Chimbuko migogoro ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) unasababishwa migongano wa kupata madaraka ndani ya chama hicho, JAMHURI limebaini

Imelezwa kuwa mtafaruku uliotokea mwishoni mwa wiki na kusababisha kusimamishwa kwa Mwenyekiti wa  Mkoa wa Arusha wa Chadema  kwa muda usiojulikana ni mgongano wa kutafuta madaraka ndani ya chama hicho.

Makundi mawili hasimu ndani ya chama hicho yako vitani kuhakikisha kila kundi linashika nafasi nyeti ndani ya Chadema .

 

Mwigamba anatuhumiwa kuwatuhumu viongozi wa wakuu wa Chadema kwa kuandika maneo haya;

 

Kufuatia malumbano yanayoendelea kwenye vyombo vya habari na madhaifu mengi ambayo tumeshayashuhudia kwenye chama kwa sasa, natoa wito kwa wana CHADEMA wote nchini kwamba wakati umefika tubadilishe uongozi wa juu wa chama.


Kihistoria, CHADEMA kati ya mwaka 2005 na 2010, agenda zetu kwa wananchi zilikuwa mbili. Kupiga vita ufisadi, iliyosukumwa sana na Dr. Slaa na ile ya utetezi wa raslimali zetu iliyobebwa na Zitto. Lakini sasa hivi chama kinaenda kwa matukio.


Naandika nikiwa mwana CHADEMA safi na nataka kila mwanachama atakayesoma atulie na kutafakari. Hili siyo jambo la ushabiki. Ni mawasiliano baina yetu wana CHADEMA na tunahitaji tutulie na kutafakari.


Nimekuwa mwanachama wa siku nyingi na nimebahatika pia kuwa kiongozi ndani ya chama kwa nyakati tofauti kwahiyo naelewa ninachokiandika. Nadriki kusema kwamba kwa sasa chama kinakwenda kwa matukio na ni bahati tu kwamba CCM inaendelea kutupatia matukio lakini CCM na serikali yake wakitunyima matukio, CHADEMA chini ya Mkt Mbowe, Katibu mkuu Slaa na Naibu Zitto utakuwa ndo mwisho wake.


CHADEMA iliyopiga kelele sana dhidi ya ufisadi, CHADEMA iliyopiga kelele mpaka sheria ya vyama vya siasa ikabadilishwa na vyama kutakiwa kukaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), eti leo inaungana na CCM kumshambulia mwenyekiti wa kamati ya bunge ya hesabu za serikali (PAC) kwa kutamka kwamba vyama havijawasilisha ripoti zake za fedha zilizokaguliwa. Kwa nini? Muungano huu wa CHADEMA na CCM maana yake nini? Kama chama kinajiamini ni kisafi kwenye hesabu zake hofu ni ya nini? Si wasubiri kikao na kamati ya bunge katibu mkuu aende na hizo ripoti na nyaraka zinazoonyesha kweli wamewasilisha hesabu hizo?


Napenda kabla sijaendelea mbele kuwapongeza wenyeviti wetu wawili wa kwanza ambao kimsingi waliweka msingi mzuri sana wakutong’ang’ania madaraka na badala yake kuachia mapema na kumwachia mwingine kidemokrasia bila vurugu. Hawakuwa madikteta na nawapongeza sana. Walijitahidi sana kutokuwa wapenda madaraka na kimsingi walituwekea utamaduni ambao walitaka wote tuufuate na kujenga taasisi imara inayojali demokrasia na haki ya kilamwanachama.


Ni kwa msingi huo waliamua kuandika kabisa katika katiba yetu kwamba kiongozi yeyote katika ngazi yoyote ya kuchaguliwa atakapogombea na kushinda ataongoza kwa kipindi kimoja cha miaka mitano na kisha ataweza kugombea nakuongoza kwa kipindi cha pili cha miaka mitano baada yapo hawezi kugombea tena katika nafasi ile ile aliyoitumikia kwa vipindi viwili. Ili kuonyesha kwamba walimaanisha kile walichokisema, wote wawili hawakuwahi kukaa madarakani kwa vipindi viwili vilivyoruhusiwa katika katiba bali wote wawili walikaa kipindi kimoja kimoja tu.


