Martial anapoonyesha ushujaa

Kama mzaha Septemba 12, mwaka huu Luis van Gaal, alifanya mabadiliko katika mchezo wa Ligi Kuu England, ambako katika dakika ya 65 alimtoa Juan Mata na nafasi yake kuchukuliwa na Anthony Martial.

Kijana huyo, usajili mpya’ aliyezaliwa Desemba 12, 1995 ni kama alipuuzwa na Liverpool, lakini ndiye aliyewaliza majogoo hao wa London katika mchezo ambao Mashetani Wekundu waliibuka kwa ushindi wa mabao 3-1.

Jumapili iliyopita, kijana huyo alianza kucheza tangu mwanzo katika mchezo dhidi ya Southampton ambako licha ya kutangulia kuongoza, lakini alikuwa ni Martial aliyesawazisha kabla ya kupiga la pili katika ushindi wa mabao 3-2. Bao la tatu lilifungwa na Mata.

Ikaja Jumatano iliyopita kwenye mchezo wa Ligi maarufu kama Capital One huko England, United ikiwa inaongoza kwa mabao 2-1, Martial pia aliingia kuchukua nafasi ya Mata kuongeza nguvu ambako akapiga bao la tatu katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Ipswich Town.

Uwezo wa Martial umemuibua Sir Alex Ferguson, ambaye mara moja anasema, “Man United imewadhuluma AS Monaco kwa kumnunua kwa dau la pauni milioni 36 badala ya dau kubwa zaidi ya hapo.” 

Hakuna ubishi kwamba Martial ameshangaza wengi kwa ushujaa wake kwani wakati anasajiliwa hakuna shabiki wa United aliyesisimka kama alivyosajiliwa Morgan Schnedellein au Memphis Depay. Ndiyo, usajili wake ulionekana ni mwepesi zaidi kuliko hata usajili Sergio Romelu.

Mashabiki walinuna na wengi wao walihoji iko wapi ahadi ya usajili mkubwa wa kushangaza aliohaidi Van Gaal. Yawezekana kutopokelewa kwa shangwe kulimsaidia Martial kutokuwa katika presha kubwa na kushangaza wengi katika mechi zake chache alizocheza.

Kwa sasa, katika vijiwe mbalimbali, mashabiki wa United wanatamba wakisema LVG aliahidi ‘surprise’ akashindwa kuitimiza na hatimaye kinda huyu amekuja kumshangaza yeye LVG na mashabiki wote na zaidi amemfungua mdomo Sir Alex.

Kijana huyu alichekesha walionuna kwa hasira za kufungwa kwa usajili bila usajili wa straika wa maana amebadili kila kitu ndani ya Manchester United. 

Baada ya dirisha la usajili bila usajili wa straika wa maana mashabiki wengi wa United walikasirika sana. Hata wale waliosema Wayne Rooney anatosha kuwa straika mkuu walimlalamikia kocha kwa kushindwa kumsajili Edson Cavan, Robert Lewandowsk na zaidi Pedro ambaye alikuwa tayari ameshaanza kuaga wachezaji wenzake pale Cataluna kwamba anakwenda United, lakini dakika za mwisho Ed Woodward akiwa ameshapanda ndege kwenda Hispania kumalizana naye, LVG akasema, “Hapana, huyo simuhitaji hapa.”

Pedro akatimkia Chelsea jambo ambalo liliwauma mashabiki wengi wa United na hapo wakaombea dirisha lifungwe kuliko kuendelea kuumiza mioyo yao. Ligi ilianza wengi wakiwa na vinyongo, lakini Martial anaonekana kusahaulisha hasira za mashabiki hawa.

Kabla ya usajili wake, Luke Shaw aliyekuwa anashikilia rekodi ya usajili ghali wa kinda ulioigharimu United Pauni milioni 27 msimu uliopita huku yeye akinunuliwa kwa Pauni milioni 36 kwa mkataba wa miaka minne.

Wengi wanasema Harry Kane alistahili kukamata rekodi hiyo, lakini mashabiki wa United wanambeza na kusema kwa Martial wao huyo Kane asubiri kwanza. Sasa mashabiki wote macho yapo kwa kinda anayefanya mambo makubwa kinyume kabisa na matarajio yao.

Ni dhahiri kuwa mechi ambazo United wangefungwa lawama zote zingeelekezwa kwa mastaa hao wawili wa United. Depay ameomba jezi namba 7 ambayo ina historia kubwa United jambo ambalo linaashiria mashabiki kusubiri mambo makubwa kutoka kwake.

