Nchi yetu inapitia wakati mgumu. Udini umetamalaki kila kona. Zanzibar wanasema yao. Kanda ya Ziwa ndiyo usiseme. Mgogoro wa kuchinja umeibua mapya. Tayari Wakristo wana bucha zao, na hata wasio na bucha wanakusanyana wananunua ng’ombe wanachinja na kuuziana nyama kienyeji.

Ukiacha udini, kuna migawanyiko ya wazi katika jamii yetu. Watu hawaogopi tena kuvunja sheria. Wakihisi haki yao imecheleweshwa wako tayari kuchoma moto vituo vya polisi au nyumba za viongozi wa chama tawala. Mauaji na kutekana vimejaa kila kona, kama ilivyotokea huko Karagwe na Geita.

Serikali hatuoni ikifanya kazi ya ziada kukabiliana na hali hii. Mpasuko unazidi kuwa mkubwa, lakini hakuna sheria au sera inayotungwa na Serikali yetu kudhibiti hali hii. Mwalimu Julius Nyerere alipambana kwelikweli na udini kulifikisha Taifa hapa tunakotoka kuelekea kuzimu.

 

Katika hotuba zake kwa Taifa hili, alilizungumzia suala la udini kwa ukali wa ajabu. Hakuwa akiuma midomo. Yeyote aliyethibitika kuchochea udini alikamatwa na kufunguliwa mashitaka papo hapo. Wengine walikabidhiwa vifungo vya ndani, na wengine walihamishwa mikoa na wilaya.

 

Nyerere alitaifisha seminari za Wakristo baada ya Uhuru na kuzifanya shule za kitaifa. Leo kila kona kuna shule za seminari za Wakristo na Waislamu. Tunajenga vyuo vikuu vya kidini. Tena kwa mbwembwe kabisa tunatangaza hivi ni vyuo vya Wakatoliki, Walutheli na Waislamu.

 

Tumefika mahala shuleni Wakristo wanadai kuvaa rozari na Waislamu wanadai kuvaa hijabu. Ukienda kwenye nyumba za wageni au polisi unaulizwa maswali ya kijinga kabisa. Unatakiwa kueleza kabila lako ni lipi. Tena wengine wanauliza hata dini yako ni ipi.

 

Hivi kabila au dini ina uhusiano gani na mtu kulala kwenye nyumba ya wageni au kumfungulia mashitaka polisi? Watu wanakwenda makanisani na misikitini wanatukana dini nyingine na wanaachwa tu. Kimsingi, tunakoelekea siko. Kama Taifa tumepotea njia.

 

Hatupaswi kuendelea na matamko ya kuchekacheka. Tunapaswa kupiga marufuku kuanzia sasa suala la dini na kabila kama ilivyokuwa katika Sensa ya Watu na Makazi 2012.

 

Tunachohitaji ni kuhudumia Watanzania na si kujua dini zao. Kwa anayetaka kujua dini aende kanisani au misikitini.

 

Kama Taifa tupige marufuku udini katika elimu, ukabila katika huduma za jamii, na yeyote atakayetaka kutupeleka huko tuwe tayari hata kumhukumu adhabu ya kifo. Bila kuwa wakali, Taifa linatukatikia mikononi. Viongozi amkeni, semeni UDINI na UKABILA hapana kwa Tanzania. Mungu ibariki Tanzania.

 

 

Please follow and like us:
Pin Share