• JWTZ watisha, maofisa Maliasili 16 wakamatwa
  • Mmoja akutwa anamiliki bunduki 5 za rifle kali
  • Mbunge Mtutura ahojiwa, Nchambi naye atajwa
  • RCO aliahidiwa dola 3,000 akawaachia Waarabu

Operesheni Tokomeza inayoendeshwa chini ya usimamizi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), imewakamata watumishi kadhaa wa Serikali wanaotuhumiwa kujihusisha na ujangili. Operesheni hiyo inaongozwa na Luteni Kanali A. Sibuti.

Pamoja na watumishi hao, wamo pia baadhi ya wabunge waliohojiwa na wengine wakitarajiwa kuhojiwa. Miongoni mwa waliohojiwa ni Mbunge wa Tunduru, Mtutura Mtutura (CCM).

Mtutura amezungumza na JAMHURI na kukiri kuhojiwa na makamanda wa Operesheni Tokomeza. Hata hivyo, amesisitiza kuwa hajihusishi na ujangili.

Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa wabunge wengine, akiwamo Mbunge wa Kishapu, Suleiman Nchambi (CCM), watahojiwa wakati wowote kuanzia leo. Kwa upande wake, Nchambi ameliambia JAMHURI kwamba hana taarifa za kuwamo kwenye orodha ya watuhumiwa wa ujangili wanaotakiwa kuhojiwa.

 

Majina ya watuhumiwa yaanza kuanikwa

Hakuna shaka kuwa watuhumiwa wakuu wa mtandao wa ujangili nchini ni watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii wenyewe kuanzia Makao Makuu, Dar es Salaam hadi ngazi za chini kabisa wilayani na ndani ya hifadhi za taifa. Mmoja wao amekamatwa akiwa na bunduki tano aina ya rifle.


Operesheni hiyo imebaini kuwa pamoja na watuhumishi hao, mtandao wa uhalifu umeimarika hadi ndani ya Jeshi la Polisi pamoja na Mahakama.


Uvunjaji wa mtandao huo umeanzia kwa watumishi wengi wa Wizara ya Maliasili na Utalii. Afisa Wanyamapori Wilaya ya Meatu, Mohamed Ismail, anayetuhumiwa kujihusisha na ujangili, sasa amefikishwa mahakamani kujibu mashitaka.


Mohamed Hassan Kidunda ambaye ni Afisa Wanyamapori Wilaya ya Meatu, naye amefikishwa mahakamani akikabiliwa na tuhuma kama hizo.


Katika Wilaya ya Serengeti, Omary Lutiginga, ambaye ni Afisa Wanyamapori, wilayani Mugumu, naye anahojiwa kwa kujihusisha na ujangili.


Mhasibu wa Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU) Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Jail Adamson Mwakabenga, amefikishwa mahakamani kwa kukutwa akiwa na pembe mbili za ndovu.


Afisa Wanyamapori Wilaya ya Bariadi, Jesca Mathias, naye amefikishwa mahakamani baada ya kukamatwa akiwa na silaha na risasi, ngozi za chui (mbili) ngozi ya chatu, na meno ya kiboko. Silaha alizokamatwa nazo ni bunduki tano za rifle aina ya 458, risasi za shotgun 107, risasi za rifle 306 (47) na risasi moja ya Sub Mchine Gun (SMG).


Derrick Kasano Mboneka ambaye ni Mhifadhi Daraja la Pili katika Hifadhi ya Maswa, anahojiwa kwa kujihusisha na vitendo vya ujangili.


Msiba Chiraka ambaye pia ni Mhifadhi Daraja la Pili katika Hifadhi ya Maswa, naye amekamatwa akiwa na bunduki ya kivita aina ya SAR na risasi 13.


Afisa Wanyamapori Wilaya ya Meatu, Michael Andrew, naye anahojiwa akituhumiwa kujihusisha na ujangili.


Mhifadhi Daraja la Pili katika Hifadhi ya Maswa, Yasinta Modest, amekamatwa akiwa na silaha ya kazini aina ya SAR na risasi 21 nyumbani kwake.


Philimony Ntandu ambaye ni Mhifadhi Daraja la Pili katika Hifadhi ya Maswa anahojiwa kwa kosa la kujihusisha na vitendo vya ujangili.


Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa kwenye orodha hiyo wapo pia William Lugobi Peter ambaye ni Afisa Wanyamapori, KDU Arusha.


Operesheni Tokomeza imemnasa pia Deonatus Makene ambaye ni Afisa Wanyamapori Arusha. Anahojiwa kwa tuhuma za kuwasaidia wahalifu wa tuhuma za ujangili.


Afisa Wanyamapori KDU Arusha, Michael Melakiti anahojiwa kwa tuhuma kama zinazomkabili Makene.


Afisa Wanyamapori Wilaya ya Serengeti, Cuthbeth Boma, yeye amefikishwa mahakamani kwa kosa la kupatikana na pembe 10 za ndovu, tembo; meno manane ya kiboko na mikia sita ya ndovu.


