Sehemu ya kwanza ya makala hii ilitoka katika toleo na. 347. Tangu wakati huo hapakuwa na nafasi kwa makala hii na safu nyingine nyingi kutokana na nafasi zake kuwekwa hotuba za bajeti za wizara mbalimbali. Tunaomba radhi kwa usumbufu huo. Sehemu ya kwanza, mwandishi alitetea hatua ya Mwendesha Mashitaka (DPP) kufuta kesi ya mauaji iliyokuwa ikiwakabili polisi waliotuhumiwa kumuua mwanafunzi Akwilini Akwilina. Sehemu hii ya pili na ya mwisho anafafanua na kutoa mapendekezo kwa Serikali ya nini kifanywe kwa wazazi wa mwanafunzi huyo. ENDELEA…

 

Nilipokuwa shuleni pale St. Mary’s School Tabora mwaka 1950, nilibahatika kuwa mmoja wa makaka (one of the school prefects). Nakumbuka siku moja kulitokea sokomoko shuleni. Basi, makaka wote tukaitwa kwa Padre Mwingereza Fr. Crook (toka Liverpool) “White Father”. Baada ya kutupa “lecture” ndefu juu ya uongozi na namna ya kuzuia sokomoko namna ile lisijetokea tena pale shuleni – alimalizia kwa usemi huu, namnukuu hapa; “Boys remember that “there is no justice under the sun”. The only justice is found in heaven! Is that clear? Tukatoka ofisini mwake kapa kabisa – maana manung’uniko ya wanafunzi hayakujibiwa!

Mimi ningali nakumbuka sana usemi ule. “Duniani hakuna “HAKI” na kwa sababu hiyo mahakamani wanatakiwa watoe hukumu za haki, lakini nako huko wenyewe wanasema kwa lugha ya mahakama; “At least Justice must seen to have been done in a Court of Law” wakimaanisha angalau haki ionekane imetendeka katika mahakama. Mnaona hilo? Akwilina wala familia yake hawakutendewa haki. Kwa kufunga “file” la Akwilina, wazazi wale wamepata mshituko mkubwa.

 

Kilichobaki sisi waandishi wa makala tutumie kalamu zetu kushawishi (solicit) Serikali katika hali kama ile ya risasi yugayuga kumuua mpita njia iweke angalau utaratibu (provision) wa kuwapa wafiwa kifuta machozi.

Ikiwa kwa wakulima, mashamba yao yameharibiwa na wanyama pori – tembo kule Bunda na kwingineko Serikali kwa utaratibu uliopo wanatoa fedha kiasi fulani kwa wakulima (kifuta jasho) kufidia mimea yao iliyoharibiwa na kuwasaidia wasife kwa njaa itakayotokea.

Sasa kwa nini Serikali isitoe KIFUTA MACHOZI kwa familia ya wale waliopoteza maisha yao kwa risasi zisizokusudiwa (stray bullets)? Hapo ndipo tunaweza kusema kama mazao yanafidiwa seuse uhai wa mwanadamu kwa vipi Serikali isitoe kifuta machozi?

 

Mwalimu Nyerere aliwahi kumwambia Kanali Muammar Gaddafi wa Libya baada ya ile Vita ya Kagera maneno haya; “He did not know the price of a human being” maana yake hakujua bei ya binadamu. Hapo dhahiri hakuna kitu kama fidia kwa uhai wa binadamu – ndiyo maana mimi naita kifuta machozi kama vile wakulima wanapewa kupangusa jasho kwa mazao yao yaliyoliwa /kuharibiwa na wanyamapori.

Haifai kuikosoa Serikali na Jeshi la Polisi kwa tukio la namna ile (occurrence of that nature). Jambo la msingi ni kuieleza Serikali ifikirie namna ya kuipoza familia ya marehemu.

Mnakumbuka kule Mirerani, Ijumaa, Aprili 6, 2018 Rais wetu alitoa kifuta jasho kwa Mzee Jumanne Ngoma – yule aliyegundua madini ya tanzanite?

Mzee wa watu amesota sana tangu enzi za Serikali ya Awamu ya Kwanza kwa Baba wa Taifa, akaambulia angalau kumtambua tu kuwa ndiye mgunduzi wa tanzanite, lakini hawakumpa chochote kama kutambua ule ugunduzi wake. Sasa Rais Magufuli siku akipokea ukuta wa Mirerani alitamka hadharani kumtuza (appreciate and acknowledge) Mzee Ngoma kipangusa jasho cha Sh milioni 100.

