Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi, wiki iliyopita amelitangazia Bunge uamuzi mgumu wa Serikali. Ametangaza kuwa Serikali sasa imeamua kufuta matokeo ya mtihani wa kidato cha nne wa 2012. Katika mtihani huo wanafunzi asilimia 65.5 walipata daraja sifuri.

Idadi ya wanafunzi waliofanya mitihani ni 367,756. Kati ya hao asilimia 6.4 tu sawa na wanafunzi 23,520 walipata daraja la kwanza hadi la tatu na 103,327 walipata daraja la nne. Waliosalia 240,909 wamepata daraja sifuri. Haya ndiyo matokeo iliyoyafuta Serikali.

 

Serikali imefuta matokeo haya kutokana na uchunguzi uliofanywa na Tume iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kubaini kuwa mfumo wa kukokotoa alama za wanafunzi umebadilishwa bila wanafunzi, walimu au wadau wengine kupewa taarifa.

 

Itakumbukwa kuwa mwaka juzi, Waislamu nchini walilalamika na kuandamana wakidai kuwa vijana wao walikuwa wamefelishwa somo la Islamic Knowledge, baadaye matokeo yao yakarekebishwa kwa maelezo kuwa mfumo uliotumika ulikuwa mpya. Ushindi uliongezeka.

 

Inawezekana Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania amejisahau. Baada ya kumaliza timbwili hilo, akaona sasa ngoja afanye majaribio kwa Taifa zima. Amefanikiwa alichokitaka. Watoto wameshindwa wakachanganyikiwa, hadi wengine wamejinyonga.

 

Zipo taarifa zinazodai kuwa Ndalichako hawezi kufikia uamuzi mkubwa kiasi hiki peke yake, kwamba huenda Waziri wa Elimu na Mfunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, anajua kinachoendelea. Lakini sisi tunasema katika hili lazima uwajibikaji uanzie kwa Ndalichako.

 

Ukaidi wake haujaanzia kwenye mitihani pekee. Leo Mtanzania yeyote akipoteza cheti cha kidato cha IV au cha VI, hata kama kimeungulia kwenye nyumba utaratibu wa zamani wa kupewa nakala halisi ameufuta. Anasema unalipia Sh 10,000 matokeo yanapelekwa unakoomba kazi au shule. Huu ni utaratibu mbovu kabisa.

 

Tutawashangaa wabunge wakati wa bajeti ya Wizara ya Elimu na Mfunzo ya Ufundi wakipitisha bajeti ya mwaka huu, bila kwanza kumbana Ndalichako aliyelitia Taifa hasara na aibu ya aina yake akawajibika. Tunasema Baraza la Mitihani bila Ndalichako linawezekana. Waziri Mkuu mfukuze Ndalichako elimu inusurike nchini.

Please follow and like us:
Pin Share