Sitaki iwe mbali, bali mapema sana kesho asubuhi nataka nitii bilakushurutushwa na mtu yoyote maana wengine wameishasema kuwa wamechoka na mchoko wao wameishauhalalisha kwa kupitisha amri, amri ambayo mahakama imethibitisha kuwa ilikuwa amri ya iliyopungukiwa vigezo kutoka kwa mtoto wa mkulima.

Mtoto huyu amezoea mji na kuanza kupinda.”…Mtapigwa tu, nami nasema mpigwe tu, maana sasa tumechoka…” Ndio, tumeshaanza kupigwa na tutapigwa tu!

 

Kesho asubuhi na mapema nafanya uamuzi wa busara. Busara imenituma nianze kuwaamini polisi, walinda usalama wetu na amani yetu. Polisi wenye mapenzi mema na nchi yetu, polisi wanaolinda na si kuua raia wa nchi hii, polisi wanaolipwa kwa kodi za Watanzania, polisi wenye mabomu, magari ya maji ya kuwasha na bunduki zinazotokana na kodi za Watanzania, nataka kuwaamini kwa moyo wote.

 

Ninachohitaji ni mwongozo! Kesho nataka kuwaamini polisi waliokuwa pale uwanja wa ndege wa KIA ambao hawakuona twiga wetu wakikunjwa shingo kama karatasi na kusokomezwa kwenye ndege ya Waarabu. Nataka kuwauliza ili niwaamini.

 

Twiga akikunjwa shingo yake huwa anafananaje? Nataka kuwauliza kama twiga wale walipiga kelele walivyokunjwa na kusokomezwa kwenye ndege au walifurahia na kukaa kimya.

 

Kesho nataka kuwaamini polisi ambao gari yao ilikamatwa ikiwa inasafirisha bangi na wao wenyewe wakaikamata. Kesho nataka kuwaamini polisi waliomchukua mtu akiwa mzima na kumrejesha akiwa mfu. Ni kesho tu, nataka kujua kuhusu wale polisi wa Morogoro waliombambikiza mfanyabiashara wa watu kichwa cha binadamu aliyeuwawa wanako kujua wao kwa malengo yao.

 

Nataka kuwauliza lengo lao lilikuwa nini, wakati nawauliza nitawatahadhirisha maelezo yao yasije yakajichanganya na tukio la kitu kizito chenye ncha kali kilichotoa uhai wa Ally Zona kwenye maandamano ya kile chama kilichokataa kukabidhi ushahidi kwa polisi kwa madai eti polisi ni wahusika wamlipuko wa bomu kule Arusha.

 

Polisi ndio wenye mabomu iweje wawe wahusika? Kesho nataka kuwaamini polisi wale ambao waliiba mishahara yao na pesa za wafanyabiashara waliokwapuliwa pesa zao na majambazi pale Kariakoo.

 

Ni kesho tu, nataka kuwaamini polisi ambao hawana historia ya kubambikizia mtu kesi, wala kumsingizia raia mwema asiye na hatia maana wengi walioko jela wana hatia zisizofungamana na mikono ya polisi, wala ushawishi wa polisi.

 

Kesho asubuhi na mapema nataka kuwaamini polisi baada ya kusoma taarifa ya uchunguzi wao makini uliomtia hatiani Joseph Mulundi yule raia wa Kenya aliye mteka, kumtesa na kumng’oa kucha na meno Daktari Steven Ulimboka halafu akaenda kutubu kule kwa Mchungaji Gwajima.

 

Kesho ndio kesho, maana hata ya Daudi Mwangosi yatakuwa hadharani. Nina imani na Kamuhanda maana kazi nzuri ndio imemfanya amepandishwa cheo, si kingine naamini tukio la kulipua bomu bahati mbaya kwa kusaidia kuokoa maisha ya Mwangosi ndio kumempandisha cheo na kupewa hongera na pongezi nyingi na Waziri wa JK.

 

Kesho ndio siku ambayo huenda sitaamini kuwa polisi wanalipua mabomu japo wamekiri kuwa kulipuka kwa mabomu ni jambo la kawaida, na wao ndio wenye mabomu. Yakilipuka ujue ni wao sema tu kwa bahati mbaya!

