Mkataba  wa  ajira  ni  sawa  na  mikataba  mingine.  Huingiwa  kwa  hiari  ya  wahusika  na  wahusika hao hao  waweza  kuondoka  katika  mkataba  huo kwa  hiari  zao.  Tuzungumzie mwajiri  kuamua  kujitoa  katika  mkataba  wa  ajira.

Mwajiri  anaweza  kujitoa  katika  mkataba  wa  ajira. Mwajiri  kujitoa  katika  mkataba  wa  ajira  maana  yake  ni  kumsimamisha  kazi mwajiriwa. Si  kosa  kumsimamisha  kazi  mwajiriwa,  bali  ni  kosa  kumsimamisha  kazi  mwajiriwa  bila  kufuata  utaratibu  wa  sheria.

Hapa  chini  tutaona  mambo  muhimu  ambayo  ni  haki  kwa  mwajiriwa  japo wote  mwajiriwa  na  mwajiri  wanatakiwa kuyajua  ili  haki  na  wajibu  viweze kutimizwa.

Taarifa ya  kuvunja  mkataba (Notice)

Notisi  hubeba  taarifa  za  kusudio  la  kuvunja  mkataba   na  sababu  za  kuvunja  mkataba.

Mambo ya kuzingatia ni  haya:

(a) Kwa mkataba  wa  ajira  ambao  malipo  yake  ni  ya  kila  mwisho  wa mwezi (monthly pay contract)  notisi  yake  inatakiwa  kutolewa  ndani  ya  siku  28  kabla  ya  siku  ambayo  mkataba  unatarajiwa  kuvunjwa.

(b) Kwa mikataba  ambayo  ni  ya  siku  moja  moja au  wiki  kwa  wiki,  basi  mwajiriwa  anatakiwa  kutoa  notisi  ya  ya  siku  4  kabla  ya siku ya  kuvunja  mkataba.

(c) Kwa  mkataba  wa  ajira  ambao  unatakiwa  kuvunjwa  ndani  ya  mwezi  mmoja tokea  kuingiwa  kwake,  basi  notisi  ya  siku  saba  kabla  inatakiwa  kutolewa  na  mwajiriwa.

(d) Ikiwa  mkataba unacho  kipengele  kinachoongelea  notisi  na  muda  wake,  basi  muda  huo  hivyohivyo  ulivyo  katika kipengele hicho unatakiwa  kufuatwa.

Gharama  za  kumrudisha  mwajiriwa  alikotolewa (repatriation expenses)

Sehemu ulikofanyia  usaili  na  kusaini  mkataba  ndiyo  sehemu  inayohesabika  kuwa  eneo  lako  la kazi  la  asili. Ukihamishwa  kutoka  hapo  kwenda  wilaya, mkoa  au nchi  nyingine, basi  hili  litakuwa ni  eneo  jingine  la kazi.

Na ikiwa mkataba  utavunjwa  ukiwa  eneo  jingine  la  kazi,  basi  unastahili  kupata  gharama  za  kurejeshwa  eneo  lako  la  kazi la asili.

Mosi, unaweza  kupatiwa  posho na  kujisafirisha  mwenyewe.

Pili, unaweza  kupatiwa  usafiri  wa  kukusafirisha  badala  ya  posho.

Usafirishaji  unakuhusu  wewe  mwenyewe  mwajiriwa, mizigo  yako  na  familia  kama  unayo. Gharama  za  chakula na sehemu ya kulala  njiani  zinajumuishwa  kama  zipo.

  

Cheti cha utumishi/huduma (Certificate of Service)

Ni cheti  ambacho  huwa  kinathibitisha  kuwa fulani  alihudumu  sehemu  fulani, kwa  cheo  fulani, ndani  ya  muda  fulani  na  huduma  yake  ilikuwa  nzuri kwa  kiwango  fulani.  Cheti  hiki  humsaidia  mwajiriwa  kupata  ajira katika eneo  jipya  kwa  wepesi na  uaminifu.

Lakini  pia  hukuza wasifu  wa  mwajiriwa na  huondoa dhana  kuwa  yawezekana  mwajiriwa  aliondolewa  kwenye  kazi  husika  kwa  makosa  ya  kinidhamu nk.

Malipo ya kisheria na kimkataba

Malipo yote ya kisheria na kimkataba yalipwe kwa mwajiriwa kabla  ya  mkataba  kusitishwa. Haya  ni  pamoja  na  mishahara  anayodai  kama  ipo, posho  zake zote, overtime  kama  zipo, likizo kama  zipo, kifuta  chozi (severance pay),  na  malipo  yote ambayo  anastahili  na  yapo  kimkataba.

By Jamhuri