· Mawaziri wengi hawadumu zaidi ya miaka miwili

DAR ES SALAAM

NA ALEX KAZENGA

Kutimuliwa kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, wiki iliyopita kumeifanya wizara hiyo iendelee kuwa miongoni mwa wizara ambazo zimeongozwa na idadi kubwa ya mawaziri kutokana na mabadiliko yanayofanyika.

Ni wizara ambayo inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya mawaziri walioteuliwa na kutenguliwa baada ya muda mfupi kuliko wizara nyingine tangu nchi ipate Uhuru Disemba 9, 1961.

Mpaka sasa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, aliyeteuliwa wiki iliyopita anakuwa waziri wa 26 kuiongoza wizara hiyo na wa nne katika Serikali ya Awamu ya Tano, ambayo imetimiza miaka minne madarakani hivi karibuni.

Wakati watu wakijadili mabadiliko ya mara kwa mara ndani ya wizara hiyo, Mbunge wa Gairo mkoani Morogoro, Ahmedy Shabiby, aliwahi kusema bungeni kuwa anatamani amwambie Rais John Magufuli aendelee kufanya mabadiliko kama hayo ili apate timu inayofaa kufanya naye kazi.

Akizungumza miezi kadhaa iliyopita, Shabiby alisema anatamani Dk. Magufuli awatengue baadhi ya mawaziri wasiofanya kazi kwa bidii na kuikwamisha azima ya kuiletea maendeleo nchi kwa haraka.

Alidai kuwa Rais Magufuli anatakiwa kupangua Baraza la Mawaziri kadiri atakavyo hadi hapo atakapopata mawaziri sahihi watakaomsaidia kuchapa kazi na si wasaka sifa na walalamikaji kama wanavyofanya baadhi ya mawaziri katika vyombo vya habari.

Kwa hakika hicho ndicho ambacho Rais Magufuli anakifanya katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kwani katika miaka yake minne madarakani tayari amekwisha kubadilisha mawaziri mara nne katika wizara hiyo.

Katika Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete, wizara hiyo iliongozwa na mawaziri watano katika kipindi cha miaka kumi na kufanya wastani wa waziri kudumu katika wizara hiyo kuwa miaka miwili tu.

Historia inaonyesha kuwa mtindo wa mawaziri kutodumu katika wizara hiyo ulianza tangu nchi ilipopata Uhuru.

Goerge Simbachawene, Mbunge wa Kibakwe mkoani Dodoma, aliyemrithi Lugola akitokea Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, anakuwa waziri wa nne chini ya Serikali ya Awamu ya Tano kuiongoza wizara hiyo.

Lugola ametenguliwa baada ya kusaini mkataba wenye thamani ya Euro milioni 408 (zaidi ya Sh trilioni moja) kuhusiana na masuala ya zimamoto na uokoaji, mkataba ambao, kwa mujibu wa Rais Magufuli, ulisaniwa kijanja na bila kupitia taratibu zilizowekwa kisheria.

Pamoja na Lugola, aliyekuwa Kamishna wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye, naye aliondolewa katika nafasi yake.

Ikumbukwe Lugola aliteuliwa kuiongoza wizara hiyo Julai Mosi, mwaka 2018 baada ya kuondolewa kwa Mwigulu Nchemba.

Sababu zilizomwondoa Mwigulu katika wizara hiyo ni pamoja na kushindwa kudhibiti ajali za barabarani zilizokuwa zimekithiri kwa kipindi hicho.

Mbali na sababu hiyo, zilikuwapo tuhuma nyingine kuhusiana na usajili wa asasi zisizo za kiraia (NGOs) kinyume cha sheria.

Rais Magufuli alieleza sababu za kutengua nafasi ya Mwigulu kuwa ni pamoja na kitengo cha Uhamiaji kutoa vibali vya kufanya kazi nchini kiholela huku maofisa wa Uhamiaji waliokuwa wakifanya ubadhirifu huo wakiachwa bila kuchukuliwa hatua.

Pia, Rais Magufuli aliyataja makosa mengine yaliyomwondoa kuwa ni kushindwa kushughulikia suala la promosheni kwa askari kwa kipindi kirefu, kushindwa kudhibiti masuala ya wakimbizi na wizara hiyo kuwa na madeni mengi Wizara ya Fedha.

