Hofu ni mtihani. Kuna aliyesema: “Hofu ina maana mbili: sahau kila kitu na kimbia; maana ya pili, kabili kila kitu uinuke.”

Huenda ilipo hofu ndipo palipo mafanikio yako. “Kila kitu unachohitaji kiko upande wa hofu,” alisema Jack Canfield.

Mara nyingi utagundua hofu ni uongo unaojiambia. Hofu ni hadithi unayojihadithia, hofu ni alama ya kusimama unayoijenga akilini.

Kuna aina nyingi za hofu: hofu ya kushindwa, hofu ya kutokuwa mwema vya kutosha, kutaja aina chache. Nelson Mandela alikuwa na haya ya kusema juu ya Hofu: “Nilijifunza kuwa ujasiri si kutokuwepo kwa hofu, bali ushindi dhidi yake, mtu mwenye ujasiri si yule ambaye hana hofu, bali yule anayeishinda hiyo hofu.”

Mtu mmoja alikuwa kwenye meza ya operesheni kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa moyo, alimwambia daktari kuwa alikuwa anaogopa upasuaji huu. Daktari alimwambia katika hospitali hii ni mgonjwa mmoja tu aliyekufa nilipofanya upasuaji.

Mgonjwa aliuliza: “Umewafanyia upasuaji wa moyo watu wangapi?” Daktari alijibu: “Wewe utakuwa wa pili.” Mgonjwa aliyekuwa kwenye meza ya operesheni aliogopa kumpokea daktari huyo kuwa daktari mpasuaji wa moyo wake, ili mgonjwa apone hana budi kumpokea daktari.

Ili mwanafunzi afaulu hana budi kumpokea mwalimu. “Hofu ya unachohofia kufanya ni dokezo tosha ya jambo unalopaswa kufanya baadaye,” alisema Ralph Waldo Emerson.

Katika maisha tunaogopa kuwapokea watu wapya katika maisha yetu, tunaogopa kumpokea mtu kuwa mwalimu wetu, tunaogopa kumpokea mtu kuwa kiongozi wetu. Watu wanasema: “Fulani watu hawakumpokea.”

Tunaogopa kumpokea mtu kuwa daktari wetu kama hadithi hapo juu inavyobainisha.  Methali kama zimwi unalolijua ni bora kuliko zimwi usilolijua, ni methali inayobainisha hofu ya kumpokea mtu. “Hofu haiishi popote isipokuwa kwenye akili,” alisema Dale Canergie.

Kuna kuogopa ambako ni kubaya. Kuna hofu ambayo inaingia kwenye nyumba  na ukweli unakimbia, kuna wazazi ambao wanaogopa kuwaambia watoto wao ukweli wa makosa yao.

Hofu hiyo ikiingia ukweli unakimbia, hiyo ni hofu mbaya. Mfano mwingine, mwanaume akimwogopa mke wake wa ndoa hawezi kuzaa naye, hiyo ni hofu mbaya.

Kuwa na maandalizi ya kutosha kwa jambo halali ambalo unategemea kulifanya ni mweleka mkali kwa hofu na tabia ya kuogopa. Mwanafunzi ambaye amejiandaa vizuri kufanya mtihani hatatoka jasho jembamba kwa sababu ya kuogopa mtihani kama yule ambaye hajajiandaa.

Ingawa panaweza kuwepo hofu kidogo, lakini hofu hiyo kwa wengine inaweza kuwaharibia hata kile wanachokijua. Jambo la kuhofia ni hofu, jambo la kuogopa ni kuogopa.

Maandalizi ni siri ya kuikabili hofu. “Ukiwa unaogopa, weka akili yako yote kwa jambo ambalo unapaswa kufanya. Na kama umejiandaa vizuri, hautaogopa,” Dale Carnegie.

Kufanya zuri unaloliogopa ni namna ya kuikabili hofu. Lifanye hilo zuri unaloliogopa mara nyingine mpaka hofu ibaki nyuma yako, kuwa na mtazamo chanya ni namna ya kuikabili hofu.

“Baada ya muda na mtu atakavyofaidi uzoefu, atajifunza kuwa mambo  yatakuwa vile ambavyo hakutegemea au hayatakuwa mabaya kama alivyoogopa,” alisema Jerome S. Bruner.

Mtoto mdogo alikuwa mmojawapo wa wachezaji wa mchezo wa kuigiza wa Krismasi. Alipewa sehemu ya kusema maneno haya: “Ni mimi. Usiogope.”

Wakati wa mchezo badala ya kusema maneno hayo alisema: “Ni mimi na ninaogopa.” Kusema kweli adui yetu namba moja ni hofu. Ikabili kwa kufanya maandalizi mazuri.

Please follow and like us:
Pin Share