na Uhusiano wa Hospitali ya Kumbukumbu ya Kairuki, Arafa Juba, kuzungumzia suala hilo na kuelezwa kuwa tayari amekwisha kulitolea ufafanuzi.

“Tumeshaweka sawa. Ni uzushi tu. Kama haujapata ufafanuzi nitakutumia kwa ‘Whatsapp’ kilichotamkwa na uongozi,” anasema.

Waraka wa ufafanuzi uliosainiwa na Arafa kuhusu mkataba wa mgonjwa na hospitali hiyo uliotumwa kwa JAMHURI unasomeka hivi:

“Taarifa za waraka uliosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuanzia Februari 2, mwaka huu SIO SAHIHI na uongozi wa hospitali unaomba wananchi waupuuze.

“Aidha, Kairuki Hospital inayo mikataba rasmi ya matibabu na taasisi mbalimbali za bima ya afya na mashirika pamoja na watu binafsi inayoelezea bayana aina za huduma na gharama zake.”

Kwa upande wa Aga Khan, wao wanakiri kuwapo kwa malipo ya awali kwa wagonjwa hospitalini hapo.

“Si kwa wagonjwa wa mfumo wa kupumua pekee, ni wagonjwa wote. Na malipo yenyewe yanatofautiana kutokana na huduma zinazotolewa,” amesema ofisa wa hospitali hiyo alipopigiwa simu na mwandishi wetu akijitambulisha kama mwananchi mwenye mgonjwa anayehitaji kupelekwa hapo.

Ofisa huyo anakiri kuwa gharama hufikia hadi Sh milioni 6.

“Kuna mambo mawili watu wanayachanganya. Vipimo vya COVID – 19 kwa mtu anayetaka kusafiri kwenda nje ni Sh 360,000; hilo ni jambo la kwanza. 

“Jambo la pili ni mgonjwa kama huyo unayetaka kumleta. Kuna gharama za kumuona daktari kwa mgonjwa wa nje na iwapo atalazwa gharama zinatofautiana kati ya wodi na wodi.

“Kwa hiyo hata advance zinatofautiana kwa ICU, wodi ya wazazi, wodi ya watoto, pia kuna wodi ya VIP hapa. Matibabu ni gharama,” anasema ofisa huyo.

Ofisa huyo anasema hakuna bima ya afya inayolipia COVID-19.

Rabininsia waruka kimanga

JAMHURI limetembela Hospitali ya Rabininsia iliyopo Tegeta jijini Dar es Salaam kutaka kujua ni namna gani wanawahudumia watu wenye matatizo katika mfumo wa kupumua na malalamiko ya wananchi mitaani.

Akizungumza na gazeti hili, Dk. Samwel Malango, anasema hospitalini hapo hakuna malipo ya advance kwa wagonjwa wenye matatizo katika mfumo wa kupumua.

“Suala hilo ni jipya sana hapa kwetu, kwa kuwa siku hizi wala hatushughuliki kupima magonjwa hayo. Ni kweli awali hospitali hii iliteuliwa kuhudumia wagoniwa wa COVID-19, lakini kwa sasa hapana, hatutoi huduma hiyo,” anasema Dk. Malango.

NHIF na magonjwa ya mlipuko

JAMHURI limebisha hodi hadi ofisi za Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) kutaka kujua sababu ya kutowalipia matibabu wanachama wake wenye matatizo katika mfumo wa kupumua.

Meneja Uhusiano wa NHIF, Angela Mziray, amesema kwa mujibu wa sera, mifuko ya bima ya afya haijihusishi na magonjwa ya mlipuko.

“Suala la kudhibiti magonjwa ya mlipuko ni la serikali. Hata COVID-19 ni miongoni mwa magonjwa hayo, ndiyo maana sisi hatulipi, kwa mfano ARVs (dawa za kufubaza virusi vya ukimwi).

“Lakini tunalipa magonjwa nyemelezi. Mtu mwenye COVID-19 akiwa anaumwa kichwa, hapo tunahusika,” anasema Angela.

Awali, Angela alitaka kufahamu iwapo hospitali washirika wa NHIF ni miongoni mwa wanaotoza ‘advance’ kwa wagonjwa.

Je, kuna uhaba wa vifaa tiba?

Kuhusu uwepo wa vifaa tiba vya kutosha kukabiliana na magonjwa yanayohusiana na mfumo wa kupumua, Ofisa Uhusiano wa Bohari ya Dawa (MSD) nchini, Benjamin Massagya, hakuwa tayari kulizungumzia.

“Hili suala (la akiba) ni la wizara na hospitali husika. Ninakushauri uende Wizara ya Afya huko utapata majibu sahihi,” anasema Massagya.

Ofisa huyo anasema kazi ya MSD ni kusambaza dawa na vifaa tiba nchi nzima.

Danadana zinaendelea

JAMHURI limewatafuta maofisa wa Wizara ya Afya kutaka kujua, mbali na kuwapo kwa vifaa tiba vya kutosha, iwapo ni halali kwa hospitali binafsi kutoza malipo ya awali kwa wagonjwa.

Hata hivyo, hakukuwa na ofisa yeyote serikalini aliyekuwa tayari kutoa majibu ya moja kwa moja, badala yake kila aliyetafutwa alimrushia mpira mtu mwingine.

Hata Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya, Dk. Leonard Subi, hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo, akimtaka mwandishi wetu kumtafuta msemaji wa wizara.

“Haya pamoja na mengine yote unayohitaji kujua utayapata kwa msemaji wa wizara. Huyo ndiye muhusika mkuu,” anasema Dk. Subi.

