Mwaka 2004 nilipata fursa ya kuzuru maeneo kadhaa nchini Marekani kwa muda wa takribani mwezi mmoja. Ilikuwa ziara nzuri. Nilijifunza mengi. Wasafiri wanasema kama hujafika Marekani, hujasafiri. Kauli hii inaweza kuwa ya kweli kwa sababu kuna mengi ya kustaajabisha na kutafakarisha – kuanzia kwenye maendeleo hadi tabia zao.

Baada ya kutua katika uwanja wa ndege, nilistaajabu mengi, lakini la kwanza lilikuwa ni lile la kuwaona watumishi wa kila aina wenye asili za kila pembe ya dunia.

 

Nilipoangaza pembeni nilimwona polisi mwenye asili ya Afrika. Nilipofika kwenye dirisha la Uhamiaji nikahudumiwa na Mmarekani mwenye asili ya China. Nilipohitaji kahawa nilihudumiwa na Mmarekani mwenye asili ya Korea. Ndani ya duka la vitabu kuna Wamarekani wenye asili ya Kiarabu!

 

Kwa maneno rahisi, Marekani ni mkusanyiko wa binadamu wenye asili zote wanaopatikana katika sayari hii. Hili ni jambo kubwa sana. Ingawa suala la ubaguzi ni gumu kufutika kabisa, ni mwiko kwa Marekani kufanya vitendo au kutoa kauli zozote za kibaguzi dhidi ya mtu mwingine. Mara kadhaa mtu wa asili moja alipoonewa kutokana na rangi yake, Wamarekani wameungana kupinga jambo hilo.  Watanzania tunapaswa kujifunza mema ya ana hii kutoka Marekani.

 

Nimewasikia wengi wakizungumza juu ya ujio wa Rais Barack Obama hapa nchini mwetu. Wapo viongozi na wananchi wanaoamini kwamba ziara hii itafungua zaidi njia ya kupata misaada! Wanasema baada ya kufanya vizuri kwenye MCC, sasa tuna fursa nyingine ya kuvuna mamilioni ya dola mengine kutoka Marekani. Huko ni kujidanganya.

 

Marekani ni taifa kubwa na lenye nguvu. Ukubwa na ukwasi wake haukupatikana hivi hivi. Mababu na mabibi zetu waliopelekwa utumwani, wana mchango mkubwa sana kwenye uchumi wa taifa hili.

 

Jambo tunalopaswa kulitafakari kwa pamoja ni hili, imekuwaje Marekani ambayo ni taifa changa, liwe na nguvu kubwa za kiuchumi na kijeshi? Kwanini isiwe Uingereza, Ugiriki, Ufaransa, Ujerumani au mengine ya aina hiyo? Kwanini iwe Marekani ambayo ilijitawala mwaka 1776? Je, ni biashara tu ya utumwa iliyolipaisha juu taifa hili? Je, ni sera zake za ubeberu ndizo zilizolinufaisha? Hili ni fumbo muhimu sana tunalopaswa kulifumbua.

 

Tunaweza kuuzungumzia utumwa kama sehemu ya mafanikio ya Marekani. Lakini ni ukweli ulio wazi kwamba yapo mataifa mengine yaliyoshiriki biashara hiyo ambayo uchumi wake ni hohehahe. Mathalani, mataifa ya Kiarabu ambayo yalipokea watumwa, kama si mafuta, pengine leo mambo yangekuwa tofauti kabisa.

 

Hapa tunachoweza kukibaini ni kwamba Wamarekani waliwatumia “vema” watumwa. Walitumia mwanya huo kujiimarisha kwa kilimo cha malighafi za viwandani na wakawa na jeuri ya kusaka masoko ya nje.

 

Siri kubwa kwenye mafanikio ya Marekani ni uchapaji kazi uliopindukia. Marekani waliamini, na wanaendelea kuamini sana katika uchapaji kazi. Sikushangaa kuwaona Wamarekani wakiwa na muda mfupi sana wa kulala, na kuwa na muda mrefu wa kuchapa kazi. Tena basi, miongoni mwa Wamarekani wenyewe ukweli na faida za uchapaji kazi vinaonekana. Ndugu zetu Wamarekani weusi ndiyo wanaoongoza kwenye kundi la masikini. Hawa ni wale walioamua kuendekeza ulevi, uvivu, kukataa elimu, au kubaki wakilalamikia vitendo vya utumwa walivyofanyiwa mababu na mabibi zao.

