Rais wa Marekani, Donald Trump, anadai kuwa dawa maarufu inayotibu malaria imethibitika nchini humo kuwa tiba dhidi ya virusi vipya vya corona.

Klorokwini ni dawa ya zamani inayokubalika zaidi kama dawa sahihi kupambana na malaria duniani.

Watu wanajiuliza, je, Trump yupo sahihi?

Klorokwini imedumu kama dawa ya malaria kwa miongo kadhaa na kwa sasa haitumiki katika maeneo mengi ya Afrika, ikidaiwa ni kutokana na usugu wa wadudu wa malaria dhidi ya dawa hiyo.

Yapo mataifa yamepiga marufuku kabisa dawa hiyo lakini imeendelea kuwa na umaarufu katika sekta binafsi ya afya ikiuzwa kwa wingi maeneo kadhaa duniani.

Nigeria ni miongoni mwa mataifa yaliyoendelea kutumia klorokwini ingawa tangu Trump alipoitaja kuwa inaua virusi vya corona, imeadimika.

Katika utaratibu wake wa kutoa taarifa kila siku, Trump alidai kuwa klorokwini imethibitishwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (FDA) ya Marekani kudhibiti corona.

“Tutafanya kila linalowezekana dawa hiyo ipatikane mara moja. Hapo ndipo FDA ilipofanya vizuri kabisa. Wamepitia mchakato mzima na kuthibitisha,” anasema Trump.

Hata hivyo, FDA wameweka wazi kuwa klorokwini haijathibitishwa kutibu wanaougua COVID-19, ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona.

“Hakuna dawa au chochote kilichothibitishwa na FDA kutibu au kukinga COVID-19,” imedai taarifa rasmi ya FDA, ikiongeza kuwa, hata hivyo, utafiti unaendelea kuona uwezekano wa dawa hiyo kupambana na COVID-19, na kwamba wameelekezwa na Trump kufanya utafiti wa kina wa kitabibu.

Baadaye, Trump akasema klorokwini imethibitishwa kwa kile alichokiita ‘compassionate use’, ambapo daktari anaweza kumpa mgonjwa aliye katika hatari ya kufa dawa hata kama bado hairasimishwi na serikali.

Katika hali hiyo, madaktari wanaweza kumpa mgonjwa klorokwini, kwa kuwa ni dawa halali Marekani.

Wanasayansi nchini Marekani wameanza kufanya utafiti wa kina kuangalia uwezo wa klorokwini huku msimamo wa wenzao duniani wakiwaunga mkono.

Kwa mujibu wa wataalamu, klorokwini ni miongoni mwa dawa zinazofahamika sana duniani, hazina gharama na rahisi kuzalishwa. Katika kutibu malaria, hupunguza homa na dalili nyingine za malaria.

“Katika maabara, klorokwini imeonekana kuzuia virusi vya corona. Kuna uthibitisho kutoka kwa baadhi ya madaktari kuwa inasaidia sana,” anasema James Gallagher, mwandishi wa habari za afya wa BBC.

Lakini kwa hakika hakuna majaribio ya kitaalamu kuthibitisha namna dawa hii inavyofanya kazi kwa mgonjwa wa corona ingawa uchunguzi unaendelea huko China, Marekani, Uingereza na Hispania.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema hadi sasa hakuna uthibitisho wa uhakika katika suala hilo, lakini kazi inaendelea.

“Lazima kuwepo na majaribio katika maabara kisha ya kitabibu ili kuthibitisha ubora wa dawa kwa wagonjwa,” anasema Profesa Trudie Lang, Mkurugenzi wa Mtandao wa Afya kutoka Chuo Kikuu cha Oxford.

By Jamhuri