Napenda pia kumpongeza mwenyekiti aliyepo madarakani, Mbowe. Kuna mengi kakifanyia chama. Kakitoa kutoka kwenye chama cha tatu ama nne kwa upinzani hadi kuwa cha kwanza na kustahili kuitwa chama kikuu cha upinzani. Kakichukua kikiwa na wabunge 5 bungeni na leo katika kipindi chake cha miaka 10 kina wabunge 49. Ni achievement kubwa! Si hivyo tu, ni wakati wake CHADEMA imebeba agenda nzito za kitaifa kama vile vita dhidi ya ufisadi, utetezi wa raslimali, katiba mpya,nk.


Lakini kuna matatizo yameanza kujitokeza na tusipochukua hatua haraka huko mbele tunaweza kupata shida kubwa. Ni muhimu kwa Mbowe kuelewa kwamba uwezo wake umefikia hapo asitake kulazimisha kusonga mbele akidhani bila yeye hakuna CHADEMA. Akiache chama kikiwa salama, abaki kama mwenyekiti mstaafu na awaachie wengine awamu inayofuata ya kuingia madarakani. Kama hataki kuwa mwelewa na kuachia ngazi, wanachama tumsaidie kwa kumpiga chini uchaguzi ujao.

 

Leo nitaainisha mambo machachetu yanayohusiana na fedha za chama na uaminifu ili wanachadema muelewe kwa nini viongozi wakuu wa chama wamehamaki sana kusikia wanatakiwa kuwasilisha ripotiza fedha wakajikuta wanapambana na mwenyekiti wa kamati ya bunge badala ya kamati na hata kufikia kusahau kwamba huyo mwenyekiti wa kamati ya bunge ni mwenzao, ni naibu katibu mkuu wa chama. Mengine nitaendelea kuyadondoa siku nyingine nitakapopata fursa:

1. Wakati tukifanya mabadiliko ya katiba mwaka 2006 hatukugusa kipengele kinachomzuia kiongozi kuongoza kwenye nafasi moja kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitanomitano. Lakini wakati katiba inachapwa chini ya uongozi uliopo, kipengele hicho kiliondolewa kinyemela. Mambo yanayotokea hivi leo yanaonyesha dhahiri kipengele hicho kiliondolewa kwa makusudi kwa maslahi na kwa faida ya viongozi waliopo madarakani kwa sasa. Hiki kinaweza kuchukuliwa kama kitendo kidogo lakini kama viongozi wetu wanaweza kutokuwa waaminifu katika jambo kama hili, ni dhahiri hawawezi kuaminika na wanaweza kufanya mambo mengine makubwa na yenye athari zisizomithirika kwa chama.


Ni muhimu wanachadema mkafahamu kwamba kitendo cha kuondolewa kwa kipengele hicho ndicho kinacholeta mpasuko leo kwenye chama unaotokana na Mbowe na Zitto kupigania uenyekiti. Kama kingekuwepoleo Mbowe alikuwa anakatazwa na katiba kugombea kipindi cha tatu na hivyo vita iliyopo kati yake na Zitto isingekuwepo na chama kingekuwa imara zaidi. Ni dhahiri Mbowe aliondoa kipengele hicho kwa makusudi ili aweze kuendelea kugombea bila mwisho na huu ni udikteta kama ule tu wa akina Lyatonga Mrema, John Cheyo na wengineo, na wanachadema hatupaswi kuuruhusu si kwa Mbowe tu bali kwa yeyote atakayepata nafasi ya kuwa mwenyekiti wa chama chetu.

