JWTZ yaifumua M23

*Wachakazwa kwa saa mbili, wakimbia waacha silaha, vyakula

*Yaelezwa wapo msituni wanashindia matunda kama ngedere

Majeshi ya kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) yanayoongozwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yameanza kupata mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya waasi.

Habari kutoka mashariki mwa Congo katika maeneo ya Goma, zinasema JWTZ wameonesha uwezo mkubwa wa kudhibiti waasi wa M23.

 

Mmoja wa maafisa aliyeomba jina lake lihifadhiwe, alisema waasi wa M23 tangu Julai mwaka huu wameanza kupeleka ujumbe kwenye vikosi vya Tanzania vilivyopo DRC, wakiwaomba wawasaidie kufanya mazungumzo na Serikali ya Congo ya Rais Joseph Kabila, badala ya kupigana vita. Hili M23 waliambiwa walifanye miaka yote wakalikataa.

 

“Hawa jamaa walitikisa kiberiti mwezi huu, wakidhani majeshi yetu ni legelege sawa na walivyozoea kuchezea majeshi ya Umoja wa Mataifa awali, wakakutana na watoto wa nyati waliojeruhiwa… JWTZ waliichakaza kwa saa 2 tu, muziki ulikuwa mzito.

 

“Wamekimbia maeneo yao, wakaacha vyakula kama unga, mchele, na vifaa vya vita kama bunduki na risasi, hivi sasa wapo msituni wanashindia matunda ya mwituni kama ngedere,” alisema mtoa habari wetu aliyeko mstari wa mbele.

 

“Baada ya kuchakazwa vilivyo, waasi hao wa M23 waliamua kufoji pasipoti wakaweka kwenye mtandao wakidai kuwa wamemkamata askari wa Tanzania, lakini katika kujisafisha wakasema hawatamtesa askari huyo, wanampa uji na ugali ale ashibe na kwa kuwa wanatuheshimu sisi Watanzania, watamkabidhi kwetu akiwa salama salimini.

 

“Kutokana na taarifa hiyo, tulilazimika kupitisha roll call tukakuta hakuna askari hata mmoja Mtanzania aliyekamatwa na waasi. Jingine lililotushangaza ni kwamba askari akiwa vitani hawezi kuwa na pasipoti yake. Askari anakuwa na namba maalum ambayo haruhusiwi kuivua muda wote wa vita hata kama anakwenda kuoga, kwa hiyo tukajua wanaugulia maumivu sasa wanatafuta huruma ya wananchi,” kilisema chanzo chetu.

 

Ukiacha mapigano ya mwezi uliopita, mapigano mapya yaliyoanza Julai 14, mwaka huu katika mji wa Goma, yameifanya Rwanda kupeleka barua ya malakamiko kwenye Umoja wa Mataifa, ikidai majeshi ya kulinda amani chini ya Umoja wa Mataifa yana ajenda ya siri ya kushirikiana na waasi wa FDLR kuingusha Serikali ya Kigali.

 

Balozi wa Rwanda kwenye Umoja wa Mataifa aliwasilisha barua ya malalamiko akisema majeshi ya Umoja wa Mataifa yanazungumza na waasi wa FDLR na pia yanawapatia silaha, huku Jeshi la Serikali ya Congo likiwaingiza waasi hao katika jeshi lake na katika kundi la makomandoo.

 

Msemaji wa Jeshi la Rwanda, Brigedia Jenerali Joseph Nzabamwita, Jumamosi jioni alilalamika kuwa majeshi ya kulinda amani na yale ya DRC yamerusha mabomu mawili ya nguvu nchini Rwanda katika vijiji vya Kageshi na Gasiza, vilivyopo Tarafa ya Busasamana na Wilaya ya Rubavu mashariki mwa Rwanda. Jenerali huyu alisema mabomu yaliyorushwa na mapigano yanavyokwenda inatishia usalama wa Rwanda.

 

Wakimbizi wapatao 700 walivuka mpaka kutoka Congo kwenda Rwanda kutokana na mapigano makali yanayoendelea. Kati ya waliokimbia inaelezwa kuwa wamo askari waasi wa kundi la M23, ambao wengi wana asili ya Rwanda.