Wakati wa kumwapisha Lugola, Rais Magufuli alimuagiza kufanya uhakiki wa madeni hayo ikiwa ni sambamba na kukiboresha Kikosi cha Jeshi la Zimamoto kwa kukipatia vifaa na magari ya kutosha.

Inaonekana tatizo hilo bado lipo, kwani wakati akizindua nyumba za Jeshi la Magereza wiki iliyopita, Rais Magufuli alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita, zimeundwa tume nyingi kuichunguza Wizara ya Mambo ya Ndani kwa tuhuma za ubadhirifu na kuongeza kuwa wizara hiyo inaongoza kwa kukopa fedha wakati Wizara ya Fedha ndiyo yenye mamlaka ya kukopa fedha kwa niaba ya serikali.

Kabla ya Mwigulu, Charles Kitwanga aling’olewa katika wizara hiyo baada ya kudumu kwa mwaka mmoja pekee kwa tuhuma za kuingia bungeni akiwa amelewa na kushindwa kujibu vizuri maswali ya wabunge yaliyoelekezwa kwenye wizara yake.

Kabla ya hapo, Dk. Emmanuel Nchimbi aliondolewa katika nafasi ya uwaziri mwaka 2013 kwa shinikizo la Bunge baada ya kubainika kasoro kadhaa katika utekelezwaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili iliyofanyika nchi nzima kwa mwaka huo.

Miongoni mwa wabunge walioshinikiza viongozi wa serikali waliokuwa wametajwa katika ripoti hiyo kujiuzulu katika sakata hilo ni pamoja na Mbunge wa Mwibala, Kangi Lugola, aliyetaka Waziri Mkuu wa kipindi hicho, Mizengo Pinda, naye kuachia ngazi.

Akichangia hoja hiyo kwa hisia kali, Lugola alieleza operesheni hiyo iliendeshwa kijeshi kwa raia wa kawaida, hali iliyosababisha watuhumiwa kufanyiwa vitendo vya kikatili huku akimtaja mtu mmoja aliyelazimishwa kufanya mapenzi na mti.

Wakati Nchimbi anaondolewa katika wizara hiyo, aliondolewa sambamaba na Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki; Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk. Mathayo David.

Idadi ya mawaziri ambao wamehudumia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi tangu nchi imepata Uhuru ni pamoja na Sir George Kahama, aliyehudumu kwa mwaka mmoja (1961-1962).

Aliyefuata ni Oscar Kambona 1962 hadi 1963, Lawi Sijaona 1963 hadi 1965, Job Lusinde 1965 hadi 1967.

Mawaziri wengine waliofuata ni Said Maswanya mwaka 1967 hadi 1973, Omary Muhaji 1973 hadi 1974, Ally H. Mwinyi 1975 hadi mwaka 1976 alipojiuzulu na Hassan Moyo 1977 hadi 1978.

Salmin Amour aliteuliwa mwaka 1978 hadi mwaka 1980, Abdalah Natepe  1980 hadi 1983 na Mhidini Kimario 1983 hadi 1990, akiwa ni waziri pekee aliyedumu katika wizara hiyo kwa kipindi kirefu.

Akafuata Nalaila Kihula, aliyeteuliwa mwaka 1990 na kutenguliwa mwaka huo huo, nafasi yake ikichukuliwa na Augustine Mrema kuanzia 1990 hadi 1994, akafuatiwa na Ernest Nyanda 1994 na kutenguliwa mwaka huo huo.

Akateuliwa Ally Mohamed, mwaka 1994 hadi 1999, Mohamed Khatibu akateuliwa mwaka 2000 hadi 2002, Omary Mapuri 2003 hadi 2005, John Chiligati 2006 hadi 2008 na Lawarence Masha 2008 hadi 2010.

Mwaka 2010 akateuliwa Nahodha na kuondolewa mwaka 2012, na kumpisha Nchimbi aliyehudumu 2012 hadi 2013 na Mathias Chikawe 2014 hadi 2015.

Chikawe, aliyeondoka baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, alifuatiwa na Kitwanga aliyeteuliwa mwaka 2015 na uteuzi wake ukatenguliwa mwaka 2016.

By Jamhuri