Rooney alikuwa ndio tumaini kubwa la magoli ndani ya United kama straika pekee. Hakika Martial amewaokoa na lawama mastaa hawa na kuwafanya wawe amani na kupunguziwa presha iliyokuwa inawafuata jambo ambalo linawasaidia kurejea katika ubora wao uliotarajiwa.

Katika hali ya hemwahemwa ya mashabiki kutokana na uwezo wa kinda huyu wengi wanahoji ulegevu wa Januzaj wakati kinda mwenzake ameonesha kujiamini na kucheza mpira wa malengo zaidi kuliko kupoozesha mashambulizi kunakofanywa na Januzaj.

Wengi wanasema kama Martial amepewa nafasi na ameonesha mwanzo mzuri, kwanini Pereira naye asipewe nafasi pana kuonesha uwezo wake klabuni hapo?

Uwezo wa Martial unafanya Rooney kucheza kama namba 10 na Martial namba 9 jambo linalomfanya Fellain aliyehamishwa kutoka kiungo kwenda nafasi ya ushambuliaji kupoteza matumaini ya kupata nafasi.

Ni ngumu kwa Fellain kuliko katika nafasi ya kiungo kugombania nafasi dhidi ya Michael Carrick, Morgan Schnedellin, Bastian Schwesteiger, Juan Mata, Ander Herrera na wengineo, inabidi agangamale nafasi ya mbele ambayo makindi kama Martial, Pereira na Rooney wanapewa nafasi kubwa kuanza msimu huu.

Maelewano ya haraka kati ya Depay na Martial yanafanya Young asubiri kwanza nje mpaka vijana hao wapoteane. Young ni mchezaji muhimu United na historia nono kwa ajira mpya ya Van Gaal ndani ya United lakini upacha mpya wa makinda hawa wawili ndani ya United unahatarisha nafasi yake.

Siku za karibuni kumekuwa na uvumi kuwa wachezaji hawana furaha ndani ya klabu hiyo ya jijini Manchester kwa kuwa kocha huyo amekuwa akiwabana na kuwafuatilia kama watoto wadogo.

Kumekuwa na uvumi kuwa kocha LVG amekuwa hamshirikishi vyema Ryan Giggs katika majukumu yake na yeye amegeukia Waholanzi wenzake madai ambayo yanaonekana na kama yanafanana na tuhuma za kocha kumpendelea Robin Van Persie.

Moto wa Martial umefanya mashabiki kuweka silaha chini na kuangalia anachofanya. Ni mapema mno kusema Martial ni kila kitu ndani ya united lakini amekuwa na mwanzo mzuri sana ambao wengi wamekuwa wakisema kama hatapata majeraha itakuwa “gud gud”.

Martial alizaliwa Desemba 5, 1995 katika mji wa Massy huko Ufaransa. Anacheza nafasi ya ushambuliaji akiwa ndani ya jezi namba 9 huku urefu wake ni meta 1 na sentimeta 81. Mwaka 2001-2009 alikuwa anapika pale katika academy ya CO Les Ulis kisha akiwa na miaka 14 maskauti wa Olympiques Lyonnais walimmulika na wakamvuta katika Academy yao.

Hapo alilelewa mpaka alipoanza kuchezea timu ya wachezaji wenye umri chini ya miaka 17 na ndipo alipong’arisha nyota yake kwa kufunga magoli 32 katika mechi 21 na huo ndio ulikuwa mwanzo wake wa kuitwa timu ya taifa lake la Ufaransa.

Alicheza Ligi Kuu Ufaransa na klabu yake ya Lyon Februari 3, 2013 kwa mara ya kwanza dhidi ya Ajazio katika kipigo cha 3-1. Msimu huo alicheza mechi 3 tu na 30 Juni 2013 AS Monaco walimsajili kwa euro milioni 5 ambako pamoja na bonas ilifika euro milioni 6 Novemba 24, 2014 alicheza mechi yake ya kwanza Monaco akichukua nafasi ya Radamel Falcao dakika ya 63 ambapo alitoa pasi ya goli katika mechi hiyo. 

Mkataba wake wa Monaco ulirefushwa mpaka mwaka 2019 baada ya kufunga magoli 9 katika mechi 36 ukiwa ni msimu wake wa pili. Agosti 4, 2015 alifunga goli lake la kwanza katika michuano ya UEFA hatua ya mtoano timu yake ikishinda goli 4-0 dhidi ya BSC Young Boys.

Septemba 1, 2015 kinda Anthony Martial akatua Manchester United ambako amekuwa na mwanzo mzuri.

 

Baruapepe: [email protected] 

Simu: 0715 36 60 10