Hifadhi ya Taifa Serengeti, iliyowavuta maelfu kwa maelfu ya wageni kutoka ndani na nje ya nchi yetu, inakufa.

Tofauti na wengi wanavyodhani, athari za ujangili Serengeti si kubwa wala tishio kwa uhai wake, isipokuwa kinachoiua Serengeti ni siasa na wanasiasa!

Ufugaji, kilimo, ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa; pamoja na shughuli nyingine za kibinadamu, ndiyo maradhi yaliyoandaliwa kuitoa Serengeti uhai.

Wakoloni, pamoja na madhila mengi waliyowafanyia Watanzania na Waafrika kwa jumla, bado walikuwa waungwana kwa kulinda rasilimali za asili, ikiwamo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Tofauti na wao, Watanzania waliodai kujitawala ili wafaidi heshima, utu na rasilimali za nchi yao, sasa wamegeuka kuwa chanzo kikuu cha kuua urithi huu.

Ni kwa namna gani wanasiasa wanaiua Serengeti? Rejea kelele nyingi zilizopigwa na baadhi ya wabunge wakati wa Operesheni Tokomeza. Walipaza sauti wakilaani kuuawa kwa mamia ya ng’ombe! Kelele zile hazikulenga kuwahurumi, isipokuwa kulaani mauaji ya mifugo yao (ng’ombe, mbuzi na kondoo) waliyowekeza kwa watu wengine.

Hivi karibuni nilizuru maeneo kadhaa ndani na nje ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kujionea hali ya mambo. Itoshe kusema hali ni mbaya. Uhifadhi unatoweka. Serengeti inaelekea kubaki uwanda usiokuwa na wanyamapori, ndege, miti na viumbe hai wengine!

Wabunge, wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa, wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo, madiwani na kila aliye na uwezo wa kununua ng’ombe, wanafanya hivyo wakijua malisho (Serengeti) yapo.

Mhifadhi Mkuu wa Serengeti, William Mwakilema, anasema: “Kuanzia Bunda, Bariadi, Maswa hadi Meatu hali ni mbaya. Wakulima wanalima hadi kwenye mpaka wa hifadhi. Kuanzia Handajega hadi Maswa mifugo imejaa hifadhini, si kwa sababu wana shida hivyo ya kuingiza mifugo hifadhini, bali kwa sababu ya kiburi na kutothamini uhifadhi. Tunajitahidi sana, lakini wakati mwingine upungufu wa watumishi na kuingiliwa na wanasiasa kwenye masuala ya uhifadhi kunatukwaza sana.

“Maelfu ya mifugo imeingizwa ndani ya Hifadhi hii, na sasa wanyamapori wamekimbia. Ng’ombe, mbuzi na kondoo wamefungwa kengele shingoni ambazo zinasababisha kelele- zinazowafanya wanyamapori wakimbie. Wanaingiza mbwa ambao wanafanya kazi ya kuwafukuza na kuwakamata wanyamapori. Kwa hali hiyo huwezi kupata mnyama,” anasema Mwakilema.

Katika Kata za Masewa na Matongo, Bariadi mkoani Simiyu, mifugo yote inaingizwa katika Hifadhi ya Taifa Serengeti, huku wahusika wakionekana kutokuwa na wasiwasi wowote.

“Huwa tunaibia mara moja moja maana lazima tuseme ukweli kwa sababu hata nyayo unaziona, tukikamatwa faini kwa ng’ombe mmoja tunalipa Sh 10,000,” anasema Doto Ngage (46), aliye katika Kitongoji cha Ighabaniko Senta, Kijiji cha Masewa.

Ngage, anakiri kuwa ng’ombe anachunga si wake, bali ni wa ‘tajiri’ wake aliyemtaja kwa jina la Sayi Kimbulu.

“Tunaingia Serengeti kwa sababu kuna nyasi nzuri na nyingi,” anasema.

Kijana Suguda Sayi (18), anasema alihitimu darasa la saba mwaka 2013 katika Shule ya Msingi Masewa. Tangu wakati huo ameajiriwa kuchunga ng’ombe 58 akisaidiana na Gingiri Mange (17).

Mwezi uliopita Diwani wa Matongo, Badu Tuyi (CCM), aliingia kwenye mgogoro na wananchi wa Matongo baada ya ng’ombe wake kula shamba la mahindi la wanakijiji.

Ingawa ng’ombe ni wake, lakini anakataa na kusema si wake, bali ni wa mtu aliyemtaja kwa jina la Emanuel.

Diwani Tuyi ni kielelezo cha namna viongozi wengi wa kisiasa, wa umma na wafanyabiashara walivyo na mifugo mingi inayohatarisha uhai wa Hifadhi ya Serengeti.

