MeruSoka la Tanzania kwa sehemu kubwa linaharibiwa na midomo ya mashabiki na ulegevu wa wachezaji.

Mashabiki wanaweza kumsakama mchezaji kwa kumzomea au kumzeesha na kumtangazia kuwa “amechuja” mpaka anapotea kwenye ramani ya soka.

Mashabiki na wadau wengine wa soka huwa wanawaua wachezaji kisaikolojia kwa kumjengea udhaifu ambao hana na mchezaji akiupokea tu anauishia huo udhaifu na kucheza kwa mang’amung’amu kisha anabaki kuwa historia.

Kisaikolojia mtu huanza kuharibika au kujengeka kiakili kabla vitendo vya kujengeka au kuharika huko hakujadhirika nje.

Ili mtu aharibike au kujengeka lazima kuwe na msukumo wa ndani na au vya nje. Moja ya vitu vinavyoharibu wachezaji ni vichocheo vya nje (zomea zomea) na ili kuvishinda basi imempasa mchezaji kuwa imara ndani (kiakili) ambako watu kama Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma Kaseja na Ivo Mapunda.

Hakuna kipindi kigumu kwa wachezaji kama kipindi cha kuzomewa na mashabiki wa timu yake. Huwa inawachanganya zaidi wanapomzomea mchezaji huku wakimshinikiza kocha amtoe mchezaji huyo. Kuna makocha wachache wenye uwezo wa kumudu kumchezesha mchezaji anayezomewa na mashabiki. 

Mholanzi Hans van Pluijm wa Yanga ni mfano kwani alipoulizwa kwanini hakumchezesha Simon Msuva katika mechi ya robo fainali Kombe la Kagame dhidi ya Azam, alijibu: “Alizomewa na mashabiki mechi iliyopita.”

Kocha alifahamu Msuva hakuwa vizuri kisaikolojia kutokana na kelele za mashabiki japo kama kocha hakuwa na tatizo na uwezo wa mchezaji huyo. Hapo unaweza kuona namna ambavyo mashabiki walivyomudu kumuweka Msuva benchi kabla ya kocha kutii uamuzi wa wanazomeazomea.

Ni heri kwa Msuva ambaye anazomewa na kushangiliwa, ni heri ya Msuva anapigwa benchi la zomeazomea na kumudu kurudi uwanjani na kushangiliwa jambo ambalo wachezaji wengi linawashinda na huo ndio unakuwa mwanzo wao wa kuangamia katika ulimwengu wa soka. 

Katika mazingira haya ya kubeza wachezaji kwa kupima mechi mbili au tatu ndipo wachezaji wengi hupotea hata kama walikuwa katika rekodi zilizotukuka uwanjani. Kuna wachezaji wachache pia wanaomudu kubezwa na kurejea katika ubora wao, wengi wao wanapopata misukosuko kama hiyo hujiangamiza kwa kuanza kujibizana na mashabiki badala ya kuwajibu kwa vitendo.

Kazi ya mashabiki kuzomea na kushangilia, lakini mchezaji anapozomea mashabiki anakuwa anajiangamiza mwenyewe. Mchezaji anatakiwa kujibu kwa vitendo jambo ambalo Cannavaro analimudu vyema ukilinganisha na wachezaji wengi hapa Tanzania. Katika kipindi kama hicho cha ugumu inatakiwa mchezaji kuwa mbunifu kwa kujiboresha na kujiimarisha bila kupiga mayowe ya kutafuta huruma. 

Huruma za mashabiki zinapatikana kwa kuonesha vitendo vya uhakika vya kiuchezaji vitakavyogusa mioyo ya mashabiki. Kwa nyakati tofauti ikiwepo hapa karibuni Cannavaro ametajwa kuwa ni mchezaji ambaye kiwango chake kimeshuka.

Bahati njema mashabiki hawakuwahi kumzomea na hata sasa hawawezi kumzomea na kinamchosaidia Cannavaro asizomewe ni heshima na utulivu uliojijengea katika ulimwengu wa soka kwa nyakati zote za kucheza kwake soka. 

Mashabiki na wadau wa soka wananong’ona chini chini kwamba “Cannavaro amekwisha”. Mashabiki hawana hoja za kisoka zaidi ya kulazimisha kumzeesha mchezaji huyo kwa madai kuwa amechoka.

Hawasemi kuwa amechoka kwa kuwa amepambana mechi nyingi mfululizo za klabu yake ya Yanga timu ya Taifa, wao wanasema umri umemtupa. Kwanini wadau wa soka wanakosa shukrani? 