2. Matumizi ya fedha za chama:

Hakuna mtu anayejua hivi sasa fedha za chama zinatumikaje zaidi ya kakikundi ka watu watatu yaani Mwenyekiti Taifa, Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Fedha. Maamuzi ya vikao hayaheshimiki tena na mabwana hawa. Baada ya uchaguzi wa 2010 vikao halali vilielekeza kiasi na aina ya fedha ambazo hazitaguswa bali zitunzwe kwenye akaunti maalum kwa ajili ya uchaguzi wa 2015. Lakini leo si tu akaunti hiyo haina fedha bali hakuna akaunti yoyote yenye fedha. Watu watatu ndo wanaamua fedha zitumikeje. Mfano mwingine ni maamuzi ya kikao cha Baraza kuu cha mwezi January kilichoamua kwamba kiasi cha fedha inayotoka serikalini kipelekwe kwenye mikoa, wilaya namajimbo na kiasi kingine kipelekwe kwenye kanda. Leo ni mwezi wa 10 maamuzi hayo hayajatekelezwa ipasavyo.


Nyinyi viongozi wa kanda, mikoa, wilaya na majimbo ni mashahidi wa hili . Lakini kuna michango ya watu binafsi kama Mzee Sabodo, hizo nazo hazijulikani zimechukuliwa lini kwa mfumo gani, zikatunzwa wapi na hatimaye zimetumikaje. Hapo sijataja fedha zinazopatikana kutoka kwenye fundraising events mbalimbali kama ile ya Dar es Salaam na Mwanza. Hizo nazo hazijawahi kuonekana na walioendesha hizo fundraising, uaminifu wao kwenye masuala ya fedha ni questionable.

3. Taarifa za fedha

Tokea baada ya uchaguzi wa 2010 mpaka leo, hakuna kikao chochote kilichowahi kupokea na kujadili hadi mwisho ripoti ya mapato na matumizi ya fedha za chama. Kila kikao agenda hiyo inarushwa kiaina. Wanaojua mchezo huo ni watu watatu tuniliowataja hapo juu na malengo ya kurusha hiyo agenda kila wakati na kukwepesha isijadiliwe pia wanayajua wao. Ni dhahiri tukiendelea na hawa watu tutafika 2015 tukiwa hatuna pesa hata ya kuweka mawakala kwenye vituo na tutapigwa tukiwa tumesimama.

4. Mipango ya kukipatia chama mapato ya ziada kutoka nje ya chama

Wakuu waliopo hawana hata ndoto ya namna ya kupata fedha za ziada. Wanachokijua ni kukusanya ‘sadaka’ kwenye mikutano ya hadhara na kuwapatia kazi watu wanaoonekana kuwa matapeli eti waendeshe harambee za kuchangisha fedha kwa njia ya matukio. Mawazo mazuri kama la kuanzisha kampuni la uwekezaji la chama litakalowekeza kwenye miradi mbalimbali, halijawahi kufanyiwa kazi, nahivyo uanzishaji wa miradi mbalimbali ya kuiingizia taasisi fedha imebaki ndoto ya mchana. Hatuwezi kufika hata siku moja bila fedha. Hata uchaguzi wa wenzetu wa Kenya juzi juzi wakuu wetu ingawa walishiriki lakini hawaonekani kama wamejifunza chochote.

5. Matumizi mabaya ya madaraka yanayoweza kuhusishwa na ufisadi

Chama chetu kinayo kamati yass tenda ambayo iko chini ya sekretariat. Lakini kamati hii haifanyi kazi imezimwa kimya kimya na wajumbe wote wa kamati ya tenda kwa kuwa ni wachumia tumbo wanaojigonga kwa wakuu,wamekubali kuzimwa. Leo ikidaiwa kamati hiyo ilete nyaraka za mchakato wa manunuzi ya magari, pikipiki, kadi za uanachama, set ya televisheni iliyofungwa ofisini kwa katibu mkuu, hawana. Manunuzi haya yote yanafanywa na wakuu bila utaratibu wowote jambo ambalo ni hatari na linarahisisha matendo ya kifisadi. Hivi tunavyoongea, ni mwenyekiti taifa mwenyewe ndiye aliyenunua magari na pikipiki zote za M4C.