 

Marekani wameendelea kwa sababu ya uchapaji kazi unaokwenda sambamba na wajibu wa kulitumikia taifa lao. Mmarekani kukwepa kodi ni kosa kubwa sana. Wanaona fahari kulipa kodi. Ni kwa njia hiyo, wameweza kuwa na mapato mengi yaliyofanikisha mipango na huduma mbalimbali za kijamii.

 

Wamarekani wameendelea haraka ndani ya miongo michache kutokana na uzalendo wao. Ni watu wanaolipenda mno taifa lao. Kila Mmarekani anajiona fahari kuwa Mmarekani. Wanaringa kuitwa Wamarekani. Wanalitukuza taifa lao kwa namna zote. Dhamira yao ni kuona taifa lao linakuwa kubwa kiuchumi na kijeshi duniani.

 

Hawana vimelea vya kujisikia au kujiona wanyonge hata pale wanapotambua kuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi kutoka kwa washindani wake, ikiwamo China. Ndiyo maana bingwa wa ngumi nchini Marekani wao wanamtambua kuwa ni bingwa wa dunia! Timu ya mpira wa kikapu inayoshinda taji la NBA, wanaiona ndiyo bingwa wa dunia! Kwao kila jema, zuri na kubwa lipo Marekani.

 

Tamaa hiyo nzuri imewafanya waendelee kuhakikisha wanazidi kuwa watawala, si tu wa dunia, bali wa ulimwengu. Ndiyo maana wameshafika katika mwezi na sasa wanasaka taarifa zitakazowawezesha kujua kama kuna uhai kwenye sayari nyingine.

 

Marekani imekuwa hivyo ilivyo kutokana na pia na ukubwa wake. Ni nchi kubwa iliyotokana na muungano wa hiari na wa lazima wa nchi zaidi ya 50. Wakati sisi Watanzania tukihoji uhalali wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, kuwaunganisha Watanganyika na Wazanzibari, kwa Marekani ni uhaini kuhoji muungano wao! Huwezi kusikia watu wakidai hati za muungano halafu wakaachwa hivi hivi.

 

Tena, heri Muungano wa Tanzania uliotokana na makubaliano ya wawakilishi wa wananchi (marais wawili). Marekani kuna majimbo yaliingizwa kwenye muungano kwa mtutu wa bunduki na mizinga. Waliotakiwa wajiunge, waliposita au walipohoji, walipigwa na wakashurutishwa kuingia kwenye muungano.

 

Leo sisi kama tuliorogwa, hatuoni faida wala raha za kuwa na muungano. Tunajitahidi kwa kila hali kuuvunja, na kwa kasi hii sioni utapona kwa muujiza upi.

 

Ardhi tunaiondoa kwenye mambo ya Muungano ili Mzanzibari atakapotaka kwenda Bara kujenga nyumba, kulima au kufanya lolote linalohitaji ardhi akaribishwe kama mwekezaji! Sijasikia Mmarekani wa kutoka Texas akitakiwa kufanya hivyo anapokwenda Illinois! Mnapoondoa ardhi kwenye muungano, huo si muungano tano.

 

Wamarekani wakiwa ni watu waliojikuta wakiwa kwenye bara ughaibuni, hawakubweteka kusubiri misaada ili waweze kujikwamua kiuchumi na kimaendeleo. Walitambua kuwa kufanya kazi ndiko kungewafanya waheshimiwe na mahasimu wao wa Ulaya.

 

Sisi leo tunajisahau na kutaka kujiaminisha kwamba kwa misaada ya Marekani, Tanzania itabadilika ghafla na kuwa nchi yenye neema kwa kila Mtanzania. Tunajidanganya.

 

Marekani imetoa sababu za ujio wa Rais Obama nchini Tanzania. Imetamka wazi kwamba hii ndiyo nchi rafiki mkubwa miongoni mwa nchi zote za Afrika Mashariki. Sawa, tunaweza kuchekelea kauli hii. Lakini tusisahau kwamba Marekani ilishangaza kwamba haina rafiki wala adui wa kudumu. Maslahi yake ndiyo yanayoamua nani awe rafiki, nani awe adui na kwa wakati gani.