 

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe, alipoulizwa na JAMHURI mwishoni mwa wiki, alisema majeshi ya Tanzania hayapo Congo kupigana, isipokuwa yanayo mamlaka ya kupigana chini ya Azimio la Umoja wa Mataifa lililoruhusu kupelekwa kwa majeshi.

 

Membe alipoulizwa iwapo pale DRC majeshi ya Tanzania na nchi za Malawi, Msumbiji na Afrika Kusini yana mamlaka ya kupigana tofauti na ilivyo kule Darfur nchini Sudan, ambako majeshi ya Tanzania yalivamiwa na waasi wakaua askari saba na kujeruhi 16, alisema:

 

“Wider mandate (mamlaka makubwa zaidi) ni ya Chapter 7 of UN Peacekeeping (walinda amani wa Umoja wa Mataifa), ambayo inatupa kibali cha kujitetea na kutwanga hasa! Chapter 6 ya Darfur ni ya kujihami tu. Pale DRC ni Chapter 7,” alisema Membe bila kufafanua zaidi, akiacha kila mtu atafsiri kinachoendelea chini ya Chapter 7 huko DRC.

 

Hata hivyo, Membe alisisitiza JWTZ hawako pale kupigna na waasi ila kama imetokea wakawa ‘wamewatwanga’ M23 ilikuwa ni katika kulinda maisha ya wananchi wasio na hatia.

 

“Hatuko pale kuwapiga M23, ila kama wakibaka wanawake, wakaua watu wasio na hatia, wakalazimisha watoto kuingizwa kwenye jeshi lao, hatutawaacha,” Membe aliiambia JAMHURI.

 

Waziri huyo alisema kwa hali ilivyo, Tanzania inayoongoza majeshi ya nchi zinazoshiriki kwenye kikosi hiki cha kulinda amani, haitaki kupiga kelele ila Wakongo na dunia kwa ujumla itarajie ushindi na amani kurejea Congo ndani ya muda mfupi ujao.

 

Membe alisema kiu ya Tanzania ni kuona amani inarejea na si vinginevyo, na akasema hao M23 wanaosingizia kuwa wanamheshimu Mwalimu Nyerere wathibitishe kwa vitendo kuwa wanamheshimu Nyerere kwa kuacha vita.

 

Tanzania ina historia iliyotukuka katika ukombozi wa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara na ndiyo maana imechaguliwa kuongoza majeshi ya kulinda amani nchini DRC.

 

Mwaka 2008 makamanda na wapiganaji wa JWTZ waliongoza vikosi vya washirika katika kazi ngumu ya kumng’oa Kanali Bacar wa Visiwa vya Comoro na Anjouan. Uamuzi wa AU kuipa kazi hiyo Tanzania kuongoza mapambano hayo haukuwa wa bahati mbaya, bali ulitokana na kuitambua kuwa ni nchi iliyoshiriki na kufanikiwa katika vita mbalimbali ya ukombozi.

 

JWTZ imeshiriki operesheni nyingi kwa mafanikio makubwa. Kuna Operesheni Kumekucha dhidi ya Wareno mwaka 1960; Operesheni Tegama – Msumbiji, dhidi ya majeshi ya Rhodesia na Afrika Kusini (1975-1980); Operesheni Safisha – Msumbiji, dhidi ya Mozambican National Resistance au Resistência Nacional Moçambicana (RENAMO) mwaka 1986-1988; Operesheni dhidi ya mamluki waliovamia Kisiwa cha Ushelisheli mwaka (1981-1982) na Operesheni Demokrasia Comoro (Machi 2008) ili kumuondoa Kanali Bacar kutoka kisiwa cha Anjouan.

 

JWTZ imeshiriki katika operesheni za kulinda amani chini ya Majeshi ya Umoja wa Mataifa. Mifano ya karibuni ni ya Liberia, Darfur na Lebanon. JWTZ ina hazina kubwa ya uzoefu kutokana na operesheni hizo. Siri kubwa ya mafaniko ya JWTZ ni umoja, ujasiri, nidhamu na weledi.

 

Mwaka jana, M23 waliandika barua kuomba JWTZ wasiende nchini Congo kwa maelezo kuwa Watanzania ni ndugu zao hivyo hawataki kuua askari wa Tanzania. Kipigo walichopata kimethibitisha bila shaka kwa nini walikuwa wanaomba JWTZ wasiende huko.

 

2216 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!