Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira imetaka bayana kwamba ujangili ni janga la kitaifa. Hatuhitaji mtaalamu wa utabiri aje kutoa kauli nyingine tofauti na hiyo.

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) umeonesha kuwa tembo wasiopungua 30 wanauawa kwa siku, tembo 850 wanauawa kwa mwezi, na hiyo ina maana kwamba mwaka mwaka mmoja, na kwa kasi hii hii, tembo 10,000 wanauawa.

 

Kutokana na kasi kubwa ya kuuawa kwa tembo, taarifa za kitaalamu kutokana TAWIRI zinathibitisha kwamba idadi ya tembo imepungua kutoka 109,000 mwaka 2009 hadi tembo chini ya 70,000 mwaka jana.

 

Kamati imebainisha wazi kwamba endapo kasi hii ya ujangili wa tembo itaendelea bila kudhibitiwa haraka, ni wazi kuwa tembo watakuwa wametoweka nchini katika kipindi cha miaka saba ijayo.

 

Hizi ni habari za kusikitisha. Lakini ni ukweli ulio wazi kwamba hii si mara ya kwanza kwa Taifa letu kukumbwa na dhahama hii ya ujangili. Katika miaka ya 1980, ujangili ulishamiri, lakini Serikali haikuweza kulala. Iliendesha Operesheni Uhai iliyoweza kuwatokomeza majangili.

 

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) hapa ndipo mahali pake. Bado tunakumbuka kazi kubwa na ya kutukuka iliyofanywa na Jeshi hilo kwa majangili wa Kisomali katika eneo la Ngorongoro. Rais Jakaya Kikwete ameshaitaka Wizara ya Maliasili na Utalii imweleze aina ya msaada inayouhitaji ili kukabiliana na majangili. Hatudhani kama mamlaka husika hazijaona umuhimu wa kuomba msaada huo.

 

Vita dhidi ya ujangili na majangili ni yetu sote. Tunapaswa kuishiriki bila kutegeana. Hii si kazi ya Wizara, TANAPA au Mamlaka ya Ngorongoro pekee. Majangili tunaishi nao. Tunawajua. Tena, basi, hakuna sababu kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania kuzuia silaha zilizoagizwa na Wizara ya Maliasili na Utalii. Tunatoa misamaha mingi ya kodi isiyokuwa na tija kwa Taifa. Hatuoni ni kitu gani kinakwaza utoaji silaha hizi ambazo zinapelekwa kudhibiti rasilimali za nchi.

 

Kwetu sisi tunaamini kwamba wakati umeshawadia wa kuwa na adhabu kali kwa majangili, ikibidi hata adhabu ya kifo! Uhujumu uchumi unastahili adhabu kali. Kuwachekea majangili ni kuchekea matatizo. Tunaua uchumi. Tunapoteza hazina muhimu kwa vizazi vijavyo.Serikali pia inapaswa irekebishe sheria, zikiwamo zinazolazimu vyombo kama TANAPA au Mamlaka ya Ngorongoro kukusanya fedha, kuzipeleka Hazina, kisha kusubiri mgawo kwa ajili ya kuendeshea mambo mbalimbali. Adha za aumuzi huu ni kwa vyombo hivyo kushindwa kuajiri askari wa kutosha ili kukabiliana na wimbi la ujangili.

 

Mwisho, tunarejea wito wetu kwa wananchi wote wa Tanzania , bila kujali tofauti zetu za kiitikadi, kuungana pamoja kupambana na ujangili na majangili. Dhima hii si ya Serikali au wahifadhi pekee. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha anaona uchungu kwa rasilimali za Taifa na kuchukua hatua za kudhibiti hali hii. Tuazimie kuwa na hitimisho la ujangili na majangili.

 

Please follow and like us:
Pin Share