Kocha wa timu ya soka ya taifa (Taifa Stars), Kim Poulsen, amesema kuwa haoni sababu itakayoizuia Tanzania kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2015.

“Tumecheza dhidi ya Zambia na Ethiopia kama sehemu ya maandalizi ya Stars kucheza AFCON mwaka 2015,” amesema kocha huyo wakati akitangaza kikosi kitakachocheza na Cameroon kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kesho.

 

Pamoja na kutakiwa kucheza mechi nyingi za kirafiki na timu bora zaidi na hasa kutoka Afrika ya Magharibi kama Cameroon hapo kesho, wachezaji wa Stars pia wanapaswa kuhamasishwa kwa namna nyingi.


Mathalani, wachezaji wa timu ya Taifa ya Ghana waliahidiwa kulipwa dola 35,000 (sawa na Sh 57,050,000 za Tanzania) kila mmoja, kama wangeingia robo fainali za AFCON 2013 na kufanikiwa.


“Tayari wameshalipwa fedha walizoahidiwa kama wangeifikisha timu katika robo fainali…kila mchezaji amepata (fedha zake),” amesema meneja wa timu hiyo, Emmanuel Kyeremeh.

Katika hali hiyo, dhamira ya Poulsen inatakiwa iungwe mkono kwa namna zote na Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Shirikisho la Kandanda Tanzania (TFF), linalotarajiwa kupata uongozi mpya baadaye mwezi huu, ikiwa ni pamoja na kutumia fedha nyingi kuwalipa wachezaji.


Inabidi walipwe, kwa mfano, mapato yote ya mgawo wa timu hiyo yatokanayo na viingilio kwa kila mechi wanayocheza na kushinda, halafu wanapotoka sare walipwe angalau robo yake na kadhalika.


Stars ilicheza fainali hizo kwa mara yake ya kwanza mwaka 1980 zilipofanyika nchini Nigeria, kisha imeshindwa kufuzu tena licha ya kusaka tiketi hiyo kila msimu na kutolewa mapema.

1126 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!