Msemaji Mkuu wa Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Ustawi wa Jamii, Prudence Constantine, ameliambia JAMHURI kuwa yeye anahusika na masuala ya maendeleo ya jamii wizarani hapo na kuahidi kumuunganisha mwandishi na Msemaji wa Idara Kuu ya Afya, Gerald Chami.

JAMHURI limempata Chami, ambaye amesema nao wamezisikia hizi taarifa wanazifuatilia kwa karibu, ila akamwomba mwandishi awasiliane na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Idara Kuu ya Afya, Profesa Mabula Mchembe. Hadi tunakwenda mitamboni, katibu mkuu alikuwa hajapatikana.

Hata hivyo, JAMHURI linafahamu kuwa kuna mwongozo unaoandaliwa na Wizara ya Afya, utakaoainisha kiwango cha gharama zinazotolewa kwa mgonjwa mwenye changamoto ya kupumua.

“Ndugu yangu, mimi nimekuwa daktari hospitalini na sasa nipo kwenye utawala kitambo. Tatizo tunalopata kila hospitali tukiuliza juu ya malalamiko ya hizi gharama, wanakana kutoza gharama hizo.

“Hapa suluhisho, inabidi ajitokeze mtu aliyepeleka mgonjwa akalipishwa au akadaiwa gharama hizo kwa ushahidi ashirikiane na sisi kukomesha uporaji huu. Watu hawapaswi kutumia fursa ya afya za watu kutetereka kujipatia fedha kwa njia  haramu. Gharama si kubwa kiasi hiki wanavyotaka ionekane.

“Kwa sasa kila mtu ana majibu yake. Mwingine anasema amechukua vifaa tiba kutoka China, mwingine Misri, mwingine Marekani au Uingereza, sasa kama EWURA wanavyoweka bei elekezi, hospitali zote nchini zitakuwa na bei elekezi ya gharama. Hii huria, imegeuka holela,” anasema mtoa taarifa.

Kwa nyakati tofauti, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Profesa Mabula Mchembe, ametembelea hospitali kadhaa za serikali kuona hali halisi.

Akiwa jijini Mwanza, Profesa Mchembe ametembelea hospitali za Bugando na Sekou Toure na kisha kuwatoa hofu wananchi akisema taarifa zinazozagaa mitandaoni kuhusu kuwapo kwa wagonjwa katika hospitali hizo kubwa Kanda ya Ziwa ni za kupuuzwa.

Kaimu Mkurugenzi wa Bugando, Dk. Fabian Massaga, amemwambia Profesa Mchembe kuwa wagonjwa wanaopokewa wenye shida ya kupumua inatokana na maradhi kama shinikizo la damu, uzito uliopitiliza na kifua kikuu.

Kauli hiyo haitofautiani na iliyotolewa na Mganga Mfawidhi wa Sekou Toure, Dk. Bahati Msaki. Wiki moja kabla ya kwenda Mwanza, Profesa Mchembe alitembelea hospitali za Muhimbili na Mloganzila jijini Dar es Salaam.

“Nimepita Mloganzila na Muhimbili, nimekutana na wafanyakazi na kuzungumza nao, pia kusikia changamoto zao.

“Nimejiridhisha kwamba si kila wagonjwa waliolazwa wana corona kama ambavyo inasemekana kwenye mitandao,” anasema Profesa mchembe.

Anasema kuna wenye matatizo ya upungufu wa damu, shida ya kupumua, waliopata ajali, kifafa, seli mundu na pumu.

“Dalili za hawa wote zinafanana. Wapo wanaoumwa kichwa, mafua, mwingine anashindwa kupumua kutegemea na mwili wake,” amesisitiza na kuiasa jamii kutotumia mitandao kuwaogopesha wagonjwa waliolazwa katika wodi za hospitali mbalimbali nchini.

TMDA wazungumzia ubora wa vifaa tiba

Kwa upande mwingine, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba nchini (TMDA), imethibitisha ubora wa vifaa vinavyotumika nchini.

Ofisa Habari wa TMDA, Gaudensia Simwanza, ameliambia JAMHURI kuwa vifaa tiba vyote, vikiwamo vinavyotumika kupima matatizo ya mfumo wa kupumua na COVID -19, huthibitishwa ubora na mamlaka hiyo.

“Wajibu wa TMDA ni kuhakiki ubora wa vifaa vyote vinavyohusiana na tiba kwa binadamu. Vinachunguzwa. Tunavipima kujiridhisha iwapo vinakidhi ubora stahiki kabla ya kupelekwa kwa mlaji,” anasema.

Gaudensia anasema upimaji wa vifaa hivyo huzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa kukidhi matumizi ya binadamu. 

Mbali na barakoa kutoka nje ya nchi, vifaa vingine vinavyohusiana na corona ni mavazi ya kujikinga na maambukizi (PPE), vifaa vya kuchukulia sampuli za mgonjwa pamoja na kemikali za kupimia kufahamu uwepo wa maambukizi ya ugonjwa huo.

Kilio cha wananchi wengi waliozungumza na JAMHURI, wanaomba ama serikali itoe ruzuku kwa hospitali binafsi zinazotibu magonjwa ya mfumo wa kupumua au iainishe gharama halisi badala ya kuwaacha wananchi kuachwa mikononi mwa watu wasiouishi uhalisia.

“Hapa tunaomba serikali iingilie kati. Unaweza kukuta ni kweli huu mzigo umekuwa mkubwa na haubebeki kwa hospitali binafsi au wanataka kutengeneza faida. Serikali itoe mwongozo, maana inazo hospitali na inafahamu gharama halisi za matibabu, huu ndio ufumbuzi halisi,” anasema mmoja wa wananchi aliyeomba asitajwe gazetini.

By Jamhuri