Katika maisha ya Kiafrika ya kizamani watu wote walikuwa sawa. Walishirikiana pamoja na walishiriki katika uamuzi wowote unaohusu maisha yao. Lakini usawa huu ulikuwa usawa wa kimaskini; ushirikiano wenyewe ulikuwa wa vitu vidogo vidogo.

Na serikali yao ilikuwa serikali ya jamaa, au ukoo, na ikizidi sana labda ya kabila zima. Kwa hiyo kazi yetu ya sasa ni kuibadilisha kidogo hali hii ya kizamani ili ifanane na shabaha zetu za kuwa na maisha yaliyo bora zaidi.

Tunaweza kufanya hivi kama tutazingatia mila za maisha ya zamani ya ujamaa, na wakati huo huo tunatumia ujuzi wa karne hii. Na njia ya kufanya hivyo ni kuunda katika Tanzania nzima jamaa ambamo watu wanaishi pamoja na kufanya kazi pamoja kwa faida yao wote, na jamaa zenye uhusiano ili kila jamaa moja ishirikiane na nyingine kwa faida ya taifa zima.

Hiindiyo shabaha iliyoelezwa katika kijitabu Ujamaa Vijijini, ambacho ningeshauri wajumbe wa Mkutano huu mkisome. Maelezo hayo ni ya kutekeleza Azimio la Arusha katika mambo yote yanayohusiana na maisha ya vijijini.

Ni muhimu ieleweke wazi kwamba yatupasa wote tufanye juhudi kutimiza lengo hilo. Maana Ujamaa Vijijini ni maelezo ya Ujamaa na Kujitegemea jinsi kunavyohusu maisha ya vijijini, watu wa vijijini, yaani jinsi Ujamaa na Kujitegemea kunavyowahusu 95 kwa mia ya watu wetu.

Kwa nchi nzima kutakuweko Mipango ya Taifa ya Maendeleo; kutakuweko mashamba ya Taifa, misitu ya Taifa, mbuga za Wanyama, na kadhalika. Lakini hii ya kwanza itaanzishwa na kuendeshwa kwa sababu ya kuisaidia haja maalum.

Lakini jinsi wengi katika watu wetu watakavyoishi katika Tanzania ya Ujamaa itakuwa katika vijiji ambavyo wao wenyewe wamevijenga na kuvitawala, na ambavyo ndio msingi wa kazi za uchumi na kuwafaa wakaao katika vijiji hivyo.

Hebu jaribu kuieleza shabaha hii kwa urahisi zaidi. Jamaa kadha zitaishi katika kijiji, na watafanya kazi pamoja katika shamba la shirika kwa faida yao wote. Nyumba zao zitakuwa zile za kujijengea wenyewe, kila mtu kwa nguvu zake.

Shamba ni lao wote, na mazao yatakuyopatikana yatakuwa mali ya wote kwa jumla. Kazi za kijiji hicho, aina na kiasi cha mazao watakayopanga kuvuna, pamoja na ugawanyaji wa mavuno hayo na vitu vingine vinavyopatikana yote yatapangwa kutokana na uamuzi wa watu wa kijiji kile wenyewe.

Maana ardhi ile itakuwa mazao ‘yetu’ ng’ombe watakuwa ng’ombe ‘wetu’. ndiyo kusema tutakuwa na jamaa ya kiasili ya Kiafrika ambapo kilakitu cha lazima kilikuwa ni ‘chetu’; lakini itakuwa ni jamaa kubwa ziadi na ya muundo mpya.

Hesabu ya watu na aina ya watu waishio pamoja katika kijiji itahitilafiana  katika kila sehemu ya nchi. Tofauti hizo hutegemea ardhi iliyoko, mimea inayoweza kuota, wanyama wafugwao, na mila za mahala pale.

Lakini kwa kuishi pamoja na kufanya kazi pamoja, wote watapata maisha bora zaidi. Badala ya jamaa 40 kila mmoja kuishi peke yake, na kila mmoja akilima kijishamba chake, akiteka maji yake, na akipeleka watoto wake shule kijiji cha mbali, sasa watakusanyika na kukaa pamoja kijijini.

Na hivyo, kwa juhudi zao za pamoja, wataweza baada ya muda kuyaleta maji kijijini kwao; wataweza kujenga jumba la maendeleo na kijiduka chao cha kuwafaa, na kadhalika.

Aidha, kwa ajili ya kulima pamoja katika shamba moja kubwa mara watamudu kununua plau la ng’ombe kufanya kazi nyingi ambazo zamani kila mmoja wao alilazimika kufanya kwa jembe la mkono ama panga.

Sasa wataweza kupata faida ya mashauri kutoka kwa wataalam kuhusu ukulima wa kisasa. Wataweza, kwa pamoja, kuweka mipango ya kuuza mazao yao, na mipango ya kuleta bidhaa wanazotaka kuzinunua kutoka nje, labda kwa kujitengenezea duka la ujamaa. Na kadhalika.

Ndiyo faida ya binadamu kuishi na kufanya kazi pamoja. Watu wote wa kijiji hicho watakuwa na hali sawa, na tofauti zitakazokuwapo za mapato zitaonekana tu kutokana na jasho la mtu. Watu watakuwa wakifanya kazi kwa ushirikiano, na wala si kwa kupingana; na watajitengenezea mambo ya kijiji chao; vile vile watafikiria matatizo yanayowakabili kama raia wa Tanzania.

