Tanzania ya leo inafuata mfumo wa vyama vingi. Katikati ya mfumo wa vyama vingi Watanzania wamegawanyika katika makundi makuu matatu.

Kundi la kwanza ni la Watanzania  wanaounga mkono chama tawala na serikali yake katika kila kitu. Ni kundi ambalo linaamini kwamba chama tawala na serikali yake viko sahihi wakati wote.

 

Kundi la pili ni la Watanzania mashabiki wa vyama vya upinzani. Ni kundi ambalo linaona kwamba vyama vya upinzani viko sahihi wakati wote na chama tawala na serikali yake vinafanya makosa wakati wote.

 

Kundi la tatu ni la Watanzania ambao hawafungamani na upande wowote. Baadhi yao wanaona kwamba masuala ya siasa si yao na kwamba siasa haiwasaidii.

 

Katika mgawanyo wa majukumu, jukumu la serikali ni kutawala ambako pia ni pamoja na kudhibiti tabia za watu. Kwa upande mwingine, jukumu la chama cha siasa ni kuhubiri siasa.

 

Kwa upande wa chama tawala jukumu lake ni kuilea na kuiongoza serikali yake. Nacho chama cha upinzani kwa kawaida hufanya kila njia kuleta picha kwa wananchi kwamba chama tawala kimeshindwa kutawala ili nacho kipewe nafasi ya kutawala.

 

Wakati chama tawala kinataka kuendelea kutawala na hakitaki kinyang’anywe madaraka, chama cha upinzani kinafanya kila kinachoweza kujaribu kukinyang’anya chama tawala madaraka ya kutawala. Hapa ndipo panapotokea mgongano mkubwa unaohatarisha hali ya amani na utulivu nchini.

 

Basi katikati ya mgongano unaojitokeza kati ya chama tawala na chama cha upinzani, unakuta wananchi wengi wanaunga mkono chama cha upinzani, na mara nyingi bila kufikiri. Hii ni kwa sababu chama tawala kinaongoza serikali na kwa kawaida watu hawaipendi serikali.

 

Serikali inawanyang’anya watu fedha yao kwa kuwatoza kodi pia inawafunga. Nani atapenda serikali? Nani atapenda chama tawala kinachoongoza serikali?

 

Kwa hivyo, utakuta kundi kubwa la wananchi hawaipendi serikali na ni mashabiki wa vyama vya upinzani. Ni kundi ambalo wakati wote linaona kwamba serikali haitendi haki. Katikati ya kundi hili wapo wale watu wanaojulikana kama wapiganiaji wa haki za binadamu. Wenyewe hupendelea waitwe “wanaharakati”.

 

Ukitaka kusema kweli karibu wanaharakati wote ni mashabiki wa vyama vya upinzani. Ni kweli wapo wanaharakati wanaofanya kazi nzuri ya kupigania haki za binadamu lakini wengi wao wamepotoka.

 

Kwa jumla mtu anapopigania haki zake au haki za watu wengine anafanya kitendo cha ushujaa. Lakini kitendo hicho kisivuke mipaka. Mashabiki wa upinzani wamevuka mipaka. Wamefungamana na upande wa vyama vya upinzani wakati haki haina upande.

 

Leo wanaharakati wametufikisha mahali ambapo wamewaaminisha wananchi kwamba serikali inafanya vibaya wakati wote na vyama vya upinzani viko sahihi wakati wote. Huu ni upotofu. Tena ni uchochezi.

 

Wanaharakati wa kweli si wachochezi. Lakini wanaharakati tulionao katika Tanzania ya leo karibu wote ni wachochezi. Wamekaa kupambana na serikali wakati wote huku wakiunga mkono upinzani wakati wote. Wengi wao wanachochea uhalifu.

 

Binafsi sijasikia hata siku moja wanaharakati wakikemea vyama vya upinzani. Wamekaa kuikemea serikali tu. Kwa njia hiyo, wanavifanya vyama vya upinzani vione kwamba vinafanya vizuri wakati wote hata pale vinapofanya vibaya. Hii ni hatari.

 

Chukua kwa mfano, wanaharakati ambao miongoni mwao ni wale wanaojiona kwamba ni wasomi waliobobea wametuchanganya. Wamemjia juu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alipovitaka vyombo vya dola visimhurumie mtu yeyote anayedharau serikali.

 

Waziri Mkuu hajasema kwamba vyombo vya dola viwachukulie hatua watiifu wa sheria. Amesema viwachukulie hatua wanaokaidi maagizo ya serikali, wale watu wanaojiona kwamba wapo imara zaidi kuliko serikali.

 

Hata shuleni, Mwalimu Mkuu au mkuu wa shule ana haki ya kuwataka viranja wasiwahurumie wanafunzi wanaodharau maagizo ya shule. Akitokea mwalimu anayedai kuwa waonewe huruma wanafunzi wanaodharau maagizo ya shule, basi huyo si mtetezi wa haki za binadamu. Huyo ni mchochezi.

 

Wanaharakati au wapiganiaji wa haki za binadamu wana wajibu mkubwa katika jamii yetu. Wajibu wao mmojawapo ni kufuatilia nyendo za vyama vya upinzani. Wasifumbie macho vitendo vibaya vya vyama vya upinzani wakisubiri kufumbulia macho vitendo na kauli za serikali.

 

Kwa kifupi mashabiki wa upinzani watibu mapema vitendo vibovu vya upinzani vinavyoweza kusababisha serikali kutoa kauli za kutisha.

 

1366 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!