Watanzania tumepata mshituko. Tumeshangazwa na mwenendo wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tumeshangazwa na jinsi siasa zilivyoanza kugeuzwa uadui. Tumeshangazwa na jinsi wabunge walivyoanza kupoteza heshima na kushindwa kujitambua.

Kwa mwenendo uliopo bungeni sasa, tunasubiri kitu kimoja tu – ambacho hakijafikiwa; kupigana ngumi. Wiki iliyopita, kama si busara za Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, kumtoa Tundu Lissu ukumbini, wabunge vijana walikuwa tayari kurusha ngumi.


Hatua ya wabunge hawa kusimama kumzingira Lissu wakisema hatolewi nje, ina maana walikuwa tayari kupambana na askari. Haishangazi pengine askari iwapo wangezidiwa nguvu, wangerusha mabomu ya machozi ndani ya Ukumbi wa Bunge, na kama yasingefanya kazi wangerusha risasi za moto.


Waheshimiwa wabunge wala msidhani tunatia chumvi, huko ndiko tunakoelekea. Mwenendo unaooneshwa na Kiti cha Spika na wabunge kwa kambi zote – Chama Cha Mapinduzi (CCM) na upinzani, hauridhishi. Kiti cha Spika ndiyo chimbuko za vurugu hizi.

Tunakumbuka enzi za Spika wa Kwanza, Chifu Adam Sapi Mkwawa, na Spika wa Pili, Pius Msekwa, wabunge walivyokuwa na adabu. Enzi za maspika hawa, mbunge asingethubutu kusema “siongei na mbwa naongea na mfuga mbwa.”  Muktadha wa lugha hii haukubaliki bungeni.


Kwanza wabunge walikuwa na hofu kwa maspika hawa, na maspika hawa walikuwa na hofu kutotenda haki. Sasa hivi Kiti cha Spika kinavunja kanuni kinazozitunga chenyewe bila hofu. Spika anasema mbunge atakayetukana atamtoa ukumbini, siku mbili baadaye mbunge wa CCM anatukana hatolewi.


Heshima ya Bunge ilianza kuharibika wakati Samuel Sitta alipochaguliwa kuwa Spika. Sitta aliingia bungeni kama “kocha mchezaji”. Serikali ikamwona kama msaliti na kama mwakilishi wa vyama vya upinzani. Sitta aliacha kazi ya urefarii, akawa anafunga mabao ya mkono.


CCM hawakumchelewesha. Vijana wa mjini wanasema “wakamla kichwa.” Wakaweka sifa ambayo hata angekwenda mbinguni na kurejea duniani asingeipata. Wakasema zamu hii Spika ni mwanamke. Sifa hii Sitta angeipata kwa operesheni maalum tu, vinginevyo haiwezekani.


Anne Makinda alivyoingia madarakani, moyoni akabaini kuwa Sitta kaondolewa kwa kupendelea wapinzani na kusababisha mpasuko ndani ya CCM, kwa kuwagawa katika makundi ya mafisadi na mitume 12. Bila shaka akaona huu ni wakati wake kuonekana kuwa ni mtoto mzuri. Aitetee CCM.


Kwa maana hiyo, akayumbisha mwanzi. Akabadili upepo kwelikweli na kuona wapinzani ni sumu ya yeye kuendelea kuwa Spika. Akabuni mbinu ya kuwanyamazisha na kuwakalisha chini. Akabuni mbinu ya kuwaminya kama mbu kwenye chandarua. Wapinzani wakachukia. Wamemgeukia.


Sisi tunasema, tulipofika sasa panatosha. Kiti cha Spika kikiendelea na mchezo wa kuhamisha milingoti ya magoli wakati mpira unaendelea, kitazaa umwagaji damu hapa nchini. Hatutaki tuelekee huko. Spika asimamie kanuni kwa usawa. Ukisema atakayetukana atatolewa ukumbini, hata kama ni wa CCM atolewe.


Ikiwa wapinzani wanatoa lugha zenye ukakasi unawakemea, basi hata wa CCM wakifanya hivyo usisubiri wapinzani waombe mwongozo wa kiti chako. Tusipochukua hatua sasa tutafunga zizi wakati ng’ombe wote wamekwishatoroshwa. Tunasema vurugu hapana. Spika tenda haki na wabunge rejesheni heshima tuliyowapa mpingane bila kupigana.

Mungu ibariki Tanzania.


By Jamhuri