‘Buffer zone’ ambalo ni eneo linalopaswa kutengwa kwa mita 500 kutoka eneo la ardhi ya wanavijiji na Hifadhi ya Serengeti, lote; ama limelimwa, limejengwa mazizi ya mifugo, au limejengwa nyumba.

Diwani Tuyi anasema: “Serikali iliyopita ilijisahau kuwapa wananchi mipaka. Ilipaswa wananchi waambiwe mwisho wao ni mita 500 kutoka kwenye mpaka wa Hifadhi, lakini hilo halikufanyika.”

Ingawa anasema hivyo, uongozi wa Hifadhi ya Serengeti umeweka vigingi vya mpaka vinavyoonekana hata kwa umbali mrefu.

Lakini sheria haisemi lolote kuhusu eneo la ‘buffer zone’-kwamba linapaswa kuachwa wazi au kuendelezwa kwa shughuli nyingine za kibinadamu.

Diwani Tuyi, licha ya ng’ombe kuonekana wakiwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, bado aliendelea kushikilia msimamo wake wa ‘ubishi’ wa kwamba hakuna mifugo katika Hifadhi hiyo.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ighabanilo, Dutu Sumbuka (Chadema), anasema kuna taarifa za baadhi ya watu wanaoingiza mifugo ndani ya Hifadhi ya Serengeti kuwalipa fedha askari.

Kuhusu ‘buffer zone’, anasema: “Hilo hatukulijua, tunatarajia sasa madiwani wetu watuelimishe; mimi binafsi sijawahi kushirikishwa.”

Anasema maombi ya kupatiwa ardhi ya malisho wameyawasilisha kwa madiwani wao ili waone namna watakavyosaidiwa.

Kuhusu tembo wanaoharibu mazao yao, anasema: “Tunamuomba Rais Magufuli, afanye utaratibu wasije mashambani mwetu.”

 

Hali ya uhifadhi

 

Hali ya uhifadhi ni mbaya katika Kijiji cha Matongo kwani wananchi, licha ya kulima hadi ndani ya Hifadhi, njia za mifugo yao inayoingia na kutoka ndani ya Hifadhi hiyo ni jambo linaloashiria kutoweka kwa Serengeti.

Mashamba ya mpunga, mahindi, mtama na mengine yamelimwa na kuzifanya nguzo ambazo ni mpaka kati ya hifadhi na vijiji, ziwe katikati ya mashamba hayo.

Mhifadhi Idara ya Ujirani Mwema (SENAPA), Nuhu Daniel, anasema hali ni mbaya kutokana na wananchi wengi kuingiza mifugo ndani.

“Mifugo ni mingi, wananchi wanaingiza si kwa sababu hawajui, ila kwa sababu wakati mwingine wanapata utetezi kutoka kwa viongozi hasa wa kisiasa ambao mara zote wametumia kigezo cha ‘kuwatetea wananchi (wapigakura) wao’,” anasema.

Anaongeza: “Hali ni mbaya zaidi vijiji vya Matongo, Senta, Ighabanilo hadi Maswa. Hifadhi imevamiwa kweli kweli, wanyama wanakimbia. Hali hii isipodhibitiwa mapema mambo yatakuwa mabaya zaidi kwa sababu hawa wavamizi si tu kwamba wanaingiza mifugo, lakini wanakata miti kwa shughuli za kibinadamu na hata kuchoma mkaa.

“Nje ya hifadhi wameharibu vyanzo vya maji na malisho ya mifugo, sasa wanaona pona yao pekee ni ya kuingia hifadhini. Kuna umuhimu wa kuwa na sheria ya kuwafanya wananchi wamiliki kiasi fulani cha mifugo yenye tija kwao, na si kuwa na mifugo mingi ambayo inaharibu uhifadhi.”

Msaidizi Mhifadhi Ujirani Mwema (SENAPA), Joyce Mungule, anasema hali ilivyo sasa kwa hifadhi-tishio si ujangili, bali ni wanasiasa ambao wako radhi kuona wananchi wakiendesha shughuli za kibinadamu ndani ya Hifadhi.

Alipoulizwa kama mifugo mingi ni ya viongozi, Joyce alisema: “Hilo linasemwa, hatuna orodha ya wanaomiliki mifugo, lakini wakati mwingine nguvu ya utetezi inayoonekana inakufanya uamini kuwa kuna wakubwa maana wananchi wanajua mipaka na wanapoona askari wa hifadhi huwa wanakimbia kujificha.

“Huko kukimbia ni ishara kwamba wanatambua wanafanya kosa kuingiza mifugo hifadhini. Kunatakiwa kazi kubwa ya kuelimisha wananchi ili wajue faida za uhifadhi. Sisi tunaendelea na juhudi za kuwaelimisha na kuwashirikisha kwenye uhifadhi, lakini hali kwa kweli si nzuri. Mifugo ni mingi mno.”