Hivi tunavyoongea kuna shilingi milioni 80 ambazo Mwenyekiti Taifa alizichukua na kuagiza kadi za uanachama tangu mwaka jana mpaka leo hizo kadi hazijawahi kuonekana. Na mwenyekiti anafanya mambo hayo yote akitambua kwamba yeye ni mwenyekiti na hayo ni masuala ya kiutendaji ambayo yako chini ya katibu mkuu kama mtendaji mkuu wa chama na kamati yake yatenda. Huu si ufisadi ni nini?


6. Makubaliano ya kifisadi na mtu binafsi anayeuza vifaa vya uenezi vya chama

Hakuna kikao chochote cha juu kilichojadili ama kilichowahi hata kupewa taarifa tu kwamba sasa kuna mtu binafsi kapewa tenda ya kuuza vifaa vya chama na chama kinanufaika vipi namauzo hayo na kwa nini vifaa muhimu vya chama kama bendera vinauzwa na mtu binafsi. Jambo hili linajulikana kwa Mwenyekiti Taifa na Katibu Mkuu wake tu.


Napenda kwanza kuipongeza kamati ya bunge kwa kuvikomalia vyama vinavyopokea ruzuku bila kujali ni chama tawala ama upinzani.


Pili namshauri CAG unaweza kutumia kampuni binafsi kwenye wizara, idara, taasisi, wakala, na asasi zote za kiserikali na serikali za mitaa kwenye ukaguzi lakini kamwe usiruhusu vyama vya siasa vikaguliwe na kampuni hizo. Hapo nenda mwenyewe ndo utajionea mwenyewe. Kampuni binafsi kwenye vyama huko zinafundishwa ziandikeje maoni yao. Nenda mwenyewe ujionee.


Pia kuna mkakati unaendeshwa na CHADEMA Makao Makuu kwa sasa wa kuwapigia simu viongozi wa mikoa hasa hapa Dar es Salaam na mikoa mikubwa kama Mwanza, Arusha, Mbeya, nk, wakiwataka viongozi wa mikoani mtoe matamko kumpinga Zitto.

 

Kataeni ushenzi huu. Hili si jambo la Zitto ni la kamati ya bunge na kimsingi ni la uadilifu ndani ya serikali na vyama. Hata kama jambo lenyewe lingekuwa limeagizwa na Mwigulu Nchemba msingetoa matamko ya kupinga zaidi ya kuwaacha viongozi wetuwakuu watoe ripoti kuthibitisha uadilifu wao japo kidogo maana ni ukweli pia kwamba kwenye ripoti wanaweza kuzuga zikawa safi lakini ufisadi umefanyika. Kama ni matamko toeni matamko ya kuutaka uongozi wetu utoe hizo ripoti, na hapo ndipo mtakapojua kwanini hampati ruzuku. Kuna matumizi mengi sana ya hovyo na ufisadi mkubwa unafanyika hapo Makao Makuu.


Nitaendelea kuwadondolea ili muonekwa nini napendekeza tuung’oe uongozi huu chini ya Mbowe.


Mkurugenzi wa Habari na Uenezi Taifa, John Mnyika, akijibu hoja hizo amesema,

Nimeitika mwito, ni kweli nilikuwa mjumbe kwenye timu zilizohusika na kuandikwa kwa katiba mpya ya CHADEMA ya mwaka 2006, aidha nilikuwepo kwenye mkutano mkuu wa chama uliopitisha katiba mpya tarehe 13 Agosti 2006.


Madai ya kwamba “Wakati tukifanya mabadiliko ya katiba mwaka 2006 hatukugusa kipengele kinachomzuia kiongozi kuongoza kwenye nafasi moja kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano mitano. Lakini wakati katiba inachapwa chini ya uongozi uliopo, kipengele hicho kiliondolewa kinyemela”; hayana ukweli kwa kadiri ya ufahamu wangu.


Mosi, mwaka 2006 hatukufanya marekebisho ya katiba bali tuliandika upya katiba ya chama kutoka ile ya mwaka 2004. Waraka uliandikwa nchi nzima kwa wanachama kutoa maoni na kuwasilisha makao makuu kuanzia kwenye ngazi zao za chini za kikatiba.


