TEF, MCT wampongeza Kikwete

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Baraza la Habari Tanzania (MCT) wamempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa hatua ya kutangaza akiwa jijini London kuwa kuanzia mwakani, Serikali itatunga Sheria ya Haki ya Kupata Habari.

Ukiacha kutungwa kwa sheria hiyo, Rais Kikwete (pichani) ameagiza kuwa kuanzia sasa taarifa zote za Serikali, ukiacha masuala yanayohusiana na ulinzi na usalama, zinapaswa kuwa wazi.

 

“Bejeti ya Serikali ni kitu kinachopaswa kuwa wazi,” alisema Rais Kikwete mwishoni mwa wiki akiwa London, katika mkutano wa Open Government Initiative uliasisiwa na Rais Barrack Obama wa Marekani.

 

Rais Kikwete alisema kwa ajili ya nchi kupata maendeleo ya kasi, vitu kama mishahara, fedha za ruzuku inayotumwa wilayani, dawa na huduma zote zinazotolewa na Serikali hazipaswi kuwa siri.

 

Alisema sheria nyingi hapa nchini zimepitwa na wakati, kwani zinaweka katika kundi la siri hata mambo yasiyostahili kuwa siri kwani wananchi ndiyo wanaolipa kodi, hivyo wana haki ya kufahamu kodi zao zinatumiwaje.

 

Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Neville Meena, aliiambia JAMHURI kuwa amelipokea jambo hilo kwa furaha, isipokuwa akawataka watendaji serikalini kubadilika na kuwa na mawazo sawa na Rais wa Tanzania.

 

“Tumepata faraja sana ilipofika mahala mkuu wa nchi akakakiri mbele ya dunia kuwa kinachotokea hapa Tanzania ni kinyume cha sheria. Yeye amesema haya ikiwa ni siku chache tu gazeti moja lilifungiwa kwa kutaja mishahara ya umma, na kwamba documents (nyaraka) za siri zimekuwa nyingi.

 

“Sheria tulizonazo na watu waliopo hawajakubaliana na hilo. Tumepata faraja kwa kuona ana mawazo ya namna hiyo, ila tunafurahi kwamba amesema, na sasa ni wajibu wa watendaji kuchukua hatua,” alisema Meena.

 

Hata hivyo, Meena alisema Rais ametoa kauli hiyo wakati Bunge linakaribia kutunga sheria mbaya nyingine kwa kuongeza faini kwa waandishi wa habari kutoka Sh milioni 1.5 katika Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, kuwa Sh milioni 5 na kifungo cha kuanzia miaka mitano, suala ambao si sahihi.

 

“Wakati mwingine ni contradiction (kujikanganya) ndani ya Serikali hiyo hiyo, ni tatizo. Tunaomba achukue hatua na watendaji nao watekeleze tupate Sheria ya Haki ya Kupata Habari kwa ajili ya Watanzania wote, si kwa ajili ya vyombo vya habari tu. Ni vigumu Watanzania wote kwenda Ikulu kutafuta taarifa, waandishi wanafanya kazi hii kwa niaba ya umma,” alisema Meena.

 

Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MVT), Kajubi Mukajanga, aliiambia JAMHURI kuwa kauli ya Rais inaashiria nia njema na ni ya kupongezwa na kila mpenda uhuru wa habari nchi.

 

“Usipompongeza Rais wetu katika hili utampongeza kwa lipi maishani,” alisema kwa furaha Kajubi, na kuongeza: “Tutafanya utaratibu maalum wa kumshukuru na kumpongeza Rais kwa hatua hii na umma tutaujulisha. Hili ndilo tulilokuwa tukilipigania muda wote.”

 

Muungano wa Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CORI) umekuwa ukipambana kwa muda wa miaka 10 sasa, kupinga sheria kandamizi za magazeti, utangazaji na zinazozuia upatikanaji wa habari nchini.

 

Chini ya Muungano huu unaojumuisha wadau 11 ambao kimsingi ulianza harakati za kudai sheria ya haki ya kupata habari mwaka 1993, wamekuwa wakidai kutungwa kwa sheria mbili ambazo ni Haki ya Kupata Habari (RTI) na Huduma kwa Vyombo vya Habari (MSB).

 

Chini ya sheria hizi mbili, wadau wanadai haki ya kupata habari kwa Watanzania wote na sheria ya huduma kwa vyombo vya habari iwe ya kuweka mwongozo jinsi waandishi wa habari wanavyopaswa kutenda.

 

Kwa bahati mbaya baadhi ya watendaji serikalini kwa muda mrefu sasa, wamekuwa na mtazamo hasi kuhusu vyombo vya habari kwa kiwango ambacho kwa mashinikizo au matakwa binafsi, wamekuwa wakifungia magazeti yenye kuchapisha taarifa na habari wanazodhani ni za siri.

 

Mwezi uliopita Gazeti la Mwananchi lilifungiwa kwa siku 14 kutokana na kutaja viwango vya mishahara ya watumishi wa umma, ambapo wizara inayosimamia masuala ya habari ilidai kuwa mishahara ya watumishi wa umma ni siri, kitu kilichoonekana sasa kupigwa teke na Rais Kikwete.

 

Gazeti la Mtanzania nalo mwezi uliopita lilifungiwa siku 90 kwa kuandika kilichoitwa uchochezi, lakini wadau wa masuala ya habari wanasema utaratibu uliotumika kulifungia gazeti hilo pamoja na la Mwanahalisi lililofungiwa kwa muda usiojulikana, si sahihi kwani Serikali, ambaye ni mlalamikaji, ndiye aliyefanya kazi ya kuyafungia magazeti hayo.

 

Msimamo huu mpya wa Rais Kikwete umechukuliwa na wadau wa habari kuwa ni hatua moja mbele, kuelekea maendeleo ya kweli kwa Taifa hili, kwani mambo mengi yamekuwa yakikwama kutokana na watendaji kutumia sheria zinazowapa haki ya kufanya siri kila jambo kufisadi fedha za umma.