Katika eneo la Ngorongoro nako Operesheni Tokomeza imeingia. Aliyenaswa ni Fredrick Flegence ambaye ni Askari Wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa ya Manyara. Anahojiwa kwa tuhuma za kuua wanyama ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).


Askari Wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa Manyara, Novatus Mosha, anahojiwa kwa tuhuma za kuua wanyama ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.


Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Makuyuni, Monduli mkoani Arusha, Bakari Salim (32), naye ni miongoni mwa waliotiwa mbaroni akiwa na kilo 40 za pembe za ndovu.


Pamoja na hao, bado majangili wengine wanalindwa na viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii. Majangili hao ni Raia wa Ugiriki Pano Canavias na raia wa Afrika Kusini, John-Martin Venter. Huyu alikamatwa mwaka 2011 na wenzake wawili, lakini aliachiwa huku magari yao yakiwa na wanyamapori waliouawa. Kwa mujibu wa jarida la The Hunting Report, Venter anaendelea kuwinda katika vitalu vya moja wa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza ulianza rasmi Oktoba 5, mwaka huu katika maeneo ambayo yamelemewa kwa matukio ya ujangili. Imegawanyika katika Kanda nne. Inashirikisha JWTZ, Polisi, Usalama wa Taifa, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), NCAA, na Idara ya Wanyamapori.

Vituko vya maafisa

Kamati inayoongoza operesheni hii imekutana navituko vya mwaka. Sheria inawataka askari wanyamapori kurejesha silaha wanazokuwa nazo wakati wa kazi na kuzisajili katika kitabu maalum, lakini operesheni imebaini kuwa silaha zote ikiwamo bunduki wanakaa nazo nyumbani kama mali zako kwa saa 24 hata siku wasizokuwa kazini.


Kilichoisikitisha kamati inayoendelea na operesheni, imebaini kuwa wengi wa maofisa hao walioshitakiwa walikuwa na tabia ya kukodisha bunduki za Serikali kwa majangili ambao walikuwa anatumia bunduki na risasi za serikali kuua tembe wanaopaswa kuwalinda.


“Kilichosikitisha wengi wamekutwa na pembe za ndofu kwenye ofisi zao na nyumbani kwao, ambazo hazikusajiliwa popote wakati sheria iko wazi kuwa wakikamata pembe za ndogu wanapima uzito na kusajili kwenye kitabu maalum kisha zinatunzwa,” kilisema chanzo chetu.


Pia chanzo kingine kilisema kuwa ilikuwa imefikia hatua ambayo maafisa wanyamapori wakikamata mtuhumiwa ana pembe za ndovu zenye uzito wa kilo 20 au zaidi, wanauza pembe hizo kisha wanatafuta pembe za tembo wadogo zenye uzito wa kilo saba au chini ya hapo na kuzihifadhi kama ushahidi wa pembe zilizokamatwa kumbe pembe halisi ziliishauzwa siku nyingine.


Baadhi ya maofisa wa polisi wasio na biashara ya aina yoyote wamethibitika kumiliki fedha na majumba makubwa wasiyoweza kuthibitisha iwapo imetokana na mishahara wanayolipwa.

RCO Arusha atorosha majangili

Uchunguzi unaonyesha kuwa Operesheni hii imewatia mbaroni raia wengi mno wa ndani na nje ya nchi, lakini mara kadhaa wanaoiendesha wamekumbana na matukio ya kuingiliwa, ama na watendaji serikalini, au wanasiasa wenye mamlaka makubwa.


Katika tukio la Arusha, raia wa kigeni wawili kutoka Saudi Arabia walikamatwa mwanzoni mwa mwezi huu. Raia hao ni Alhassan Alli Auwayship mwenye hati ya kusafiria namba IC 886898 na Nader Ali Mbooh mwenye hati namba L 381854.


Walikamatwa Loliondo baada ya taarifa za kiintelejensia wakiwa na kilo 84 za pembe za ndovu na silaha mbili. Hata hivyo, uchunguzi unaonyesha kuwa waliachiwa kwa amri ya Mkuu wa Upelekezi (RCO) Mkoa wa Arusha wa Arusha, Duani Nyanda akishirikiana na msaidizi wake kutoka katika Kituo Kikuu cha Polisi Arusha Mjini, OCD Ngonyani.


Taarifa zinaonyesha kuwa watuhumiwa hao walitakiwa kuachiwa kwa sharti kuwa wangetoa dola 3,000 (Sh milioni 4.8) kwa kamanda huyo wa polisi ili awaachie watuhumiwa hao. Dola moja ya Marekani ni shilingi zaidi ya 1,600.


Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa baada ya kuachiwa, hati za kusafiria zilibaki kituoni ila baada ya muda na kwa maelekezo ya vigogo walirudishiwa na hivyo kuwafanya watoroke.


