Matarajio ya kukiachia kizazi kijacho urithi wa rasilimali za wanyamapori, hasa tembo yanafifia nchini Tanzania .

Ujangili unaoendeshwa kwa silaha za kivita, zikiwamo silaha hatari aina ya AK 47 katika Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) unaangamiza idadi kubwa ya tembo kiasi cha kuhatarisha uwapo wao nchini.

 

Akitumia takwimu za Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, anasema ujangili umepunguza idadi ya tembo nchini kutoka 141,000 mwaka 2006 hadi 110,000 mwaka 2009.

 

“Kupungua huku kunatokana na ujangili uliosababishwa na mahitaji makubwa ya meno ya tembo katika masoko haramu kwenye nchi zilizopo Mashariki ya Kati na Mbali,” anasema.

 

Balozi Kagasheki alikuwa akizungumza kwenye warsha ya siku tatu kwa wahariri wa habari nchini, iliyobebwa na kaulimbiu ya, “Wajibu wa Vyombo vya Habari katika Kupambana na Ujangili.” Iliandaliwa na Shirika la TANAPA na kufanyika mjini Iringa, wiki iliyopita.

 

Kwa upande mwingine, matatizo ya umaskini wa Watanzania wengi, rushwa na mmomonyoko wa maadili miongoni mwa watumishi wa umma yanatajwa kuchangia vitendo vya ujangili ndani na nje ya TANAPA.

 

“Masuala mengine yaliyochangia kupungua kwa idadi ya tembo ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi, majanga ya asili na magonjwa,” ameongeza Balozi Kagasheki.

 

Anasema licha ya kuhatarisha uwepo wa tembo, ujangili pia unaathiri uchumi wa nchi, amani na usalama katika Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba na Mapori Tengefu.

 

“Ujangili pia unasababisha kupungua kwa idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi hizo, lakini pia unaathiri pato la Taifa, ambapo asilimia 17 ya pato hilo inatokana na shughuli za utalii,” amesema Waziri Kagasheki.

 

Amesisitiza kuwa hatua za dhati zinahitajika kuchukuliwa haraka kuongeza uwezo wa kukabili kama si kukomesha vitendo vya ujangili ambavyo kwa sasa vimejikita katika matumizi ya teknolojia na silaha za kisasa.

 

Analaani usaliti unaofanywa na baadhi ya watumishi wa umma katika bandari za Dar es Salaam, Tanga na Zanzibar ambako meno ya tembo yamekuwa yakisafirishwa kwenda Hong Kong, Vietnam na Ufilipino.

 

“Pale [bandari za Dar es Salaam , Tanga na Zanzibar ] kuna askari, watu wa Usalama wa Taifa. Kontena linapita na kwenda kukamatiwa Hong Kong , Vietnam , Ufilipino… linatokaje?” Anahoji.

 

Kutokana na ukubwa wa tatizo la ujangili nchini, Waziri anawaomba waandishi wa habari wasaidie kunusuru tembo na wanyamapori wengine kwa kuandika habari, makala na kutayarisha vipindi vitakavyosaidia kufichua mtandao wa ujangili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.

 

“Tunatarajia msaada kutoka kwa waandishi wa habari kuhakikisha kuwa vizazi vijavyo vinakuta na kunufaika na rasilimali za nchi zikiwamo za wanyamapori na mazingira hai, sisi kama Serikali tuko tayari kushirikiana na vyombo vya habari.

 

“Eneo la uhifadhi na utalii litabaki kuwa ndiyo injini ya uchumi wa Taifa hili for many years to come (kwa miaka mingi ijayo),” anasisitiza Waziri Kagasheki.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Allan Kijazi, ameahidi kuwa shirika hilo la umma litaendelea kushirikiana na vyombo vya habari katika kupiga vita ujangili na kuhamasisha uhifadhi na utalii wa kigeni na wa ndani.

 

“Waandishi wa habari ni miongoni mwa wadau muhimu wa TANAPA, ndiyo maana tumekuwa tukiwaandalia ziara na vikao vya kuhamasisha shughuli za uhifadhi na utalii. Lakini pia tunaamini kuwa vyombo vya habari vinaweza kutusaidia kutokomeza ujangili,” anasema Kijazi.

 

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, amesema Serikali katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania kwa kushirikiana na TANAPA na vyombo vya habari inajizatiti kuweka mikakati madhubuti ya kudhibiti vitendo vya ujangili ndani na nje ya Hifadhi za Taifa.

 

Nao, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, wamepongeza nia ya Serikali kutaka kutokomeza ujangili, lakini wakaitaka kutowafumbia macho watumishi wa umma wanaochangia tatizo hilo .

 

“Tunasema sana kwa sababu tunaipenda nchi hii, kufa ni kufa, afadhali kufa kwa kutetea mambo yenye maslahi ya umma kama hili la uhifadhi wa rasilimali zetu,” anasema Lembeli.

 

Naye Msingwa anasema, “Tuna wajibu wa kutunza hifadhi zetu. Nasikitishwa na watumishi wasio na hata chembe ya uadilifu wa kulinda wanyamapori, badala yake wanakuwa ndiyo wahujumu wa rasilimali hizo.”

 

Inahofiwa kuwa huenda idadi ya tembo hapa nchini imepungua hadi chini ya 100,000 kutokana na wimbi la ujangili wa kutumia silaha za kivita kuendelea kushika hatamu ndani na nje ya TANAPA.

 

By Jamhuri