Mwaka 2015 kuelekea Uchaguzi Mkuu wa taifa letu la Tanzania, niliandika makala nyingi sana katika Gazeti hili la Jamhuri. Makala zangu zilikuwa zinakosoa mwenendo wa Chama tawala (CCM).

Sihitaji kusimulia kilichonitokea lakini inatosha kudokeza kiduchu: ‘Niliambulia vitisho vya kuondolewa uhai wangu’. Nilijiuliza maswali mengi sana. Je, ni kweli kwamba kuikosoa serikali ni dhambi?

Na kuisifia ni utukufu? Je, ni kweli kwamba kukikosoa chama tawala ni dhambi? Kama kukisifia chama tawala ni utukufu, kwa nini kukikosoa iwe dhambi? Ni maswali mepesi sana kujibika lakini yanahitaji busara kuyajibu.

Nikiwa katika hali ya kujiuliza maswali mengi nilikutana na nasaha ya Mwanaharakati wa Afrika Kusini, Steven Biko. Mwanaharakati huyu, Steven Biko, aliyepata misukosuko katika taifa lake, alipata kunena nasaha hii: “Ni bora ukaishi miaka michache duniani jina lako likabaki linaishi kwa wema na haki duniani kuliko kuishi miaka mingi duniani na ukatoweka kama mzoga.”

Nikiwa katika tafakuri ya kina nilisoma maisha ya Mt. Agapitus. Huyu alikuwa ni kijana shupavu aliyeitetea imani Katoliki mpaka akawa tayari kuutoa uhai wake kwa ajili ya kuitetea na kuilinda imani Katoliki.

Kijana huyu alipoambiwa aikane imani yake, aliwaambiwa watesaji wake maneno haya: “Niko tayari kufa kwa ajili ya Kristo.” Kijana huyu aliyekuwa na umri wa miaka 15 alikatwa kichwa chake kwa kuishuhudia imani yake.

Katika maisha yangu namwomba Mungu vitu vitatu. Kitu cha kwanza, namwomba Mungu anijalie kukiishi kile ninachokiandika na ninachokizungumza. Kitu cha pili, namwomba Mungu anijalie fadhila ya unyenyekevu. Kitu cha tatu, namwomba Mungu anijalie niifie dini.

Niko tayari kufa kwa kutetea haki za wanyonge, uhifadhi bora wa mazingira, demokrasia safi, siasa safi na utawala bora. Niko tayari kufa kwa kuitetea, kuipenda na kuilinda imani Katoliki. Mimi si mwanasiasa na sihitaji kuwa mwanasiasa.

Kuwa mwanasiasa katika nchi za Kiafrika ni gharama sana, mimi ni mwanasaikolojia, mtunzi wa vitabu vya mageuzi ya kifikra na mtunzi wa vitabu vya imani Katoliki.

Leo wasomaji wangu wengi mnaweza kujiuliza swali hili: ‘Leo Bhoke ametoka kwenye makala za mageuzi ya kifikra mpaka kwenye makala za siasa?’ Ninafahamu kwamba ninao wasomaji zaidi ya 600 katika ukurasa huu wa ‘TUZUNGUMZE’ ambao ninawasiliana nao kila mara.

Gazeti hili la Jamhuri limeniongezea familia kubwa sana. Na sasa kila mkoa nina mwanafamilia. Hii ni zawadi ya familia takatifu niliyoipata katika Gazeti hili la Jamhuri. Namshukuru sana Deodatus Balile na Manyerere Jackton kwa kuanzisha gazeti ambalo limenikutanisha na Watanzania ambao sasa ni wanafamilia wangu.

Niruhusu niendelee na mada yangu. Mimi kama Mtanzania, ninayo haki ya kikatiba ya kutoa maoni yangu katika taifa langu, haijalishi maoni yangu yatapuuzwa ama yatapokelewa. Leo ninataka kuzungumza kile ninachokiona kikitokea katika taifa langu.

Katika makala hii nafahamu nitatofautiana na mawazo ya walio wengi hasa watawala wasio na hadhi ya kiutawala na wasomi wasio na hadhi ya usomi. Furaha yangu ni kuona ninatofautiana na walio wengi, kwani katika kutofoutiana nao nitanufaika kwa kujifunza mwono wa fikra zao thabiti ama fikra zao dhaifu.

Mwanasayansi Sir Isaac Newton (1642-1727) anasema: “Mkituona tumesimama juu, ujue tumesimama kwenye mabega ya miamba iliyotutangulia na kama katika maisha yangu nimefanikiwa kuona mbali kuliko watu wengine ni kwa sababu ya kusimama mabegani mwa watu wakubwa.”

Historia yetu kutoka ukoloni hadi leo ni shule ya awali mpaka chuo kikuu cha mafunzo ya amali za maisha, umakini, fikra na utendaji, tulipotoka ni mbali, tujipime na tujitafakari. Tanzania ni yetu, wa kuiua ni sisi wenyewe na wa kuijenga ni sisi wenyewe. Maisha yana ladha pale tu tunapotofautiana mitazamo.

Please follow and like us:
Pin Share