Baada ya kukusanya maoni kulikuwa na timu tatu, timu moja ilihusu kuandika falsafa na itikadi ya chama ambayo Mwenyekiti wake alikuwa Profesa Baregu na katibu wake nilikuwa mimi.


Sehemu hiyo ya katiba niliandika neno kwa neno mapendekezo ya awali kwa kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa, tulifanya mapitio pamoja na Profesa Baregu na hatimaye ikaingia kwenye vikao vya kikatiba vya chama na kupitishwa.


Sehemu ya falsafa kwa sehemu kubwa tulinukuu kwenye katiba kama ilivyokuwa mwaka 2004, sehemu ya itikadi tuliandika upya kabisa haikuwepo katika katiba ya CHADEMA ya zamani.


Sehemu zingine katika katiba kwa sehemu kubwa kazi ya kuunganisha maoni mapya na kufanya pia rejea kwenye katiba ya zamani ilifanywa na timu ya watu watatu tukiongozwa na muasisi wa chama Mzee Victor Kimesera pamoja na Mkurugenzi Benson Kigaila na mimi.


Kulikuwa na timu nyingine ya kuandaa miongozo ya mabaraza ya chama: Baraza la Wazee, BAVICHA na BAWACHA ambao nao walifanya kazi kwa upande wao na nilishiriki katika kupendekeza mwelekeo na  mapitio ya kulinganisha rasimu ya miongozo yao na rasimu ya katiba ya chama.


Kwa ninavyokumbuka hicho kinachoitwa  “kipengele kinachomzuia kiongozi kuongoza kwenye nafasi moja kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano mitano” hakijawahi kuingizwa kwenye katiba mpya ya CHADEMA.


Baada ya timu zote kufanya kazi yake; rasimu ya katiba ilipita katika vikao vyote vya kikatiba yaani sekretariati, kamati kuu, baraza kuu na hatimaye mkutano mkuu. Katika vikao vyote hivyo, iwapo kipengele hicho kingekuwa kimeondolewa ‘kinyemela’ kama inavyodaiwa, mwandishi wa tuhuma hiyo angehoji toka Agosti 2006.


Aidha, baada ya katiba kupitishwa na kuanza kutumika kifungu hicho kingekuwa kimeondolewa kinyemela kati ya mwaka 2006 mpaka 2008 mtoa madai au mtu mwingine yeyote ndani ya chama angekuwa amehoji wakati wa matumizi. Kumekuwepo pia mchakato wa kufanya marejeo kwa ajili ya kushughulikia makosa ya uchapaji (errata) kwa nyakati mbalimbali, suala hili si kati ya mambo yaliyoibuliwa.


Mwaka 2009 CHADEMA kilifanya uchaguzi mkuu wakae mkuu nchi nzima ambapo vifungu vya masuala ya uchaguzi wa ndani ya chama vilifanyiwa rejea mara kwa mara. Mwandishi wa madai hayo alikuwepo wakati huo, suala hili la kwamba kuna kifungu kimeondolewa kinyemela sikulisikia likilalamikiwa kwenye vikao vyovyote vya kikatiba iwe ni sekretariati, kamati kuu, baraza kuu na mkutano mkuu.


Kwa vyovyote vile kwa historia ya chama toka mwaka kilipoanzishwa mpaka wakati huo wa uchaguzi wapo viongozi ambao walikuwa wanagombea wakiwa na vipindi viwili wakati huo kwenye cheo kimoja cha ngazi moja; kifungu hicho kingekuwepo toka 2006 kingetumika kuwawekea mapingamizi. Na kama kingekuwa ‘kimeondolewa kinyemela’ kungekuwa na malalamiko mengi kiko wapi kwa kuzingatia ‘joto’ la uchaguzi wa wakati huo.


2010 mpaka 2013 madai hayo hayajawahi kutolewa kwenye kikao chochote cha kikatiba katika ngazi ya taifa kwa kuwa mimi ni mjumbe wa vikao vyote vya kitaifa ambavyo yeye amesema kwamba ni mjumbe.