Hiyo ndiyo shabaha yenyewe. Imeelezwa wazi wazi na kwa urefu katika kitabu kile nilichotaja cha ‘Ujamaa Vijijini’. Hatuna budi kulielewa jambo hili, ili tufahamu lengo letu. Lakini si kitu cha kutimizwa kwa kufumba na kufumbua. Bado tuna kazi kubwa ya kufanya.

Maana mambo yaliyokuwa yakitokea katika miaka iliyopita ni tofauti kabisa. Hatukufikiria kukuza au kuendeleza maisha yetu ya kiasili ya ujamaa kwa kutumia ujuzi wa kisasa; badala yake tumependelea kulima vishamba vidogo kwa mtindo wa kikabaila.

Wakulima wetu wengi wenye juhudi, na hasa wale waliokuwa radhi kujifunza maarifa mapya, ndiyo waliojitenga na kujilimia kila mtu peke yake. Hawakupanua mashamba yao kwa kusgirikiana na wenzao katika hali ya usawa, lakini wameyapanua mashamba hayo kwa kuweka vibarua.

Kwa hiyo tumefikia mwanzo wa kuwa na vibarua wa kilimo wanaoajiriwa, na matajiri wanaoajiri vibarua. Kwa bahati nzuri, hali hii haijafika mbali sana, tunaweza kuizuia bila ya shida kubwa.

Lakini tusifanye mabadiliko hayo kwa kuwasimanga wakulima walioendelea; kwani sisi ndio tuliowaachilia wakaelekea njia hiyo! Badala yake yatupasa tutafute njia za kushirikiana nao, na kuwaingizia katika ukulima wa ujamaa kwa kuwaonyesha kuwa watapata faida wakifuata njia hiyo. Maana juhudi na ari waliyotuonyesha wakulima hawa itatufaa sana katika maendeleo yetu. Tunawahitaji watu hawa.

Tunawezaje kuondoka katika hali hii ya sasa, na kuunda mitindo ya vijiji vya ujamaa? Kile kitabu nilichokitaja, ‘Ujamaa Vijijini’, kinaeleza baadhi ya hatua zinazoweza kuchukuliwa katika sehemu mabali mbali, lakini ni muhimu kukumbuka mambo mawili.

Kwanza ni kwamba hatua zenyewe za mwanzo zinazofaa kuchukuliwa zitahitilafiana baina ya kijiji na kijiji. Na pili watu wenyewe ndiyo watakao amua kama wako tayari kuchukua hatua hiyo au bado.

Maana jitihada yetu siyo ya kuongeza uchumi peke yake, bali pamoja na hilo tunajaribu kuleta mtindo mpya wa kuishi kwa watu wetu walio wengi. Na hilo linaweza tu kufanyika ikiwa watu wanaelewa shabaha za hatua hiyo, na wanaamua kushiriki katika mpango huo.

Tusijaribu kuiharakisha mipango hii; jambo kubwa si mbio bali shabaha . hatuna budi kuwatia moyo na kuwasaidia watu; tusijaribu kuwashurutisha. Maana aina hii ya kijiji ipo Tanzania, na wale waishio humo wanaona faida zake.

Lakini pia wakati mwingine watu wamejaribu kuanzisha kitu cha namna hii, na wameshindwa. Mara nyingi sababu ya kushindwa ni kwamba matumaini yao yalikuwa makubwa mno.

Walikuwa na ari nyingi mno na wala hawakuwa na subira. Kinachotakiwa ni watu wenyewe wafikirie kwa makini na kupanga hatua za kuchukuliwa. Ndiyo maana inafaa zaidi kuanza pole pole, labda kwa kulima shamba la shirika pamoja na shamba la kila mtu; au pengine kwa kusaidiana. Hapo basi jinsi matatizo yanapotokea, na yanapotatuliwa na wakulima wenyewe, ndipo watakapokuwa na imani ya kujaribu hatua ya pili.

Lakini kufanya mambo polepole maana yake siyo kufanya mambo bila ya moyo. Mtu ye yote anayeelewa shabaha hii anaweza kuanzisha mawazo ya kuelekea kwenye kijiji cha ujamaa.

Si lazima awe kiongozi wa TANU au mkuu wa Serikali. Mtu ye yote anaweza akajiunga na kikundi cha rafiki zake, na wakaamua kuanza. Maana vijiji hivivitajimiliki wenyewe, na wakaaji wa vijiji hivyo lazima waendeshe mambo yao wenyewe.

Hakuna mtu mwingine ye yote anayeweza kuwafanyia hivyo. Kwa hiyo kikundi cha vijana kinaweza kikaazimu kuanza, au watu wanaoongozwa na balozi mmoja wa TANU, au watu wa kanisa fulani, au watu wa msikiti fulani.

Au mwalimu katika shule ya kijiji anaweza akaanzisha mpango kwa kuwaomba wazazi wa watoto kushirikiana na shule katuka mpango fulani. Na kadhalika.

By Jamhuri