 

Nataka kuamini kuwa hawahusiki na kulipuka kwa bahati mbaya au makusudi kwa bomu la pale Soweto Arusha kama jinsi ilivyo kuwa bahati mbaya kwa Mwangosi na juzi pale Ubungo kwenye mkutano wa Mnyika.

 

Nani ataniongoza nataka kuwaamini polisikuwa hawahusiki na mabomu! Nataka kuwaamini polisi, sitaki kuamini ile ripoti niliyo isoma kwenye gazeti la “The East African” la tarehe 8 Aprili, 2013; ambalo eti ripoti yake inaonyesha kuwa Jeshi la Polisi linaongoza kwa uonevu, kutunga kesi zauongo, kubambikiza kesi na makosa makubwa ya uongo ambayo kisheria hayana dhamana, makosa ya mauwaji, makosa ya kutumia nguvu na makosa ya ugaidi.

 

Eti kwa mujibu wa ripoti hiyo, Jeshi la Polisi linahitaji kusafishwa maana limekuwa ni jeshi la kihalifu. Mimi haya yote sitayaamini na siyaamini. Ninachohitaji ni mwongozo usiokuwa na shaka kwa ya jeshi letu la polisi japo Lwakatare amefutiwa kesi yake ya ugaidi.

 

Nataka kuamini kuwa FBI wapo Arusha kuchunguza tukio la bomu kama tulivyotangaziwa na afande wetu wa mkoa kuwa FBI na wataalamu kutoka China wako kazini kule Arusha. Sitaamini ile taaarifa ya Ubalozi wa Marekani nchini kukana eti kuwa FBI hawapo Arusha.

 

Taarifa ya Ubalozi wa Marekani niya kichochezi na haina ukweli. Kwa kuwa nataka kuwaamini polisi nitaamini taarifa ya polisi wetu si ile ya Wamarekani ambao hata ujio wa Rais wao hawakuamini ulinzi wetu eti wamepekua mpaka viongozi wetu wakuu wa polisi!

 

Wale jamaa hawafai na hapaswi kuaminiwa! Kwa lugha ya mipasho kutoka Magogoni Modern Taarabu wale jamaa ni “vizabi zabina wanaotapatapa”. Nataka kuwaamini polisi wanaosingiziwa kuwa eti wanawaogopa wanasiasa wa chama tawala wenye ushahidi wa matukio makubwa ambao wanaweza kuutoa hata mbele za Mungu, lakini eti polisi wetu wanakuwa na busara hadi pale Mungu atakapo waita ili wakatoe ushahidi wao huko.

 

Chama tawala hawana shida napolisi ila nataka tu kuamini maneno ya JK kwa chama tawala “… Na nyinyi muache kuwategemea polisi.” Nataka kuwauliza kama ni kweli polisi huwa wanawabeba CCM hadi kuitwa Poli-CCM au JK aliteleza tu ulimi?

 

Polisi wanaaminika bwana, iweje? Kesho ndio kesho, nataka kusikia ili niwaamini polisi. Nataka kusikia kama wanatumia nguvu zilezile za kwenda usiku kwenye nyumba ya Mbowe au Lema kama wamewahi kufanya hivyo hivyo kwa walio kwapua hela za Kagoda, EPA,Meremeta, Deepgreen na Kawira?

 

Nataka kujua pia kama wameshawahi kuvamia Magogoni usiku wa manane kumshurutisha Msafiri ataje majina ya wauza unga ambayo anayo chini ya godoro lake. Sema anaamua kufanyanayo safari kila kukicha!

 

Kesho itakuwa historia polisi watakapoonekana na kuniambia ukweli kuwa wote wanaoingia depo kule CCP ni wenye sifa na huwa hakuna rushwa bali wanasingiziwa. Majibu yao lazima niyaamini maana nataka kuwaamini. Naisubiria kesho kwa hamu.

 

Nipe mwongozo nisubirieje? Nilindwe na ‘green guard’ au ‘red brigade?’ “Tukosoane, Turekebishane, Tuwajibishane, ndipo Tusameheane”. Regia Mtema.

 

Mwandishi wa makala haya, anapatika na kwa Na 0713246764 au 0784246764.

1155 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!