Madai kama hayo yangetolewa na asiye mwanachama au walau mwanachama wa kawaida tungesema tu ni maoni ya kawaida yaheshimiwe na aelimishwe. Lakini madai kama hayo yakitolewa na kiongozi wa chama mwenye nafasi ya kuujua ukweli wote huo yanaacha maswali kuhusu dhamira yake. Naamini mamlaka zinazohusika za chama zitatumika katiba, kanuni, maadili na itifaki kuchunguza na kuchukua hatua kuanzia kwenye ngazi yao huko tukio lilipotokea.


Hata hivyo, kwa maoni binafsi (yasichukuliwe kuwa ni kauli ya nafasi ninazoshikilia kwenye chama), dhamira ya haya inajionyesha kwenye andiko lenyewe la muhusika kuanzia aya ya kwaza “ Kufuatia malumbano yanayoendelea kwenye vyombo vya habari namadhaifu mengi ambayo tumeshayashuhudia kwenye chama kwa sasa, natoa wito kwawana CHADEMA wote nchini kwamba wakati umefika tubadilishe uongozi wa juu wachama.


Mtoa madai anaendelea kuandika kwamba “ Ni muhimu wanachadema mkafahamu kwamba kitendo cha kuondolewa kwa kipengele hicho ndicho kinacholeta mpasuko leo kwenye chama unaotokana na Mbowe na Zitto kupigania uenyekiti. Kama kingekuwepoleo Mbowe alikuwa anakatazwa na katiba kugombea kipindi cha tatu na hivyo vita iliyopo kati yake na Zitto isingekuwepo na chama kingekuwa imara zaidi. Ni dhahiri Mbowe aliondoa kipengele hicho kwa makusudi ili aweze kuendelea kugombea bila mwisho na huu ni udikteta kama ule tu wa akina Lyatonga Mrema, John Cheyo na wengineo, na wanachadema hatupaswi kuuruhusu si kwa Mbowe tu balikwa yeyote atakayepata nafasi ya kuwa mwenyekiti wa chama chetu.


Anaendelea kuandika madai mengine mengi ya upotoshaji lakini  mwishoni anamalizia kwa dhamira yake ile ile “ Nitaendelea kuwadondolea ili muonekwa nini napendekeza tuung’oe uongozi huu chini ya Mbowe.”. Kwa hiyo, dhamira yake ni uchaguzi na mabadiliko ya uongozi; dhamira yeyote njema ifuate mkondo wa katiba, kanuni, maadili na itifaki; kinyume chake ni ‘njama ovu’ na ‘utovu wa maadili”.


Nimekuwepo chaguzi mbili kuu za CHADEMA 2004 (nikiwa mtazamaji sio mwanachama) na 2009 nikiwa katikati ya chaguzi hizo kama kiongozi. Naamini uchaguzi huu wa chama ulioanza kuanzia mwaka huu 2013 utakamilika mwaka 2014 CHADEMA ikiendelea kusimamia dhima yake ya kuleta uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganizesheni thabiti kwa maendeleo endelevu ya nchi yetu.


Mogogoro wa kuwania madaraka ndani ya chama hicho kwa mara ya kwanza ulianza mwaka 2008 wakati Marehemu Chacha Wangwe alipotangaza kugombea nafasi ya uenyekiti ndani ya chama hicho.


Hatua hiyo ya Marehemu Wangwe kutangaza kugombea nafasi hiyo ilizua majadala na hatimaye kuzua mzozo wa ndani ya chama hicho hali uliotishia uhai wa chama hicho.

Hata hivyo ndoto za  kushika nafasi hiyo kwa marehemu Wangwe ambaye alitoa upinzani mkubwa kwa Mwenyekiti wa sasa, Freeman Mbowe zilikatishwa na ajali ya gari ilitokea Julai 2008 na kuchukua uhai wake.


Hata hivyo baada ya kufariki kwa Wangwe kiti hicho cha kugombea nafasi hiyo kilishikwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zitto Kabwe.