Cannavaro amepambana miaka miwili mfululizo kwa ajili ya timu yake ya Yanga na Taifa lake, lakini ajabu ni kuwa mashabiki hao wanashindwa kumshukuru ila wanauona uzee wake, kwa uzee upi alionao Cannavaro? Mashabiki hao hao ndio walimpigia kelele Kaseja kuwa amezeeka badala ya kumpa pole ya uchovu wa kuipigania klabu yake ya Simba na Taifa lake. Leo Ivo Mapunda tayari amekuwa si lolote wala chochote pale Msimbazi, ameonekana “babu” na imebidi akajibanze huko Azam FC akivizia usajili siku za usoni. 

Wachezaji wengi Tanzania wanazeeshwa kabla hawajazeeka. Hawa wabongo wanaowapigia kelele Cannavaro, Ivo na Kaseja ndio hao hao wanamshangilia Berbatov, Etoo, Buffon, Pirlo, Lampard, Terry, Casilas, Evra na wengineo huko Ulaya.

Ni mara ya pili sasa katika kipindi cha miaka mitatu Cannavaro anatajwa kuwa amezeeka na hana jipya lakini ubunifu wake ndio huwazibika midomo wote wanaomzeesha. Cannavaro ni kiongozi uwanjani na msemaji mzuri wa timu anapohitajika kufanya hivyo. 

Katika nyakati ngumu yeye amedumu katika utulivu na kuwa msaada wa timu. Mara ya mwisho aliposemwa vibaya kuwa amekwsha kwa uzee wake aliamua kurejea kwa kuwa kisiki maradufu huku akifunga magoli muhimu kwa timu yake na hapo uzee ukasahaulika.

Mchezaji yeyote ambaye ameamua kucheza mpira kwa mafanikio anatakiwa kuwa na roho ngumu ili mpira wake usipotezwe na mashabiki wa soka wanaosahau mema na kukwepa ukweli. Wakati wanaposema Cannavaro amezeeka hawasemi ni kijana yupi anaweza kuwa kiongozi kama Cannavaro kwa klabu yake ya Yanga na timu ya Taifa. 

Ni wazi wengi wanapenda tu kuwa watabiri wa mwisho wa soka la mchezaji lakini hawapimi thamani ya mchezaji huyo kwa timu. Kwani toka Simba waliposema Kaseja amezeeka waliwahi kupata kiongozi wa wachezaji uwanjani na kufikia hata robo ya mafanikio ya uongozi wa mchezaji huyo?

Kama hakutokea maana yake uzee wake bado ulikuwa dawa kwa timu yake. Ivo Mapunda alipopigiwa kelele za kushuka kiwango kwa “uzee” wake alitimkia Kenya alikogeuka lulu na hatimaye Simba wakamrejesha nyumbani. Amedakia timu vyema huku ikiwa haina na kumlea kinda Manyika Peter Jr leo tayari amepoteza thamani yake kwa uzee. 

Ninawatazama Cannavaro wa Yanga, Kaseja wa Mbeya City na Ivo Mapunda wakija na ubunifu utakaowaboresha na kuwasuta wote wanaouona uzee badala ya shukrani kwa juhudi na bidii mfululizo kwa timu zao.

Walau kupitia haya wachezaji wajifunze kuwa na ngozi ngumu maana ndivyo mashabiki walivyo na kwa hilo Msuva anastahili pongezi maana anawasikia wakimzomea na kumshangilia mara kwa mara.

Wachezaji wanahitaji kufahamu kuwa mashabiki wanataka kuona mchezaji anacheza vyema mechi zote na akiyumba mechi mbili au tatu, tayari watamtafutia sababu ya kumshusha morali. Akiwa na umri mkubwa watasema amezeeka na akiwa kijana watamuambia ameendekeza anasa au ana akili ya kitoto ili mradi lawama. Kwa hiyo mazingira kama haya ndiyo hunifanya nihimize mara kwa mara wachezaji kuwa na wataalamu wa saikolojia ili wawasaidie kuwarejesha mchezoni kila wanapoondolewa mchezoni kwa viroja. 

Ninasubiri ubunifu wa Kaseja na Cannavaro utakaowarejesha katika ubora wao ili tujifunze kuheshimu na kuwavumilia wachezaji pale wanapopitia nyakati ngumu katika uchezaji wao. 

 

Baruapepe: amrope@yahoo.com 

Simu: 0715 36 60 10

2220 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!