Pori la Akiba la Kijeleshi, ni sehemu ya ikolojia ya Serengeti. Kwa sasa Pori hilo limekimbiwa na wanyamapori kutokana na kuwapo maelfu kwa maelfu ya mifugo.

Mapema mwaka huu, maelfu ya ng’ombe walikamatwa, lakini ikatolewa amri kutoka juu serikalini waachiwe. Hatua hiyo ya serikali ikawa chachu ya kuwafanya wafugaji wengi zaidi waingize mifugo katika Pori hilo lenye mandhari ya pekee.

Katika kufuatilia hatima ya Pori hilo, JAMHURI imeshuhudia mbwa wakikosa wanyama kwa mlo, hivyo kulazimika kuwaua mbuzi na kondoo. Baadhi ya picha zinathibitisha hali hiyo ya kusikitisha.

 

Nini kifanyike?

Yapo mambo mengi yanayopaswa kufanywa ili kuinusuru Serengeti, hifadhi nyingine pamoja na mapori mbalimbali nchini.

Mosi, sheria za nchi hazina budi kuheshimiwa. Viongozi na wananchi wote kwa pamoja wazisimamie na wazitekeleze.

Pili, wakati umefika sasa wa kuwa na ufugaji wenye tija. Haiwezekani Tanzania iwe nchi ya pili kwa kuwa na mifugo mingi katika Afrika, lakini ikawa ya mwisho kupata mchango wa rasilimali hiyo kwenye Pato la Taifa (GDP). Wafugaji wafuge mifugo michache, itunzwe kisasa na iwape tija.

Tatu, wakati umefika kwa kila mkulima na mfugaji kuwa na eneo lake kisheria. Huu utaratibu wa mkulima au mfugaji kulima au kufunga kokote anakotaka, ukomeshwe. Ardhi zipimwe na zitengwe kulingana na mahitaji ya wananchi na vijiji husika.

Nne, tuutambue utalii kama chanzo muhimu kabisa katika mapato ya nchi yetu. Ili hilo liwezekane, hatuna budi kutambua kuwa utalii unawezekana tu kwa kuwa na hifadhi na mapori yaliyotunzwa kwa uasili wake na kwa maana hiyo yaweze kutunza wanyama, ndege, miti na vyanzo vya maji.

Tano, viongozi wenye maelfu ya mifugo ambao kuna ushahidi wa wazi kuwa ndiyo wanaochochea uvamizi katika hifadhi na mapori nchini mwetu, sharti washughulikiwe kimaadili. Mifugo yao ikitaifishwa, wananchi wengine wa kawaida wataogopa na hivyo kuheshimu mipaka ya uhifadhi.

Sita, siasa iwekwe mbali kabisa na uhifadhi. Mwanasiasa anayeomba nafasi kwa ahadi ya kumega maeneo ya hifadhi kuwapa wananchi wake, awekwe kwenye kundi la watu wasiofaa kuwa viongozi.

Saba, sera na sheria zetu zinazotawala maeneo yote ya hifadhi nchini vibadilishwe ili kama kuna maeneo ambayo yanaonekana yanaweza kubadilishwa matumizi, yafanywe hivyo. Maeneo yanayoweza kuwa Mapori Tengefu au Mapori ya Akiba, yafanywe hivyo mapema.

Nane, iwe dhima ya kila Mtanzania kuwa mstari wa mbele kuyalinda na kuyahifadhi maeneo yote ya uhifadhi katika nchi yetu kwa kutambua kuwa urithi huu unapaswa kuwa endelevu.

Tisa, hatuna budi kutambua ukweli kwamba hata kama Serengeti yote watapewa wafugaji, bado haitatosha. Hii ina maana hakuna siku eneo la ufugaji au kilimo litatosha, hasa katika mazingira haya ya kuhamahama. Lililo la muhimu ni la kutumia eneo dogo kisasa ili liwe na tija kwa ufugaji na kilimo.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, amesema ni wajibu wa viongozi na wananchi wote katika mkoa huo kuhakikisha Serengeti na mapori mengine vinalindwa na kudumu kwa maslahi ya Taifa zima.

“Hilo la mifugo tumeshalizungumza, na kuahidi kuwa hatua za kuinusuru Serengeti kwa upande wetu zitachukuliwa mapema iwezekanavyo,” amesema.

Wizara ya Maliasili na Utalii imepata viongozi makini. Hasisubiri kuandikwa vibaya kwenye vitabu vya kumbukumbu kwamba wakati wao walikaa kimya hata Serengeti ikatoweka. Uwezo wa kuiokoa Serengeti tunao. Kwa umoja wetu tuinusuru lulu hii ya Tanzania, Afrika na dunia.

By Jamhuri