Hatua hiyo ilizua mgogoro mkubwa ndani ya chama hicho kati ya wanachama  wanaomkubali Zitto na wale wanaomkubali Mbowe.


Hata hivyo kupitia baraza la wazee lilimuamuru Zitto kuondoa jina lake katika uchaguzi huo.


Jina la Zitto liliondolewa kwa madai ya kuwa bado umri wake ni mdogo kushika madaraka hayo ndani ya chama licha ya kuwa ya kuungwa mkono na wanachama wengi.


Taarifa zilizopo kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa huo ulikuwa mwisho wa urafiki kati ya Mbowe na Zitto waliopigania kufa na kupona usiku na mchana kukijenga chama hicho.


Hata kurudi kwake kwenye nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Chadema kulitokana na busara za wazee, kwani Mbowe hakumtaka kabisa Zitto aendelee kuwa na madaraka ya juu katika chama.


Katika hotuba yake kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema, Mbowe hakuficha kutamka wazi kuwa alinyanyaswa vya kutosha, na kwamba baada ya kuchaguliwa kwa mara nyingine kuwa mwenyekiti, alikuwa na uamuzi wa kuamua nani awe nani ndani ya chama hicho.


Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini na kuthibitishwa na mmoja wa kiongozi mwandamizi wa chama hicho kwamba mzimu wa Marehemu Wangwe bado utaendelea kukitafuna chama hicho iwapo hakitafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.


Kiongozi huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini kwa sababu za kiusalama  amesema kuwa ndani ya chama hicho hakuna demokrasia ya kweli.


Amesema inashangaza kuona kuwa siku zote viongozi wa chama hicho wamekuwa wakihubiri demokrasia lakini hawaitendi kama wanavyoihubiri katika majukwaa.


Amesema bila kufanya hivyo kamwe hakutakiondoa Chama Cha Mapinduzi  madarakani.

Amesema mbali na Chadema kuendeshwa kibabe hata vyama vingine kama CUF, NCCR Mageuzi na TLP navyo vinaendeshwa bila kufuata kwa misingi ya kidemokrasia.


Ametoa mfano kuwa katika Chama cha CUF ni vigumu kumsema vibaya au kumpinga na kwa hoja na Maalimu Seif Hamad na iwapo utabainika kufanya hivyo utapewa adhabu ya kufukuzwa ndani ya chama hii yote inatokana na ubinafsi ndani ya vyama hivyo.


Amesema mambo hayo yako katika vyama vya NCCR Mageuzi na TLP.


“Leo hii ukitangaza kumpinga Mbowe kwa hoja yeyote tayari umejitangazia vita ndani ya chama hicho kama si kufukuzwa basi utatengwa kushirikishwa katika maamuzi yote ya chama.


“Mfano mzuri ni Zitto Kabwe ambaye alitangaza kugombea uenyekiti ndani ya chama hicho hadi leo ametelekezwa na chama  maamuzi yote yanayotolewa na chama  wanaojua ni wakina Mrema  na wengine wanaomtii Mbowe sasa amekuwa kama mtoto mkiwa ndani ya chama anafichwa kila kitu kinachofanyika ndani ya chama,” amesema kiongozi huyo na kuongeza kuwa.


“Hata katika uongozi wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere alipingwa lakini hakuwahi kumfukuza kazi mtu au kumtenga alipingana kwa hoja na si kama ilivyo katika vyama hivi vinavyojiita vya upinzani,” amesema.


Amesema kuwa hadi sasa Chadema imegawanyika vipande viwili kimoja kinachomuunga mkono, Zitto Kabwe na kingine kinachomuunga mkono Mbowe.


Kiongozi huyo amesema kuwa vyama hivyo sasa vimekuwa kama Vyama vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) kwani kila anayeingia madarakani hataki kuondoka kutokana  na maslahi anayoyapata ndani ya chama huska.


Amesema inashangaza kuona CCM ambayo wamekuwa wakiilaumu kuwa imeshindwa kuongoza lakini kwa kiasi fulani ina demokrasia ndani kutokana na  wenyeviti wake kuachiana madaraka kila baada ya kipindi cha miaka kumi.