Kwa kuwa wafiwa ni wazee maskini na wanyonge, sheria haijui hilo; basi, sisi wanadamu tumwombe rais anayewajali maskini na wanyonge atende tendo la huruma katika hali iliyojitokeza hapa. Familia ya binti Akwilina ipewe kifuta machozi. Hilo jamani limo katika uwezo wa kila binadamu. Tunaita “HUMANITARIAN ACT” – ni ubinadamu kupeana pole katika majanga (in calamity like this) kama hili la kuuawa kwa “stray bullet”. Ni tukio la bahati mbaya sana. Halikukusudiwa.

Najua mwandishi wa habari ile katika gazeti la JAMHURI ameonesha uchungu wake mkubwa sana kwa uamuzi wa DPP, lakini afahamu kama alivyohitimisha makala yake ile katika JAMHURI uk. 19 kwa maneno haya: namnukuu “…Je, ningekuwa mimi ndiye nimejibiwa hivi ningejisikiaje?” Katika kufunga makala yake ile alisema, “Bado naamini majibu mepesi aliyotoa DPP ni kwa sababu “hayajamfika haya yaliyowafika wazazi wa Akwilina”. Akaomba Mungu amsamehe maana na yeye (mwandishi wa makala ile) ni mzazi. Anaumia mno kila akijaribu kuvaa hali waliyonayo wazazi wa Akwilina haelewi uamuzi ule wa DPP.

Mimi niulize hapa kuwa laiti mwandishi angekuwa ndiye DPP kwa hali ile iliyotokea na katika mazingira namna ile angaliamuaje? Nashauri sana atafakari usemi wa Bwana Yesu kuwa “msihukumu, msijehukumiwa na ninyi (mat: 7:1) (kwa kilatini, “NOLITE JUDICARE, NE JUDICATI SIETIS”. Tunajua kabisa kuwa hapa DUNIANI HAKUNA HAKI!” Upo usemi wa Kiingereza usemao “WHAT CAN’T BE CURED MUST BE ENDURED” ukimaanisha kuwa “LILE LISILOPONEKA LIVUMILIWE”

Nakumbuka zamani wakati wa Vita Kuu ya Pili – 1945 nilimsikia askari Mwingereza mmoja anasema “it is a CRUEL WORLD” yaani hii dunia i katili.

 

Kumbe yule askari alikuwa rubani wa ndege vita. Basi ndege yale ilidunguliwa na adui, kwa bahati nzuri yeye akachupa kwa parachuti lake akafika ardhini salama. Wakati anasindikizwa nyumbani kwake nako huko akakuta mabomu ya adui yameteketeza mji ule na nyumba yao haikuwapo tena ndipo alisikika akilia kwa sauti ya uchungu sana, “Oh! It is a cruel world!” (ilikuwa mwenye movie ya Vita Kuu ya Pili). Hii nafananisha na mshituko na majonzi ya familia ya Akwilina na mshituko aliopata yule askari. Hapo lazima utalia kumbe dunia hii ni KATILI!

Basi, sisi wanadamu tusiwe wepesi kuona makosa na hivyo kutoa hukumu. Tujaribu sana kutafakari mazingira ambamo tukio limetendeka. Tuombe neema ya Mwenyezi Mungu tujaliwe hekima kama alivyojaliwa Mfalme Suleyman (I Falme sura ile ya 3 mstari wa 9) namna ya kupambanua mema na mabaya ndipo tutaweza kuishi kwa amani na utulivu.

Tusahau yaliyopita, tugange yajayo. Hili la Akwilina tuiachie Serikali, lakini tumuombe Mwenyezi Mungu aijalie kuliona hilo kwa jicho la huruma. Familia hii angalau iweze kufutwa machozi ya kifo cha mpendwa wao Akwilina. Ni tukio gumu kulipokea, halisahauliki, lakini kwa msaada wa neema za Mungu linabebeka! Tumwambie Mungu “Baba” mapenzi yake yatimizwe hapa duniani kama mbinguni. Amen.

1609 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!