 

Historia inaonesha kuwa Marekani ilishakuwa rafiki mkubwa wa Libya chini ya Muammar Gaddafi. Ilishakuwa rafiki mkubwa wa Saddam Hussein. Kina Jonas Savimbi (Angola) na Mobutu Sese Seko (Zaire) wote walikuwa marafiki zake. Mwisho wa urafiki wao wengi wanaujua.

 

Marekani inapozungumza kwamba Tanzania ndiyo rafiki yake mkubwa katika ukanda huu, ni vema tukaangalia pia kinachoujenga urafiki huo. Huhitaji shahada ya unajimu kutambua kuwa Tanzania ina gesi, ina mafuta, ina urani na madini ya kila aina. Je, nani anaweza kusita kuamini kuwa urafiki wetu unajengwa juu ya matamanio yake ya kunufaishwa na rasilimali hizo?

 

Tunamkaribisha Rais Obama na ujumbe wake. Tusiishie kumwimbia nyimbo na kisha kumwomba misaada zaidi, hasa ya kifedha. Tunapaswa kutafakari sababu zilizotufanya tuwe masikini wa kutupwa ilhali tuna rasilimali zote. Tunafanya kujiuliza na kujiridhisha kama kweli misaada kutoka Marekani na mataifa mengine rafiki ndiyo suluhu ya kuondokana na umaskini huu.

 

Tunapaswa kuiga mambo mazuri yaliyoiwezesha Marekani kuwa hapo ilipo. Kwa mfano, kwenye suala la elimu – hapo ndipo pa kuanzia. Huwezi kuwa na taifa lenye maendeleo bila kuwapa elimu bora watoto. Hatuwezi kuendelea kama hatuwekezi kwenye utafiti na mafunzo, badala ya upuuzi huu wa semina, makongamano na warsha zisizokuwa na mbele wala nyuma. Huwezi kuwa na taifa imara kiuchumi kama wasomi wengi ni wale wa masomo ya sanaa badala ya sayansi. Baba wa Taifa akihutubia kwenye kilele cha Mei Mosi mkoani Mbeya mwaka 1995 alitoa hadhari juu ya utegemezi.

 

Alisema hivi: Tukasema kwamba “Hatuna budi kujenga nchi hii kwa kujitegemea”. Hatuwezi kuwa tunataka maslahi yetu ya Watanzania ya afya bora, maisha bora na elimu nzuri lakini eti tudhani tunaye mjomba huko nje atakuja kutuletea maslahi hayo. HATUNA! Tutajenga nchi hii kwa faida yetu wenyewe sisi wenyewe. Akipatikana mtu kutusaidia, tutamshukuru. Lakini kazi ya kujenga nchi hii kwa manufaa ya Watanzania wote ni kazi ya Watanzania, si kazi ya mtu mwingine. Msimamo huo tukauita Siasa ya Kujitegemea.

Msingi huo umekufa. Hivi mmeshapata mjomba? Hivi kweli mtawadanganya wafanyakazi hawa msiwaambie “chapeni kazi kama mnataka maslahi yenu yaboreshwe, tuchape kazi kwa faida yetu!” Tuache kuwaambia wakulima kwamba “kama tunataka maendeleo, tuchape kazi hivyo hivyo”. Hivi mtawaambia hawa kwamba “tumeshapata mjomba msiwe na wasiwasi!” Mjomba huyo ni nani? Mimi nitafurahi kumwona.

Nitakwenda kumwona, lakini sitamwuliza lo lote. Nitafurahi kumwona. Halafu mkinionesha, “ndiye huyu mjomba”, nitacheeka! Hali ya nchi hii haijabadilika hata kidogo. Tunaweza kujenga nchi kwa maslahi ya Watanzania kwa siasa ya kujitegemea tu, lakini kwa manufaa ya wote. Manufaa ya wote ndicho tulichokiita Ujamaa. Mwisho wa kunukuu.

Mwisho, napenda tuige mazuri ya Marekani. Mawili ambayo napendekeza tuanze nayo, ni UZALENDO kwa Taifa letu na kufanya KAZI kwa juhudi na maarifa kama walivyo wao. Tuwe na nchi ambayo tukiwa popote ndani ya Afrika na duniani kote, tutaona fahari kujitambulisha kwamba tunatoka Tanzania.

By Jamhuri