“Hivi angalia Maalimu Seif amekuwa Katibu wa CUF tangu ilipoanzishwa wakati huo Mwenyekiti wa CCM alikuwaRais Ali Hassan Mwinyi akaja Rais Benjamin Mkapa sasa Rais Jakaya Kikwete lakini katika vyama vya upinzani ni wale wale ukihoji unaambiwa umevunja kanuni za chama wanakufukuza.


“Kama wapinzani hatutakaa pamoja na kuangalia ni wapi tunakosea hatuwezi kushika dola hata siku moja leo matatizo yaliyoko CUF, NCCR Mageuzi TLP   ni sawa  yale yalipo Chadema, vyama hivi vimejaa ubinafsi,” amesema.


Amesema viongozi hao wasijidanganye kuwa wanaongoza mabadiliko nchini wakati ndani ya vyama vyao wameshndwa  wanaongoza hayo  mabadiliko ni wananchi wa kada za chini kwani wao kweli wanahitaji mabadiliko ndio yanafanya vyama hivyo vionekane kuwa viko mbele na si viongozi.


Amesema Mbowe yuko nyuma ya mabadiliko lakini wanachama wa kawaida wako mbele kutaka mabadiliko na wanajua wanataka nini si kama Mbowe.


Amesema ndani ya chama hicho hakuna uhuru wa kujieleza hata kama una hoja muhimu ya kujenga chama lakini ikiwa inapingana na mawazo ya Mbowe tayari umetangaza mgogoro naye.


Akizungumzia tukio la wanachama na viongozi wa chama hicho kupigana kiongozi huyo amesema kuwa huo ni moja muendelezo wa makundi hayo mawili ndani ya Chadema.

Amesema kuwa ni moja ya njia ya Mbowe ya kutaka kuidhoofisha kambi ya Zitto ndani ya Chadema.


Amesema  hoja iliyotolewa na Samson Mwigamba  ndani ya mtandao wa Jamiiforum iwe ni kweli au si kweli kuwa ndiye aliyeandika, ni uhuru wake wakutoa maoni.


Amesema kilichotakiwa kufanywa na mkutano huo ni kujadili hoja iliyotolewa mezani, na kama kuna ukweli hatua zichukuliwe.


Lakini kwa kuwa walioandikwa ni viongozi wa juu wa chama hicho wameamua kumuadhibu Mwigamba bila ya kumsikiliza.


Hata hivyo kiongozi huyo amesema kuwa mbinu ya kuwafukuza ndani ya Chadema wafuasi wa Zitto hazitafua dafu kutokana na  kundi hilo kuzidi kujiimarisha zaidi kimapambano.

Moja ya sababu zinazotajwa kuchochea au kuibua makundi kusaka madaraka.


Zitto anatajwa kama mmoja wa vinara wa migogoro ndani ya Chadema, akidaiwa kutumia umaarufu wake kama kinga ya kufanya lolote analotaka akiamini kuwa “Chadema bila Zitto, haipo”.


Pia urafiki wake wa karibu na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, na viongozi wengine waandamizi wa CCM umekuwa ukiwatia shaka baadhi ya wanachama, wafuasi na viongozi wa Chadema.


Maelezo ya kiongozi huyo yameungwa mkono, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Kitila Mkumbo ambaye amasema.


Tatizo letu tunapenda sana kuangalia nani kasema nini badala ya amesema nini. Sasa kwenye hili imekuwa Mwigamba badala ya yale aliyoyasema. Lazima tuendeleze kuhimiza uvumilivu na uhuru wa maoni kwa sababu ndio misingi mojawapo muhimu ya demokrasia. Tutafika tu tupo safari katika ujenzi wa demokrasia yetu.


Tayari  chama hicho kimewafukuza uanachama, David Kafulila ambaye sasa ni Mbunge wa Kigoma Kusini, Juliana Shonza Mtela Mwampamba na wengine.


By Jamhuri