Machi 28 mwaka huu, Serikali ya Marekani ilisitisha na kuvunja uhusiano wake na Serikali ya Tanzania katika mambo yote yanayohusu miradi ya mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC) kwa kuondoa dola za Kimarekani milioni 472.8 (zaidi ya shilingi trillion 1 na billion 20).

MCC ilifikia hatua hiyo ya kuinyima misaada Tanzania kutokana na mambo mawili. Kwanza, kutoridhishwa na mwenendo wa uchaguzi wa Zanzibar ambao matokeo yake yalifutwa isivyo halali. Pili, kutoridhishwa na matumizi ya sheria ya mitandao ya 2015 ambayo Marekani inaona ni mbaya kwa sababu inakandamiza uhuru wa wananchi kwa makusudi.

Chama tawala CCM kilitumia nguvu kubwa kupitisha haraka haraka muswada wa sheria hiyo kwa lengo la kuwabana wapinzani wakati wa uchaguzi. Wapinzani wakavamiwa, wakanyang’anywa kompyuta na simu zao kisha wakatiwa hatiani kwa kosa la kukusanya matokeo ya uchaguzi.

Kana kwamba hatua ya Serikali ya Marekani kutunyima misaada haikutosha, siku mbili baadaye mataifa kumi kutoka nchi za Magharibi yalitangaza kwamba yalikuwa yanasitisha ufadhili wao kwenye bajeti ya Serikali ya Tanzania. 

Mataifa hayo kumi ni pamoja na Norway na Sweden, mataifa ambayo yamekuwa washirika wetu wakubwa wa maendeleo tangu enzi za Mwalimu Nyerere. Mbele ya mataifa haya masuala ya demokrasia na utawala bora hayana mzaha.

 Katika tamko lake la kuacha kuisaidia Tanzania, Marekani ilisisitiza kwamba moja ya vigezo vikuu vya kupata fedha za MCC ni nchi mshirika kuwa na rekodi ya kuendesha mambo yake kidemokrasia na hasa kufanya chaguzi huru na za haki ambazo inaonekana Tanzania imeshindwa.

Je, Tanzania imeathirika vipi kwa hatua hii ya kunyimwa misaada? Kwanza, kwa upande wa fedha za MCC, hizo ni fedha zilizokusudiwa kugharamia miradi ya sekta ya umeme nchini na hasa vijijini, pia zingenufaisha wananchi vijijini, lakini vile vile fedha hizo zilikusudiwa kulifanyia mageuzi Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Kwa upande wa fedha tulizonyimwa na mataifa kumi, hizo zilikuwa za kutuongezea nguvu kwenye bajeti ya Serikali ikizingatiwa kuwa misaada ya nchi wahisani hufidia kama asilimia 30 ya bajeti kila mwaka.

Baada ya mataifa hayo kumi kujitoa, hali hiyo imefanya Tanzania kubaki ikitegemea misaada kutoka Jumuiya ya Ulaya (EU), Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) na nchi za Denmark, China, Japan na India.

Je, Tanzania imeonewa katika hatua hii ya kunyimwa misaada? Waziri wa Mambo ya Nje,  Balozi Augustino Mahiga, anakiri kwamba Tanzania imenyimwa misaada kutokana na kupoteza sifa za kupewa msaada huo kwa sababu ya uchaguzi wa Zanzibar na sheria ya makosa ya mitandao.

Pengine hapa cha kusikitisha ni kusikia kauli zinazoonesha kwamba Tanzania haijali kunyimwa misaada eti kwa sababu inaweza kujitegemea! Maskini anapuuza kunyimwa misaada!

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Makamu wake wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, inasema kwamba hakuna mradi utakaosimama kutokana na kunyimwa fedha hizo. Hii ni kusema kwamba hawajali aibu ya kunyimwa misaada. Kuna madai pia kuwa Tanzania haiwezi tena kutegemea misaada yenye masharti.

Hapa ni vyema tukatia maanani sababu halisi iliyofanya tunyimwe misaada. Hatukupewa sharti la kuukubali ushoga ili tupewe misaada. Tumenyimwa misaada kwa sababu ya ubabe wetu. Tumekiuka misingi ya demokrasia kwa kufuta uchaguzi uliokuwa huru na haki na kupitisha sheria iliyokuwa na lengo la kukandamiza upinzani.

Hayo si mambo ya kujivunia wala ya kuonea fahari. Ni mambo yaliyotutia aibu mbele ya mataifa yanayoheshimu misingi ya demokrasia.

Yametolewa madai pia kwamba kitendo cha Tanzania kunyimwa misaada kitaongeza kasi ya Rais Magufuli katika juhudi zake za kutaka Tanzania ijitegemee.

Hakuna asiyeona juhudi za Rais na hakuna anayetaka kumkatisha tamaa. Lakini juhudi zake haziwezi kufanya Tanzania ijitegemee kesho. Kujitegemea ni safari ndefu, na mambo ambayo yangetusaidia kufika haraka kwenye nchi ya kujitegemea hayapo tena.

Tumeua viwanda vilivyoanzishwa na Mwalimu Nyerere kwa lengo la kutusaidia kujitegemea. Tumemaliza madini yetu kwa mikataba mibovu iliyoruhusu wageni kuchukua asilimia 97 ya pato la madini yetu. Tumewakatisha tamaa wakulima wa pamba na korosho kwa kuwalipa malipo yasiyo ya haki. Tumemaliza tembo wetu kwa kuchelewa kuwachukulia hatua majangili. Na deni letu la Taifa halikamatiki.

Kusema kweli, Rais Magufuli ni mtu wa kuhurumiwa. Ameshika nchi wakati mbaya, tumwombee kwa Mungu amsaidie kutimiza malengo yake.

By Jamhuri