Walioshiriki kuwawekea dhamana ni Salum Islam Salehe, ambaye ni raia mwenye asili ya Kiarabu. Kwa mjini Arusha, Salehe anajulikana kwa jina maarufu la “Kichwa”. Inadaiwa kuwa huyo ndiye aliyefanikisha kutoroka kwa watuhumiwa hao.


Salehe imebainika kuwa ni wakala wa kupokea wageni kutoka nje ya nchi na kufanya mipango ya kuwinda. Kazi hiyo ameifanya kwa muda mrefu.


Oktoba 7, mwaka huu Salehe akiwa na wenzake, Shafii Firozi Dalla (ambaye ana asili ya Kiasia), Gerald Kashiro Joseph ambaye ni Mtanzania, walikamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na uwindaji haramu.


Hata hivyo, mtuhumiwa Salehe hadi jana taarifa zinaonyesha kuwa alikuwa hajaandikiwa hati ya mashitaka, jambo ambalo lilionekana wazi kuwa kulipangwa aachiwe bila kuchukuliwa hatua za kisheria.

Watuhumiwa ni wengi mno

Taarifa kutoka ndani ya Operesheni hiyo zinasema kuwa idadi ya watuhumiwa wanaokamatwa pamoja na zana zao ni kubwa mno.


“Tunakamata bunduki za kivita ambazo hatujawahi kuziona hapa Tanzania , zina darubini na hiyo inathibitisha kuwa wana uwezo wa kumlenga na kumuua tembo akiwa mbali kabisa.

“Ukubwa wa janga hili la ujangili unawafanya viongozi wetu wanuie kuomba waongezwe muda ili kuendelea kutokomeza majangili haya, kama hali hii ingeachwa, nakuhakikisha ndani ya miaka mitano Tanzania isingekuwa na tembo wala mnyama yoyote porini,” kimesema chanzo chetu.


Habari ambazo hazijathibitishwa zinasema Amiri Jeshi Mkuu Rais Jakaya Kikwete ameamua kuongeza muda wa Operesheni hiyo. Hadi sasa Serikali haijapokea msaada wa kifedha kutoka nje kufadhili operesheni hii. Fedha zote za operesheni zinatoka Hazina ya Tanzania .

JAMHURI lilikuwa la kwanza kuandika kuanza kwa Operesheni Tokomeza katika toleo lake namba 104. Hata hivyo, viongozi kadhaa wa Wizara ya Maliasili na Utalii walikanusha jambo ambalo tayari Rais Kikwete alishautangazia ulimwengu wakati akiwa Marekani.


Baada ya Operesheni Tokomeza kuzinduliwa, kilichofuata ni kusambazwa kwa askari katika mapori mbalimbali, wakianza na yale yaliyoandamwa mno na majangili. Kati ya mapori hayo ni Pori la Akiba la Selous ambalo linajulikana miongoni mwa majangili kama ‘shamba la bibi.’


Kamati ya Bunge: Tembo wanakwisha

Kamati ya Kudumu ya Bunge imesema ujangili dhidi ya tembo kwa sasa ni janga la kitaifa.

“Ni ukweli usiofichika kwamba leo hii si tu tembo wanauawa, bali wanateketezwa. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), taarifa zinazoshabihiana na za utafiti wa kimataifa zinaonesha kwamba tembo wasiopungua 30 wanauawa kwa siku, tembo 850 wanauawa kwa mwezi, na tembo 10,000 wanauawa kila mwaka (TAWIRI 2011).


“Kutokana na kasi kubwa ya kuuawa kwa tembo, taarifa za kitaalamu kutokana TAWIRI zinathibitisha kwamba idadi ya tembo imepungua kutoka 109,000 mwaka 2009 hadi tembo chini ya 70,000 mwaka 2012.


“Endapo kasi hii ya ujangili wa tembo itaendelea bila kudhibitiwa mara moja, ni wazi kuwa tembo watakuwa wametoweka nchini katika kipindi cha miaka saba ijayo,” imeonya Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kahama, James Lembeli.


Kamati hiyo imeongeza kusema, “Hali hii ni hatari na aibu kwa nchi yetu ambayo ni ya pili barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya tembo. Kinachosikitisha ni kwamba Wizara imekuwa na kigugumizi katika kuitikia kauli ya Rais Jakaya Kikwete iliyoitaka Wizara kuomba msaada kwake kama tatizo la ujangili limewashinda. Jambo hili linaweza kutafsiriwa kuwa ni hujuma inayofanywa na baadhi ya watendaji wa Wizara ambao wamepuuza kauli ya Mheshimiwa Rais.”


Kamati inapendekeza kufanywa kwa Operesheni kama Operesheni Uhai kwa nchi nzima kama ilivyofanya miaka ya 1980. Pia imependekeza Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 ifanyiwe marekebisho kwa kuweka adhabu kali kwa watu watakaothibitika kuhusika na ujangili, hasa wa tembo.

 

2555 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!