Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini, Mwalimu Mwajuma Nyamka, amesisitiza umuhimu wa kuwathamini wazee na makada waasisi wa chama hicho, akieleza kuwa wao ni nguzo muhimu katika historia, ujenzi na uimara wa CCM.
Akizungumza katika muendelezo wa ziara yake kata ya Msangani, alikokwenda kuwashukuru wananchi kwa kuiunga mkono CCM katika uchaguzi mkuu uliopita, Nyamka alitembelea mabalozi pamoja na Mkuu wa Wilaya mstaafu ambaye pia ni miongoni mwa waasisi wa chama, Kanali Mstaafu Shaban Lissu, kwa lengo la kupata mawazo na busara zake.
Amesema ni wajibu wa viongozi na wanachama wa CCM, hususan vijana, kuendelea kuwaheshimu wazee kama hazina ya hekima na historia ya chama na taifa kwa ujumla.
“Viongozi wa sasa ni muhimu kushuka chini, kusikiliza wananchi na kuwatembelea wazee ili kupata ushauri utakaosaidia kuboresha utendaji wetu,” alisema Nyamka.
Aidha, alibainisha kuwa CCM Kibaha Mjini itaendelea kuweka mikakati ya kuwatambua na kuwasaidia makada wake waliotoa mchango mkubwa katika ujenzi wa chama na taifa.
Kwa upande wake, Kanali Mstaafu Shaban Lissu alisema alijiunga na CCM mwaka 1979, akieleza kuwa siri ya chama hicho kuendelea kudumu ni kujijenga, kujitambua, uwezo wa kujikosoa na kutoa matokeo chanya.
Aliongeza kuwa kiongozi bora anapaswa kuwa na uadilifu, uzalendo, maadili, kujituma na uwezo wa kukitumikia, kukilinda na kukiendeleza chama.
Lissu aliwasihi viongozi wa CCM kutimiza wajibu wao kwa kufanya vikao kwa wakati, kuongeza wanachama wapya, kuwa na mshikamano na kuimarisha umoja wa chama.
Awali, Diwani wa Kata ya Msangani, Frank Msimbe, alieleza kwa miezi mitatu miradi mitatu ya maendeleo yenye thamani ya shilingi milioni 134, ikiwemo upatikanaji wa madawati 330 yaliyosaidia kupunguza changamoto ya wanafunzi kukaa chini.
Hata hivyo, alitaja changamoto zinazoikabili kata hiyo kuwa ni uharibifu wa miundombinu ya barabara kutokana na mvua, ukosefu wa umeme katika baadhi ya maeneo na upungufu wa huduma ya maji safi na salama.









