Katika kukabiliana na ugonjwa wa homa kali inayosababishwa na virusi vya corona, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amewataka maofisa afya kwenye mipaka yote nchini kufanya ukaguzi wa kina kwa wageni wanaoingia nchini badala ya kuishia kwa kuwapima joto la mwili pekee.

Waziri Ummy ameyasema hayo wiki iliyopita akiwa katika mpaka wa Namanga, wilayani Longido mkoani Arusha katika ziara yake ya kukagua maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya washukiwa wa ugonjwa huo.

“Kama mtaishia kupima joto la mwili pekee kuna uwezekano mkubwa wa kupitisha watu wenye virusi vya corona kwa sababu kitaalamu iwapo mtu atakuwa anatumia dawa za kutuliza maumivu kama ‘Panadol’ joto lake huwa si kali. Kwa hiyo kwa kuangalia tu joto bado tutakuwa hatujafanya kazi vizuri,” anasema.

Amewataka maofisa hao kuhakikisha wanachunguza historia ya mgeni kwa kuangalia sehemu alikotoka iwapo ni miongoni mwa nchi zenye maambukizi ya corona, hivyo kupata taarifa sahihi na za kina zitakazosaidia kukabiliana na tatizo hilo.

Akikagua sehemu maalumu iliyotengwa kwa ajili ya washukiwa wa ugonjwa huo katika Hospitali ya Rufaa ya

Mount Meru jijini Arusha, Waziri Ummy alitoa wito kwa waganga wakuu wa hospitali zote nchini kuweka

utaratibu wa wagonjwa kutembelewa na ndugu zao.

“Kama ambavyo rais ametangaza kuwa tuhakikishe hakuna misongamano sehemu yoyote, ninaagiza kila hospitali ihakikishe wagonjwa waliolazwa wasitembelewe na ndugu wengi. Hakikisheni wanaowatembelea wagonjwa wao wasizidi watu wawili kwa mgonjwa mmoja.

“Niwatoe hofu watumishi wa afya, serikali tunawahakikishia kuwa tutawalinda kwa kuwapatia vifaa vyote vya kujikinga na katika mazingira ya kazi. Pia niwatoe hofu wakazi wa hapa Arusha wasiogope kuja kupata huduma Mount Meru kwani sehemu iliyotengwa kwa ajili ya washukiwa haiingiliani kabisa na wagonjwa wengine,” anasema Ummy.

364 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!