Habari mpendwa msomaji. Kwanza kabisa niombe radhi kwa kutoendelea na makala ya ‘Nina Ndoto.’ Makala hizi zitaendelea kama kawaida wiki ijayo.

Mapema Alhamisi ya wiki mbili zilizopita ilikuwa asubuhi yenye majonzi kwa Watanzania wengi. Tuliondokewa na mpendwa wetu Dk. Reginald Abraham Mengi.

Mengi amekuwa mtu aliyegusa maisha ya watu wengi ndiyo maana nikaona si vema kuacha jambo hili lipite tu bila wewe mpendwa msomaji kujifunza kitu kutoka kwenye maisha yake  kinachoweza kubadili maisha yako pia.

Reginald Abraham Mengi alikuwa bilionea tajiri, mfanyabiashara Mtanzania akiwa na utajiri wa dola milioni 560 za Marekani. (Kutokana na Gazeti la Forbes.)

Ni mwanzilishi na mmiliki wa kampuni za IPP Ltd zinazomiliki vyombo vya habari kama vile ITV, Capital TV, EATV na East Africa Radio, lakini pia magazeti mengi, yakiwamo ya Nipashe na The Guardian.

Alizaliwa wilayani Machame, Kilimanjaro mwaka 1942, akiwa mmoja wa watoto saba wa Abraham na Ndeekyo Mengi. Alifariki dunia usiku wa kuamkia Mei 2, mwaka huu akiwa na umri wa miaka 77.

Ameandika kitabu kiitwacho ‘I Can, I Must, I Will’ kinachoangazia historia ya maisha yake tangu akiwa mdogo hadi kuwa mfanyabiashara mkubwa.

Hadi mauti yanamfika, Mengi alikuwa Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT).

Leo ningependa tujifunze mambo haya kutoka kwenye maisha ya Mengi:

Mosi, kuzaliwa maskini si kosa lako, kosa ni kufa maskini.

Huu ni msemo anaopenda kuutumia mwanzilishi wa Kampuni ya Microsoft, Bill Gates. Mengi alizaliwa katika familia yenye umaskini wa kutupwa, lakini hilo halikumfanya akate tamaa na aseme hawezi kufanikiwa.

Anasema: “Nimekulia kwenye umaskini, lakini siku zote nimekuwa nikiona umaskini kama changamoto. Habari njema ni kuwa, unaweza kuushinda umaskini kama uko tayari kulipa gharama. Gharama hiyo ni kufanya kazi kwa bidii.”

Pili, ukitaka kufanikiwa ongeza maarifa. Ukisoma kitabu chake utabaini Mengi alikuwa mtu anayependa kusoma vitabu, alipenda kuongeza maarifa kila uchao. Mafanikio yako leo yatategemeana na kiwango cha maarifa ulichonacho. Soma vitabu ufanikiwe, soma vitabu ufungue ukurasa mpya wa  maisha yako.

Tatu, anza biashara kwa kuangalia kitu kisicho sokoni.

Wazo la kuanzisha televisheni ya Capital lilikuja baada ya kuona hakuna televisheni yoyote yenye kutoa maudhui kwa lugha ya Kiingereza hapa nchini. Mwaka 2009 televisheni hiyo ilianza kurusha matangazo.

Nne, matatizo ni fursa. Siku moja wakati kaka yake Elitira amerudi kutoka masomoni Uingereza walipanga kumfanyia sherehe, lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida walikosa vinywaji baridi katika mji mzima wa Moshi. Iliwalazimu kusafiri kilometa 74 hadi Arusha ili wapate vinywaji hivyo. Hapo ndipo Mengi aliona uhaba wa vinywaji baridi katika ukanda wa Kaskazini na kuamua kuanzisha kiwanda kilichokuwa kinazalisha bidhaa zilizo chini ya Kampuni ya Coca-Cola.

Tano, woga wako ndio umaskini wako.

Dk. Mengi anasema Watanzania wengi ni waoga wa kufanya biashara. Wengi wao wanakosa uthubutu. Huwezi kufanikiwa kwenye maisha kama ukibaki na woga na hali  ya kutothubutu. Mengi anawasihi Watanzania kuanza biashara na kuachana na visingizio vya maneno kama: “Siwezi” au “Sina mtaji” au “Sina uzoefu” au “Nimezeeka” au “Bado  mdogo”; haya yote yanatokana na kukosa ujasiri. Woga ni adui mkubwa wa mafanikio.

Weka alama

Maisha ya Mengi yamekuwa maisha yaliyogusa maisha ya watu wengi, kuanzia watoto, vijana na hata wazee. Ametoa misaada mbalimbali kwa watu wenye ulemavu, ametoa mitaji kwa vijana waliokuwa na mawazo bora ya biashara, amewasaidia watu waliokuwa wakikumbwa na majanga mbalimbali.

Mengi ni mfano wa kuigwa na watu wengi waliofanikiwa. Anasema katika kitabu chake: “Furaha ya kweli ni kujitoa kwa yule anayetoa na anayepokea.” Mtu tajiri hawezi kuwa na furaha wakati wale wanaomzunguka wanaishi katika mazingira magumu.

“Tutakapoaga dunia msitutafute katika makaburi yenye marumaru na chokaa safi, bali  tutafuteni katika mioyo ya watu tuliowatumikia,” alisema Ibn Battuta wa Morocco (1304-1368), mfanyabiashara na mwanafalsafa.

Kuna maswali manne ya kujiuliza kwa mtu anayetaka kuacha alama; Mosi, kama ningefanya kitu kimoja kwenye maisha yangu kingekuwa kitu gani?

Pili, kama nisingekuwa na upungufu wowote ningefanya nini?

Tatu, ni jambo gani litanifanya nikabiliane na changamoto kubwa zaidi yangu?

Nne, kama nikisimama mbele ya Mungu, atanipongeza kwa kufanya jambo lipi?

1010 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!