Uongozi wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) iliyopo jijini Arusha, unazidi kuandamwa na kashfa mbalimbali. Safari hii imebainika kuwapo matumizi makubwa ya fedha kwenye ujenzi, utoaji zabuni na ununuzi wa vifaa.

JAMHURI imethibitishiwa kuwa ujenzi wa karakana ni miongoni mwa maeneo ambayo yametafuna fedha nyingi, huku ujenzi ukiendelea bila kuwapo bango linaloonesha ujenzi huo, kama sheria inavyotaka.

“Lengo ni kukwepa isijulikane na kuzuia mamlaka husika kama TBA kuja kukagua,” amesema mtoa habari wetu.

Sh milioni 300 zilitengwa awali kwa kazi hiyo, na mkandarasi akalipwa lakini baadaye akaondoka kazi ikiwa haijakamilika.

“Aliombwa kuendelea na kazi bila ya mafanikio. Baada ya muda mrefu akaonekana kama amerudi kufanya kazi, lakini kimsingi anayefanya kazi si yeye ni mtu mwingine nyuma ya pazia.

“Gharama zimepanda hadi Sh milioni 602 na bado zinaongezeka. Gharama hizo zimekuwa zikipanda bila ya idhini ya Baraza la Uongozi wa Chuo.

“Makamu Mkuu wa Chuo amekuwa na kawaida ya kuomba Baraza libariki matumizi ya fedha kwa kazi hiyo,” kimesema chanzo chetu.

 

Kulipa riba ya Karangai

Uchunguzi umebaini matumizi ya Sh milioni 500 zilizotumika kulipa riba kwa eneo lililonunuliwa la Karangai; kitu ambacho hakikuwamo kwenye mkataba wa ununuzi wa eneo hilo. Mkaguzi wa nje kwenye ripoti yake amebaini kuwapo kwa ufujaji huo wa fedha za umma.

Aidha, mashine mbili za ‘Kora System’ na ‘Sensor’ zilinunuliwa nchini Kenya kwa ajili ya maktaba bila kufuata kanuni za ununuzi, licha ya vifaa hivyo kupatikana hapa nchini.

 

Zabuni zenye utata

Chuo kilipoanzishwa kilikuwa kinatumia Bodi ya Zabuni ya Tanzania Atomic Energy, baadaye kikaunda bodi yake.

“Kimsingi, hakuna kipindi ambacho chuo kilikosa huduma ya Bodi ya Zabuni. Mkuu wa Taasisi amekuwa akiingilia mchakato wa utoaji zabuni,” kimesema chanzo chetu.

Kampuni ya REND inadaiwa kupewa zabuni mfululizo licha ya gharama zake kutajwa kuwa ni za juu.

“Kampuni hii imekuwa ikitumia maafisa kadhaa wa chuo na ofisi za chuo kuendesha shughuli zake, kwanini kampuni nyingine zinazoomba zabuni chuoni hazipewi nafasi hizo?” Amehoji mtoa taarifa wetu.

Uchunguzi umebaini kuwa mmoja wa maafisa wa kampuni hiyo, anayetajwa kwa jina la Sanga, anayehusika na ajira za wafanyakazi wa kampuni hiyo, amekuwa akisaidiwa na ofisi za Taasisi kufanya kazi zake.

“Bodi ya Zabuni ya Chuo ilipotaka ipatikane kampuni nyingine tofauti na REND, Makamu Mkuu wa Chuo aliingilia kati na kuiwezesha kampuni hiyo kupewa kazi eneo la utawala kwa sababu lina malipo makubwa kuliko maeneo mengine. Baadhi ya wajumbe wa Bodi hiyo inayokuwa chini ya Mwenyekiti Daniel Fisso, walitishia kujiuzulu,” imeelezwa.

Makamu Mkuu wa NM-AIST, Profesa Burton Mwamila, ameulizwa na JAMHURI na amesema: “Kiasi ambacho Kampuni ya RENDI ililipwa kwa mujibu wa mkataba wa kutoa huduma ya usafi chuoni hapo, ilikuwa ni Sh milioni 15.75 kwa mwezi.

“Japo Kampuni ya RENDI iliomba tena kupewa tenda ya usafi mwaka 2013/2014, lakini haikufanikiwa. Badala yake kampuni iliyoshinda na kupata zabuni hiyo mwaka 2013/2014 ilikuwa ni Care Sanitation & Suppliers Ltd.”

Malipo mengine yaliyoidhinishwa na Makamu Mkuu wa Chuo yanahusisha shughuli ya harambee aliyopewa raia wa Uingereza. Taarifa za Mkaguzi wa Ndani zinaonesha kuwa Mwingereza huyo amelipwa Sh milioni 100.

“Kwa nini asitumie wataalamu wa ndani ya nchi, au wa taasisi kwa kazi hiyo ya harambee?” Kimehoji chanzo chetu.

 

Ujenzi wa ‘incinerator’, uzio

Ujenzi wa kifaa cha kuteketezea taka (incinerator) umegharimu Sh milioni 50; lakini kumekuwapo malalamiko kuwa kiasi hicho cha fedha ni kikubwa mno kuliko kazi yenyewe.

Kiasi kingine cha Sh milioni 94.5 kimetumiwa kujenga uzio wa eneo la Karangai, na aliyepewa kazi hiyo ni mume wa mmoja wa wahadhiri wa chuo hicho. Uchunguzi unaonesha kuwa kuna malipo mengine ya shilingi zaidi ya milioni 20 yaliyoongezwa kwenye kiasi hicho cha awali.

Katika hatua nyingine, chuo kimetumia mamilioni ya shilingi kununua vifaa vya umeme kwa ajili ya pampu ya maji bila kutangaza zabuni. Vifaa hivyo vimekufa siku chache baada ya kufungwa na sasa vimetelekezwa hapo hapo kisimani.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwapo kwa idadi kubwa ya majengo yaliyojengwa chini ya kiwango. Miongoni mwa majengo hayo ni la utawala ambalo lina nyufa nyingi. Nyufa nyingi pia zipo Wing A, Wing D, Wing C na Wing B. Majengo haya yana umri usiozidi miaka mitano tu.

“Chuo kama cha Dar es Salaam kina miaka zaidi ya 50 lakini majengo yake bado yapo katika hali nzuri, hapa Mandela majengo yameshaanza kupasuka na hiki kinaitwa Chuo cha Sayansi na Teknolojia!” anasema mtoa taarifa wetu.

Katika hatua nyingine, uongozi wa NM-AIST umeanzisha ‘msako’ dhidi ya watumishi wanaodaiwa kuvujisha siri zinazoendelea kuchapishwa katika gazeti la JAMHURI.

Baadhi ya watumishi wanaodhaniwa kuvujisha siri hizo wamepata vitisho vya kufukuzwa kazi, kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kuvunja kanuni za utumishi.

Wakati mkakati huo ukiendelea, uongozi pia umekuwa ukitumia mamilioni ya shilingi kuvilipa vyombo vya habari na waandishi wa habari ili kusafisha ‘hali ya hewa’.

1434 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!